Mbinu za kujiongezea thamani kazini

Picha na Citizen Tv

Muktasari:

Ndani ya mashirika binafsi na serikalini, wapo watu waliofanya kazi kwa muda mrefu, lakini kufanya kazi kwa kipindi kirefu hakusaidii kama huendi na mabadiliko ya nyakati.

Kupata kazi ni jambo la kwanza lakini muhimu ni namna unavyoweza kuilinda ajira yako.

Ndani ya mashirika binafsi na serikalini, wapo watu waliofanya kazi kwa muda mrefu, lakini kufanya kazi kwa kipindi kirefu hakusaidii kama huendi na mabadiliko ya nyakati.

Vijana wapya wanaingia kwenye soko la ajira wanakuwa na thamani kubwa, kwa sababu wanaingia kazini wakiwa ni rasilimali inayotosheleza mahitaji ya wakati. Mtu ambaye alikuwa kazini zaidi ya miaka 20 anaonekana si mali kitu.

Kwa nini ufike wakati uonekane una thamani ndogo kwenye kazi ambayo umekuwa ukiitumikia kwa miaka mingi na unaiweza? Kwa nini vijana wadogo wageuke rasilimali ghali kwenye kazi ambayo wewe umeifanya kwa miaka mingi?

Haiwezi kukuvutia hata kidogo, kijana ambaye wakati wewe ulipokuwa unaanza kazi na kusifiwa na viongozi wako kutokana na uwezo wako, yeye hakuwa ameanza hata shule.

Utaumia kupewa kijana sawa na mwanao au mdogo wako wa mbali awe kiongozi wako, huku mshahara wake ukiwa mkubwa hata kuzidi mara tatu wa ule wa kwako. Lakini huyu anabebwa na thamani aliyoingia nayo kazini. Wewe ni rasilimali inayoshuka thamani kwa kasi.

Hivyo basi, zingatia mambo matatu; mosi ni kupata kazi, pili kuilinda hiyo kazi yako, tatu na muhimu zaidi ni kuhakikisha unajiongezea thamani ukiwa kazini. Unapoweza kujiongezea thamani kazini unapata faida mbili, kuilinda ajira na kuendelea kuwa rasilimali muhimu ofisini kwako.

Zipo mbinu tatu ambazo ukizitumia vizuri utaitetea thamani yako kazini kila wakati. Na ukiwa na thamani kazini kwako hutakuwa na wasiwasi wa kushushwa cheo wala kuondolewa kazini.

Nenda na wakati

Katika eneo la kazi yako kuna mabadiliko gani? Tupo kwenye ulimwengu wa teknolojia, wagunduzi wanaingiza ugunduzi mpya kila kukicha. Unatakiwa kufungua macho na masikio kuhusu taaluma yako.

Haitakiwi watu wa idara nyingine wajue kuwa sasa hivi kuna ugunduzi mpya wa namna ya ufanyaji kazi katika idara yako, wakati wewe mwenyewe huna habari. Utaonekana huendi na wakati. Siku zote wakati ndiyo hushusha au kupandisha thamani ya mfanyakazi.

Mathalan wewe ni mhasibu na siku zote unatumia programu ya Microsoft Excel kuweka sawa mahesabu yako na takwimu za kiofisi kuhusiana na masuala yote ya kifedha. Hupaswi kubaki nyuma kufahamu kuwa kuna programu toleo la mwaka 2016 (v16.0).

Huo ni mfano tu. Inatakiwa kila mmoja kwa nafasi yake aonekane anakwenda na wakati. Ukiwa mkusanya kodi, unapaswa kufahamu njia mbalimbali mpya ambazo wakwepa kodi huzitumia.

Umeajiriwa kwenye kampuni ya kudai madeni, kwa hiyo unatakiwa ujitume kutafuta maarifa mapya ambayo wadaiwa sugu hutumia ili kuendelea kutolipa madeni wanayodaiwa.

Eneo la kwenda na wakati lina maana ya kuwa na maarifa mapya yenye kwenda na wakati. Unapaswa kujua dunia inavyokwenda kuhusiana na kazi yako. Unatakiwa uwe mfuatiliaji.

Kama wewe ni msanifu kurasa katika magazeti, vitabu, majarida na kadhalika na unatumia programu ya Adobe InDesign, unatakiwa uwe na taarifa kuwa kuna toleo jipya la Novemba 2, mwaka huu la CC 2017.

Hata kama ni mwajiriwa katika kampuni ya ulinzi, unahitaji kufahamu mbinu mpya ambazo wezi wanazitumia kuiba.

Jitahidi kujifunza

Ukishajua mambo mapya kuhusiana na kazi yako anza kujisomea. Unaweza kwenda darasani au kujisomea wewe mwenyewe kupitia vitabu na mitandao. Maarifa utakayoyapata hakikisha unayaingiza kazini kwako ili uonyeshe tofauti.

Viongozi wako watakuheshimu zaidi kutokana na maarifa mapya ambayo unayaingiza kazini kwako kila wakati. Wataingia vijana wapya kutoka vyuoni lakini wanachoingia nacho tayari unacho na baada ya muda unawapita kwa kasi kutokana na tabia yako ya kupenda kujifunza.

Tupo kwenye ulimwengu ambao watu wanaamini zaidi vyeti kuliko maarifa ndani ya kichwa. Kwa maana hiyo unapopata nafasi ya kurejea darasani ili uwe na cheti chenye kuonekana, utakuwa unajiongezea thamani thamani kubwa zaidi.

Amua kuwa mtu wa kutafuta maarifa mapya na kuyaingiza kichwani kwako. Hilo siyo tu litakusaidia kukuongezea thamani kazini kwako, bali pia hata taasisi nyingine ni rahisi kukumulika na kutamani kufanya kazi na wewe kama rasilimali ya wakati mwafaka.

Kuwa mbunifu

Hakikisha huzoeleki kazini kwa namna unavyofanya kazi zako. Ukiwepo na usipokuwepo lazima tofauti yako ionekane. Si kwa sababu ya kuficha maarifa yako ili wenzako wasiyatumie, hapana. Ni kutokana na ubunifu ambao unakuwa nao kila siku katika utendaji wako.

KIla unapotoka kazini, unarejea nyumbani na kulala. Usiku unaamua kujinyima hata dakika chache kuifikiria kazi yako hasa jinsi ya kuifanya tofauti.

Ukiwa mbunifu unaweza kufanya kazi kwa muda mrefu bila kuchokwa. Na kila mara utafikiriwa kuongezewa maslahi kwa sababu unahitajika zaidi.

Kwa kawaida wafanyakazi wabunifu thamani yao huwa juu. Pale taasisi inapofikiria kupunguza wafanyakazi ili kuondokana na mzigo wa uendeshaji, mfanyakazi mbunifu hubaki kutokana na umuhimu wake kimaarifa.

Luqman Maloto ni mmiliki wa tovuti ya Maandishi Genius www.luqmanmaloto.com