Mbinu za kushinda maswali ya usaili wa kazi - 3

Muktasari:

Pamoja na maswali mengine, unaweza kuulizwa maswali kuhusu uzoefu wako wa kikazi huko ulikotoka.

Katika makala yaliyopita tuliona maeneo manne muhimu ya kuzingatia unapoingia kwenye usaili.

Pamoja na maswali mengine, unaweza kuulizwa maswali kuhusu uzoefu wako wa kikazi huko ulikotoka.

Tuliona kuwa unapoulizwa maswali kama hayo, lengo ni kupima namna unavyoweza kuwa mkweli.

Usikimbilie kumponda mwajiri wako wa zamani kwa kutoa sababu za kutoridhika na mshahara, migogoro ya kazi uliyokuwa na mwajiri wako, kutoelewana na wakubwa wako wa kazi au watu uliokuwa unawasimamia.Ukifanya hivyo utaonekana wewe ni mtu wa matatizo.

Badala yake, toa sababu chanya zinazoleta picha ya mtu mkomavu kazini. Kwa mfano, unaweza kuonyesha kuwa uliacha kazi uliyokuwa nayo kwa sababu ulipata fursa ya kutumia vipaji vyako vizuri zaidi kwingineko, au kwamba kazi uliyoipata ingekuwezesha kukua kiujuzi zaidi. Katika makala haya, tutatazama maeneo mengine manne unayohitaji kujiandaa ili kushinda maswali utakayoulizwa kwa mafanikio.

 

Matarajio yako kwa mwajiri

‘Unadhani tukulipe mshahara kiasi gani?’

Hili swali linatafuta kujua vipaumbele vyako ukiwa kazini. Ni kweli unatafuta kazi ili upate fedha uboreshe maisha yako. Lakini kuonyesha kuwa ari na kujituma kwako kazini kunategemea na kiasi cha pesa unacholipwa ni kosa la kiufundi. Kosa hili linaweza kuwa kikwazo cha kukukosesha kazi.

Unahitaji kuonyesha ukomavu kwa kuelewa kuwa taasisi bora kama hiyo unayotaka ikuajiri, zina utaratibu rasmi wa kuwalipa wafanyakazi wake. Mtu hulipwa kwa sifa alizonazo. Kwa uelewa huo, utapata alama za ziada.

Hata hivyo, pamoja na majibu hayo wapo wasaili wanaoweza kukubana uwaambie matarajio yako. Fahamu kuwa kujadili mshahara wa kazi ambayo bado hauna uhakika nayo, haiwezi kukusaidia.

Ikiwa utalazimika kutaja tarakimu, inatarajiwa kuwa tayari utakuwa umeshafanya utafiti wa taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na viwango vya mishahara.

Taja kiwango ambacho hakitaonyesha huna thamani, lakini pia usitaje kiwango kitakachoonyesha kujikweza kupita kiasi.

 

Uelewa wa mambo na ujuzi wa kazi

Unaweza kuulizwa maswali yanayopima uelewa wako wa kawaida kwa mambo yanayofahamika. Lakini pia unaweza kuulizwa masuala ya moja kwa moja yanayohusiana na kazi unayoomba.

Wakati mwingine, baadhi ya wasaili hutumia mtihani wa kuandika kujaribu kuthibitisha kama kweli una uwezo na ujuzi uliouonyesha kwenye wasifu wa kazi.

Maswali yanayoulizwa yanaweza kupima moja kwa moja utaalamu uliousomea darasani au namna unavyoweza kutatua changamoto halisi za kazi. Jiandae ipasavyo kwenye maeneo muhimu.

Kilicho muhimu ni namna unavyoweza kutafsiri nadharia zako katika mazingira ya kazi.

