MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Methali na malezi kwa watoto, vijana wetu

Muktasari:

Methali ni kauli zinazobeba ujumbe wenye hekima na busara kwa lengo la kutoa maadili katika jamii, kufunza, kuongoza, kurekebisha na kuonya. Kutokana na umuhimu wake, methali zimekuwa zikipewa nafasi maalumu katika magazeti, vitabu na majarida mbalimbali.

        Methali ni kipengele cha semi katika fasihi simulizi.

Methali ni kauli zinazobeba ujumbe wenye hekima na busara kwa lengo la kutoa maadili katika jamii, kufunza, kuongoza, kurekebisha na kuonya. Kutokana na umuhimu wake, methali zimekuwa zikipewa nafasi maalumu katika magazeti, vitabu na majarida mbalimbali.

Hata hivyo, wazazi na walezi wanapoongea na watoto na vijana, wamekuwa wakitumia methali kama njia ya kukazia ujumbe wao.

Gazeti maarufu la ‘Mwenge’ linalochapishwa na Wabenediktini wa Peramiho, takriban muongo mmoja uliopita lilikuwa na safu maalumu iliyoitwa ‘Methali Zetu’.

Safu hiyo iliwasaidia watoto kujifunza methali zenyewe na maadili yatokanayo na methali husika. Halikadhalika, vijana na watu wazima walijifunza mengi kuhusu maisha kupitia safu hiyo.

Kwa wakati huu, hali ni tofauti kidogo, kiwango cha matumizi ya methali kimepungua. Bila shaka sababu kubwa ya kupungua huko ni utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakiibeza fasihi simulizi na vile vinavyopatikana ndani yake.

Hata hivyo, umuhimu wa methali hizi unabaki palepale. Tena katika zama hizi, methali hizi zinahitajika zaidi katika malezi kutokana na uchangamani wa mambo.

Utandawazi umetuletea mengi mazuri na mabaya. Changamoto kubwa kwa wanajamii ipo katika kufanya uchaguzi wa jema la kuigwa na baya la kuachwa. Wengi wamekuwa wakiyavamia maisha huku mambo yakiwatokea puani.

Vijana wengi wakati huu, wameziba masikio, hawasikii la kuambiwa, wanataka kujionea wenyewe. Laiti methali zingetumika kwa dhati kuwafunda watoto na vijana katika malezi, huenda mambo yasingekuwa yalivyo.

Hebu tuangalie methali chache zenye dhima kubwa katika malezi. Hizi ni: ‘Majuto ni mjukuu’, ‘asiyesikia la mkuu huvunjika guu’ na ‘asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu’

Ni methali zitoazo maonyo na hadhari zikiwataka watu wazingatie yale wanayoelekezwa.

Kwa mfano, baadhi ya vijana wamekuwa wakivamia miji na majiji bila maandalizi yoyote. Matokeo yake maisha yanapowashinda, hujiingiza katika makundi mabaya yanayojihusisha na vitendo viovu.

Kwa kufanya hivyo hujikuta wakiangukia mikononi mwa vyombo vya dola. Methali hizi na nyingine, zinawataka wanajamii hususan watoto na vijana kuzingatia maoni ya wakubwa wao.

‘Mwenda tezi na omo, marejeo ngamani’ ni methali nyingine inayowataka watu kuwa watulivu badala ya kuhangaika.

Wapo watu wapendao kuzurura huku na kule. Baadhi ya vijana hupenda kufanya hivyo licha ya wazazi au walezi kuwasihi kutulia.

Wengi hupuuza ushauri wao na kuendelea na taratibu zao mbaya za maisha. Vijana wengi wa kike kwa wa kiume, wanapotangatanga na kufikia pahali wakagonga mwamba, hurejea kwa wazazi na kuwasababishia usumbufu mkubwa.

Mathalani, baadhi ya vijana wanaojihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya na ukahaba wanapoona wameharibikiwa, hurejea nyumbani wakihitaji msaada wa wazazi na walezi. Laiti wangezingatia mwongozo wa wazazi au walezi wao, wasingeharibikiwa.i na semi nyingine ni nyenzo bora ya kuwafundia watoto na vijana kuhusu maisha.

Kauli hizi zenye busara zinapaswa kutumiwa ili kuwasaidia vijana kukua wakiwa waadilifu, hivyo kuwawezesha kuwa na mustakabali mwema.