Mbinu za kukabiliana na utoro shuleni Bungo

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bungo iliyopo Manispaa ya Morogoro, Roman Luoga, akiwasaidia wanafunzi wake kujifunza. Shule hiyo imeamua kuwapa uongozi wanafunzi watoro kama mbinu ya kupambana na utoro shuleni. Picha zote na Juma Mtanda

Utoro unatajwa kuwa moja ya changamoto kadhaa zinazozikabili shule za umma nchini.

Takwimu za elimu msingi mwaka 2016 (BEST, 2016), zinaonyesha kulikuwapo watoto 139,866 watoro katika shule za msingi na sekondari katika shule mbalimbali nchini.  Kiwango hicho ni zaidi ya asilimia 94 ya sababu zinazochangia watoto kuacha shule.

Shule ya Msingi Bungo na utoro

Shule ya Msingi ya Bungo iliyopo  Manispaa ya Morogoro, imebuni njia za kuzuia utoro kwa wanafunzi wake.

Hii ni miongoni mwa shule za msingi za Manispaa ya Morogoro zinazofanya vizuri kwa wanafunzi wa darasa la saba.

Tangu mwaka 2003 shule hiyo ya Serikali, imekuwa na wastani wa kufaulisha wanafunzi  kati ya asilimia 92 na 100.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Roman Luoga anasema kuwa shule yake ipo katika mipango ya kutokomeza utoro, ili ishike nafasi ya kwanza kwa ngazi ya manispaa, mkoa na taifa.

“Zipo mbinu ambazo tunaendelea kuzitumia ili mwanafunzi apende shule na tumeweka malengo ya kutokomeza utoro, ili tufanye vizuri kwa kushika namba moja katika mitihani ya Taifa ya kuhitimu elimu ya msingi,” anasema.

Luoga anafichua mbinu hizo zinazomshawishi na kumvutia wanafunzi kupenda kuhudhuria masomo shuleni, kuwa  ni pamoja na kuwapa uongozi wanafunzi wenye tabia ya utoro.

“Shule ya Msingi Bungo tuna vivutio vingi vinavyochangia mwanafunzi  apende kusoma. Hivi ni  kama uwepo wa chakula cha mchana, vipindi vya michezo ya kompyuta, mpira wa miguu, pete, ngoma lakini  bendi ya shule imekuwa kivutio kikubwa kwa wanafunzi,’’ anaeleza.

Anasema baada ya kubaini wanafunzi watoro kutokana na sababu mbalimbali, wanafunzi hao  hupewa uongozi unaowazuia kutoroka shuleni.

Mbinu nyingine anasema ni kuwasaidia wanafunzi wanaofanya utoro kwa sababu ya hali ngumu ya maisha.

 “Wapo wanafunzi wanaofanya utoro kwa sababu za msingi lakini baada ya kufuatilia tumegundua  baadhi ya watoto ni yatima na wanaishi katika mazingira magumu hivyo tuna  jukumu la muda mrefu la kumsaidia mwanafunzi husika,’’ anasema na kuongeza:

“Ipo timu maalumu ya walimu na wanafunzi yenye kazi ya kuwatembelea wanafunzi wote watoro nyumbani na imekuwa ikisaidia kujua matatizo yanayosababisha kuwa watoro ambapo tunasaidiana na walezi kutatua matatizo hayo.’’

Kwa wanafunzi  wanaoishi katika mazingira magumu, shule imekuwa na utamaduni wa kuwatambua idadi yao kila mwaka na kuwanunulia vifaa vya shule lakini pia kuwapatia chakula maalumu shuleni.

Ziara za kimasomo nje ya nchi

Shule ya Msingi Bungo imekuwa ikifanya vizuri kwa kuchangiwa na ujuzi unaotokana na kufanya ziara za kimasomo ndani na nje ya nchi kwa lengo kujifunza na kubadilishana  uzoefu wa ufundishaji na ujifunzaji.

Mwalimu wa taaluma,  Rose John anasema shule yao ina utamaduni wa kufanya ziara ya kujifunza katika  shule za msingi zinazofanya vizuri katika mitihani ya Taifa ndani na nje ya nchi.

“Ziara za kimasomo ndani na nje ya nchi, zimetusaidia walimu kupata mbinu mbalimbali za ufundishaji kutoka  shule tulizotembea nasi kuongeza ubunifu wetu kwa wanafunzi,’’ anasema.