Kwa mfano, unaomba kazi ya uhasibu msaili mmoja anakuuliza, ‘Chukulia ofisini kwako kumetokea wizi wa fedha. Utachukua hatua gani?’ Au unaomba kazi inayohusika na utawala, ‘Chukulia kama kiongozi umesikia wafanyakazi wa chini yako wana mpango wa kugoma. Utafanyaje?’

Hayo ni maswali ya uchokozi. Usitumie muda mrefu kutafuta masuluhisho yasiyokuwepo. Jibu kwa ujasiri kuwa hutarajii kuwa matatizo ya namna hiyo yatajitokeza. Lengo ni kuonyesha una uwezo wa kuikinga taasisi yako na changamoto kama hizo.

 

Malengo yako ya baadaye

‘Unajiona ukifanya nini baada ya miaka 10 ijayo?’

‘Una malengo gani ndani ya miaka mitano ijayo?’

Hapa unahitajika kuonyesha ari ya kukua kiujuzi na kiuweledi. Ongelea mipango ya kujifunza zaidi kufikia kwenye malengo makubwa yanayoendana na malengo mapana ya kitaasisi. Kuzungumzia malengo yasiyoendana na kazi unayoomba kutakupunguzia alama.

‘Umeomba kazi kwingine?’ Wanahitaji kuwa na uhakika na maamuzi yako. Ni kweli inawezekana utakuwa umeomba kazi maeneo mengine. Lakini utaonekana mkomavu ukiweza kuonyesha kuwa kazi hii unayosailiwa ndio chaguo la kwanza.

 

‘Utafanya kazi na sisi kwa muda gani?’

Hapa wanataka kujua kama wewe ni mpita njia au la. Inawezekana kweli unaweza kuwa na mpango wa kufanya kazi kwa muda mfupi na utafute njia nyingine. Lakini kuonyesha wazi kuwa unapita wakati hata kazi hujapata si busara. Onyesha ungependa kufanya kazi kwa muda mrefu kadri utakavyohitajika.

‘Unaota kufanya kazi gani nzuri baadae?’ Ukitaja kazi nyingine mbali na hiyo unayoomba, unaleta wasiwasi kuwa hutaridhika na kazi unayoomba. Ongelea mazingira ya kazi bila kutaja kazi mahususi. Kwa mfano, kazi inayokufanya utumie vipaji vyako na ujuzi ulionao. Kazi inayokufanya ukue kiujuzi na kiuzoefu.

‘Uko tayari kuanza kazi lini?’Kama huna kazi, ukisema uko tayari kuanza kazi mara moja inaonyesha utayari ulionao. Lakini kama unabadilisha kazi, kuonyesha utahitaji muda mfupi wa kukamilisha taratibu za kukabidhi majukumu uliyonayo na kuaga, itakupa alama.

 

Fursa ya kuuliza swali

Kwa kawaida, baada ya kuulizwa maswali mengi, kikao cha usaili kitahitimishwa kwa kukukaribisha kuuliza swali. Kama tulivyosema, kila swali lina maana. Unapoulizwa, ‘Je, una swali ungependa kuuliza?’ lengo ni kutaka kujua ulivyo na ari ya kufanya kazi na taasisi hiyo.

Usipouliza swali lolote, maana yake ama huna uelewa wa mambo mengi au huna ari ya kutosha. Uliza swali kuhusu taasisi hiyo. Waliuze wanatarajia nini kwa mtu atakayepata kazi hiyo. Pia unaweza kuulizia mambo yanayohusiana na fursa wanazoweza kutoa kukuza ujuzi wako kama mfanyakazi wao.

Epuka kuuliza maswali ya kimaslahi kama kuuliza’ mtanilipa bei gani?’ Hii inaonyesha huna mtazamo mpana wa kazi. Unaweza hata usijibiwe au ukajibiwa jibu litakalokunyong’onyeza.

Shukrani kwa Fr Aldalbert Donge, Mkurugenzi wa Raslimali Watu, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenye kwa kuchangia uzoefu wake katika makala haya. 0754 870 815