Mchungaji Msigwa: Kilimo ni utajiri na heshima

Mbunge wa  Iringa Mjini, Mchungaji  Peter Msigwa akiwa katika moja ya mashamba yake mkoani Iringa. Na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

  • 16 Ekari za mahindi alizolima mwaka huu, huku sita zikitumia kilimo cha umwagiliaji.
  • 50 Ekari anazotumia kufuga wanyama.

Siyo tu  siasa, hata kwenye kilimo, Mbunge wa  Iringa Mjini (Chadema),  Mchungaji Peter Msigwa ni kinara. Kila anapopata nafasi, huchukua jembe kisha kuelekea shambani.

Kuna wakati hulima kwa kutumia jembe la mkono na wakati mwingine kwa zana za kisasa kama vile  trekta kulingana na eneo au mazao aliyoamua kulima kwa wakati huo.

Baadhi ya watu wanamshangaa na hata kujiuliza kwa nini hatumii zaidi vibarua, badala yake huamua mwenyewe kufunga kibwebwe.

Imefika hatua wananchi wamemzoea kwani licha ya kujishughulisha na kilimo, aina ya maisha yake akiwa mjini Iringa ni ya kawaida, kiasi cha kupata mlo wake kwa ‘mamalishe’ bila wasiwasi wowote.

Maeneo yaleyale aliyopenda kutembelea wakati hajawa mbunge ndiyo anayotembelea hivi sasa. Tangu hajawa mbunge alipenda kilimo na sasa jitihada zake kwenye sekta hiyo zimeongezeka zaidi.

Mchungaji Msigwa anasema kilimo ni utajiri na kimempa heshima siyo tu kwa wananchi waliomchagua bali hata kwa viongozi wenzake, hususan wabunge.

 “Naona fahari kulima, kilimo kimeniongezea heshima kwa jamii kwani licha ya kuongeza kipato changu, nimekuwa mwalimu mzuri kwa ninaowaongoza hasa vijana wenye fikra finyu kwamba kilimo ni cha watu wa kada ya chini,”anasema.

Anakiri kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa taifa na kinaweza kukuza uchumi wa nchi, ikiwa kutakuwa na jitihada za kuamua kuwekeza ipasavyo.

Analima nini?

Msigwa amejikita katika mazao mbalimbali ya biashara na chakula ikiwamo miti, mahindi, nyanya, vitunguu na mengine aina ya kunde. Pia, ni mfugaji mzuri wa kuku wa nyama na mayai.

“Nikiwa nyumbani naingia bandani mwenyewe kuhudumia kuku, nimezoea hivyo na siwezi kuacha,”anaeleza.

Mchungaji Msigwa alianza kujishughulisha na kilimo tangu hajapata ubunge na imekuwa vigumu kwake kuacha asili yake, na hivyo kuwa mfano kwa wakulima wengine katika mkoa huo. Anachofanya ni kusadifu usemi wa jasiri haachi asili.

Wakati hajawa mbunge, alifahamika zaidi wakati alipokuwa akiuza miche ya miti ya aina mbalimbali aliyokuwa akiandaa kwenye vitalu vyake.

Hakuwa na aibu  kuuza miche hiyo huku wakati mwingine akiikokota  kwenye toroli lililokuwa kikivutwa na gari yake. Kwake ilikuwa  fahari na wengi walimtambua kwa uchapa kazi wake.

Kwa nini kilimo?

Kwa kuwa anaamini  kilimo siyo kazi ya watu wa chini kama wengi wanavyodhani, aliamua kuongeza jitihada ili awe mfano kwa vitendo kwa wananchi  anaowaongoza.

Anasema wazazi wengi wanatamani kusomesha watoto wao na kuwasihi wasije kuwa wakulima jambo ambalo si la kweli, japokuwa naye alipitia huko kimtazamo.

Anasema ukweli ni kwamba kilimo ni fursa kubwa kwa watu kufanikiwa kiuchumi, ikiwa kitaendeshwa kwa kufuata kanuni bora ikiwamo matumizi ya pembejeo na kuwatumia wataalamu.

“Utapata chakula na utaweza kupata mavuno na kuuza, utajiri upo shambani,” anasisitiza.

Anasema hajawahi kujuta kuwa mkulima. Kwa mwaka huu amefanikiwa kulima eka 10 za mahindi zinazotegemea mvua, ekari sita za mahindi zinazotumia kilimo cha umwagiliaji na ekari 50 ameamua kufuga ng’ombe na wanyama wengine.

Anakiri kuwa zipo faida nyingi alizopata kupitia kilimo mpaka sasa ikiwamo za kiuchumi kwa kuwa hategemei zaidi fedha za mshahara wa ubunge.

Hata hivyo, anasisitiza kuwa nia yake ya kutoa elimu kwa vitendo kwa wananchi imewafanya wakazi wa Iringa mjini hasa vijana kuona wana jukumu la kutafuta mashamba na kuwekeza kwenye kilimo.

“Vijana wengi walikuwa wakija na kulialia maisha magumu huku wakitaka kupewa fedha. Kila wakiniona nimeshika jembe na nimekaa mkao wa kwenda shambani wanapata kigugumizi cha kuomba. Wanajikuta wanaamua kwenda kulima,” anasema na kuongeza: “Napenda kuwapatia wananchi wangu nyavu wakavue samaki, siwezi kuwapatia samaki. Huwa nawaambia waziwazi kwamba, lazima tufanye kazi kwa bidii ili tuje kuishi maisha mazuri baadaye.”

Changamoto anazokutana nazo

Msigwa anasema mabadiliko ya tabia nchi ni kati ya changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo kwa sasa. Anasema mazao mengi yanaharibikia shambani kutokana na jua kali lakini hilo halimzuii kuendelea na kilimo.

Hata hivyo, anasema wakulima wasingeumizwa na hali hiyo kama nchi ingewekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji.

Aidha, anasema  ukosefu wa soko kwa baadhi ya mazao ni changamoto nyingine inayowakumba wakulima wengi akiwamo yeye.

Anasema yapo mazao kama nyanya ambayo ikiwa yatakosa soko la uhakika kipindi yanapohitaji mavuno ya uhakika yanaweza kusababisha hasara kubwa.

Mchungaji Msigwa anasisitiza kuwa ipo haja kwa Serikali kuwekeza katika kilimo ili iwe rahisi kufikia ndoto za Tanzania ya viwanda.

“Soko litapatikana la uhakika tukiwa na viwanda vya kutosha na kuweza kusindika mazao yetu. Ukosefu wa soko la uhakika kwa mazao ya wakulima ni changamoto kubwa,’’ anaeleza.

Kuhusu changamoto ya pembejeo hasa mbolea, anawaasa wakulima kutumia samadi badala ya kutegemea mbolea ya ruzuku.