KILIMO CHA KISASA: Menejimenti ya mbolea katika ukuaji wa mmea-1

Mbolea ni hitaji muhimu kwa maendeleo ya mmea. Hata hivyo, kunahitajika umakini katika kuweka mbolea shambani. Picha na mtandao wa university of missouri

Muktasari:

Mazao haya mengi hayaji kwa kubahatisha, bali kwa kuzingatia kanuni maalumu za uwekaji wa mbolea kwenye mmea wake tena kwa wakati maalumu. Na hapa ndipo mahala ambapo wakulima wengi hukwama.

Ikumbukwe kuwa ili mkulima aweze kupata faida anapaswa kupata mavuno mengi kwenye eneo lake, ambayo atakuja kuyauza kwa bei ambayo itamsaidia kulipia gharama.

Mazao haya mengi hayaji kwa kubahatisha, bali kwa kuzingatia kanuni maalumu za uwekaji wa mbolea kwenye mmea wake tena kwa wakati maalumu. Na hapa ndipo mahala ambapo wakulima wengi hukwama.

Ieleweke kuwa ukuaji wa mmea na maendeleo yake kwa ujumla, vinahitaji virutubisho ambavyo ndiyo chakula cha mmea. Kama tulivyoona hapo mwanzo virutubisho huweza kuongezwa udongoni kwa njia asili kama uwekaji wa mimea jamii ya mikunde shambani, kuacha majani yaoze shambani, au kinyesi cha wanyama

Pia, utengenezaji wa mboji kwa kutumia mabaki ya mimea na wanyama na nyinginezo katika njia asili. Lakini mkulima akikosa mbolea asili, anaweza kuupatia mmea wake virutubisho kwa njia za kisasa yaani matumizi ya mbolea za dukani.

Ila kabla ya uwekaji virutubisho shambani mkulima anapaswa kujua kuwa kila shamba lina historia maalumu ambayo humaanisha kuwepo kwa virutubisho fulani vya madini ya fosiforasi na potasiamu.

Virutubisho hivi vinaweza vikawa hamna, vichache, vingi zaidi ya mahitaji. Haya yote hutegemeana na shamba husika na historia yake, mazao yaliyolimwa kipindi kilichopita, mbolea iliyowekwa kipindi kilichopita na sababu nyinginezo.

Mkulima hapa hawezi kubahatisha kujua virutubisho vilivyopo katika udongo wake kwani anapaswa kupima na kujua. Kujua virutubisho vilivyopo kunamsaidia mtaalamu kumshauri kuhusu uwekaji wa aina gani ya mbolea na kwa kiwango kipi.

Madhara ya kuweka mbolea bila kujua virutubisho vilivyopo ni kiasi gani, huchangia mkulima kuzidisha virutubisho ambavyo badala ya kuusaidia mmea vitakuwa kikwazo cha ukuaji wa mmea.

Uwekaji mbolea za viwandani

Kitaalamu, mkulima hushauriwa kuweka virutubisho vikuu vitatu ambavyo huhitajika kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa mmea na maendeleo yake kwa jumla. Virutubisho hivi ni naitrojeni, fosforasi na potasiam. Kuna vingine ambavyo pia huhitajika kwa kiasi kikubwa, lakini si kama vilivyotajwa hapo juu; navyo ni salfa, magnesiam na kalshamu.

Mbolea za viwandani huwekwa kwa njia tofauti tofauti kutegemeana na ukubwa wa shamba, aina ya zao, lengo la uwekaji na rasilimali fedha.

Njia kuu za uwekaji ni njia ya kurusha, njia ya kuzungushia mmea na njia ya kuichanganya na maji na kuingiza katika matone. Njia nyingine ni kuweka kwenye majani.

Njia ya kurusha

Hii ni ambayo mbolea za chengachenga huwekwa katika mmea kwa njia ya kurushwarushwa shambani. Shamba huhitajika liwe limelowa ili iweze kunyonywa na mimea husika. Mara nyingi njia hii hutumika katika mashamba makubwa pale ambapo wafanyakazi ni wachache.

Pia, husaidia mbolea kwenda katika maeneo mengi kwa usawa mzuri kabisa. Aina hii hutumika katika mazao kama vile vitunguu, mpunga, shayiri, ngano na mengineyo.

Njia ya kuzungushia mmea

Mbolea huwekwa kwa kuzunguka mmea husika. Hapa mbolea haitakiwi kugusa mmea hata kidogo. Baadhi ya wakulima hutumia njia hii, lakini kwa kurusha mbolea, hilo ni kosa kwa kuwa mbolea inaweza kugusa mmea na kuudhuru.

Inashauriwa mbolea iwekwe mbali kama sentimeta nne kuzunguka mmea. Unaweza kutumia njia hii kwa mazao kama hoho.

Njia ya kuchanganya mbolea na maji

Hii inatumika kwa wale wanaotumia mfumo wa matone. Kunakuwapo pipa maalumu ambalo huchanganywa mbolea na maji kisha inaingizwa katika mfumo wa umwagiliaji wa mmea kwa kipindi maalumu. Njia hii inaweza kutumika katika matikiti maji, hoho, nyanya na mazao mengine.

Njia ya uwekaji kwenye majani.

Njia hii ni nzuri maana mbolea iliyokwisha kuchanganywa na maji hupuliziwa katika majani ya mmea moja kwa moja.

Kwa kawaida, mkulima atambue kuwa anapopiga kiwango cha dawa katika mbogamboga huchukuliwa haraka sana kuliko anapopiga katika mimea ya miti kwani miti huchelewa kuichukua mbolea hiyo. Itaendelea wiki ijayo