Mechi tano ziliwalaza Simba SC na viatu

Muktasari:

  • Pamoja na Simba kutwaa ubingwa huo wa 19 ikiwa na michezo mitatu mkononi, Simba ilipambana kwa jasho na damu katika mechi hizi tano na kupata matokeo au kuambulia pointi moja.

Ukisema mwaka huu ulikuwa mwepesi kwa Simba hadi kutwaa ubingwa, utakuwa umebugi. Mambo hayakuwa mepesi kihivyo.

Pamoja na Simba kutwaa ubingwa huo wa 19 ikiwa na michezo mitatu mkononi, Simba ilipambana kwa jasho na damu katika mechi hizi tano na kupata matokeo au kuambulia pointi moja.

Simba vs Mtibwa Sugar

Mechi zote za Simba na Mtibwa, ile ya Oktoba 15 mwaka jana ambayo ilimalizika kwa sare ya 1-1 na mchezo wa marudiano ambao Simba ilishinda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Katika mchezo wa kwanza, Simba ilikiona cha moto kwa kulazimisha sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam mbele ya Mtibwa Sugar ambao walionekana kuwa na msimu mzuri.

Stamili Mbonde aliifanya Mtibwa Sugar kuongoza kwenye kipindi cha kwanza, Simba ilitumia nguvu kubwa kusawazisha bao hilo ndani ya dakika tatu za nyongeza kupitia kwa Emmanuel Okwi.

Okwi alipiga mpira wa faulo nje ya 18 na kuujaza upande wa kushoto wa kipa Benedict Tinocco, ikawa ahueni ya Simba siku hiyo.

Mchezo wa pili, kama ilivyotarajiwa, ulikuwa mgumu kwa Simba ambao walicheza kwa jitihada zote kuhakikisha wanashinda. Hata walipofunga bao dakika ya 23 kupitia kwa Okwi tena, Simba hawakuwa na uhakika wa maisha kutokana na Mtibwa Sugar kuwapeleka puta na kucheza kwa tahadhari hadi dakika ya 90.

Singida United vs Simba

Pamoja na kwamba Simba ilishinda mabao 4-0 na tayari wana ubingwa, na ulikuwa mchezo wa heshima kwa Simba lakini ulikuwa mgumu kutokana na Singida kutaka kulipa kisasi na Simba kuweka heshima.

Bao la Shomari Kapombe lilitosha kuwafanya Wekundu hao wa Msimbazi kupumua na hata kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Simba vs Yanga

Mchezo wa duru la kwanza wa ligi ulimalizika kwa sare bao 1-1 haukuwa wa presha kutokana na mazingira ya mchezo huo.

Shughuli ilikuwa Aprili 29, mechi ya duru la pili, kulikuwa na mtifuano wa kutosha kwa timu hizo mbili. Hata hivyo Simba ilishinda kwa bao 1-0 la Erasto Nyoni, japo lilikuwa bao jepesi, lakini Simba walihangaika kiasi chake.

Simba vs Lipuli

Simba iliingia mechi na Lipuli kwa tahadhari, waliikamia na walipata pointi mbili tu , walitoka sare ya 1-1 mechi zote, Dar es Salaam na Samora mjini Iringa.