ELIMU NA MALEZI : Mfundishe mtoto namna ya kudhibiti hisia zake

Muktasari:

  • Kwa maelezo yake, mwanawe ana tabia ya kulia bila sababu za msingi na mara nyingi hushitaki wenzake kwa makosa madogo, ambayo kwa mujibu wa mama yake, angeweza kuyashughulikia bila kulazimika kusema.


        Majuzi nilizungumza na mama Rehema (si jina lake halisi) mzazi mwenye mtoto wa miaka 14.

Kwa maelezo yake, mwanawe ana tabia ya kulia bila sababu za msingi na mara nyingi hushitaki wenzake kwa makosa madogo, ambayo kwa mujibu wa mama yake, angeweza kuyashughulikia bila kulazimika kusema.

Mbali na tabia hiyo ya kudeka, mama Rehema anasema mwanawe ana shida ya kulipuka. Katika michezo, kwa mfano, Rehema hupandwa na hasira kiasi cha kuweza kuwashambulia wenzake kwa makonde na maneno makali.

Inavyoonekana mwanzo mama Rehema alichukulia tabia hii kirahisi. Lakini kadri Rehema anavyokua, hali inaendelea kumtia wasiwasi.

Kwa sasa anasema wakati mwingine Rehema hutamka maneno makali kwa mtu yeyote bila kujali atakavyojisikia.

Katika kujadiliana na mzazi huyu, yalijitokeza mengi. Mojawapo ni tatizo la uchanga wa kihisia. Mtu mchanga wa kihisia ana uwezo mdogo wa kudhibiti hisia zake.

Mbali na kushindwa kuishi vizuri na watu, anaweza pia kujidhuru kiafya na hata kisaikolojia.

Vile vile, kutofanya vizuri masomoni, kunaweza kuchangiwa na uwezo mdogo wa mtoto kudhibiti hisia zake.

Hisia ndizo zinazoongoza maamuzi ya mtu. Mtu mwenye ukomavu wa kihisia anapokutana na mazingira yanayomkatisha tamaa, anakuwa na uwezo wa kukabiliana nayo na hivyo kurudi katika hali yake ya kawaida kirahisi.

Hivyo mzazi unao wajibu mkubwa katika kumjenga mtoto kihisia tangu mapema. Ukiweza kumsaidia mtoto kuwa mkomavu kihisia, unampa uwezo wa kujitambua na kuwa mlinzi wa hisia zake mwenyewe.

Makala haya yanalenga kukushauri mambo matano rahisi unayoweza kuyafanya ili kumjenga mwanao kihisia.

Mfundishe kukubali hisia zake

Watu wengi wana tatizo la hisia kwa sababu wamelelewa kwenye mazingira yanayowanyima fursa ya kutambua hisia zao.

Kwa kujua kuwa hisia fulani hazikubaliki, watu hawa wamejifunza kuficha na kukana hisia zao ili wawe salama.

Hali hii ina hasara kubwa mbili. Kwanza, inajenga tabia ya kuwategemea watu wengine kulinda hisia zao. Wanapojisikia vibaya wanafikiri kuna mtu mwingine amefanya wajisikie vibaya na wao hujiondoa kwenye wajibu.

Hasara ya pili, inajenga mazoea mabaya ya kuhukumu watu wengine wanapoonyesha hisia zisizotarajiwa.

Hisia ni maumbile. Mfundishe mtoto kuzitambua na kuzikubali. Mtoto ajue tofauti ya kufurahi, kukasirika, kukereka, wasiwasi, huzuni, hofu na hisia nyingine. Kutambua hisia zake kutamsaidia kujielewa anapokuwa katika hali fulani.

Katika mazingira ambayo wewe kama mzazi umemruhusu kuzionyesha, mtoto hatojisikia hatia kuzikubali.

Mfundishe mtoto kumiliki hisia zake

Ongea na mtoto aelewe kuwa hisia alizonazo ni zake. Hana mtu mwingine wa kumlaumu anapokuwa na hisia fulani. Hasira, huzuni, kukata tamaa, wasiwasi, havisababishwi na mtu mwingine bali yeye mwenyewe.

Mtoto anahitaji kufahamu kuwa vile tunavyojisikia ni matokeo ya vile tunavyofikiri. Hasira, huzuni, furaha vyote vinaanzia kwenye mawazo yetu. Namna gani tunatafsiri mambo ndiyo hasa chanzo cha hisia tulizonazo.

Mtoto anapofahamu uhusiano huu kati ya fikra zetu na hisia tunazokuwa nazo, unakuwa umemsaidia kuwajibikia zaidi hisia zake. Hatokuwa mwepesi kumlaumu mtu mwingine pale anapojisikia vibaya, kwa sababu ataelewa kilichomfanya ajisikie vibaya si mtu mwingine.

Mruhusu kuonyesha hisia zake

Kuna nyakati sisi kama binadamu tunakuwa na huzuni. Mioyo yetu inaweza kuomboleza, kusikitika, kuhuzunika kwa sababu kuna mambo fulani tusiyoyatarajia yametokea kwenye maisha yetu.

Hisia hizi zina faida kwetu. Tunapoomboleza, tunajipa matibabu ya nafsi. Mtu anayeomboleza anajisaidia kukabiliana na kile kilichotokea na anajiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kurejea kwenye hali ya kawaida baada ya muda mfupi.

Mtu asiyejipa muda wa kuomboleza mara nyingi anajizuia kukubali hali halisi. Mtu huyu huchukua muda mrefu kurejea kwenye hali yake ya kawaida. Wakati mwingine anaweza kupata shida ya matatizo ya nafsi kwa sababu hakuipa nafsi yake nafasi ya kucheua.

Ni muhimu wazazi kuwafundisha watoto kutoa hisia zao hasa zile hasi. Mtoto anapokasirika, anaposikitika, usimkemee kumfanya aamini kuwa hasira ni kitu kibaya. Somo muhimu analolihitaji mtoto ni kuchunga kile anachokifanya akiwa amekasirika.

Mfundishe kukabiliana na hisia

Kama nilivyotangulia kusema, hisia ni maumbile. Hatuwezi kuhukumiwa kwa kuwa na hisia fulani. Changamoto, hata hivyo, ni vile tunavyovifanya tunapokuwa na hisia fulani.

Ili uweze kumfundisha mtoto kudhibiti hisia zake, hatua ya kwanza ni wewe mwenyewe kuelewa hisia mbalimbali. Nikuulize, kwa mfano, hisia zipi kati ya hizi unakumbuka kuzipata ndani ya juma lililopita: hasira, furaha, wasiwasi, faraja, furaha, masikitiko, huzuni, kukerwa? Ulichukua hatua gani kukabiliana na hisia hizo?

Kuna mbinu nyingi unazoweza kuzitumia kukabiliana na hisia zako mfano kupumzika mahali palipotulia, kusoma kitabu, kuangalia televisheni, kupooza hasira kwa kufanya utani, kushiriki michezo, kuongea na mtu mwingine.

Mfundishe mtoto namna ya kukabiliana na hisia zake kwa kutumia njia sahihi. Kufoka, kupigana, kutafuta wa kumlaumu si mbinu mwafaka.

Onyesha mfano mwema

Tumesisitiza mara kwa mara kwamba wazazi tunawafundisha watoto kupitia yale tunayoyafanya sisi wenyewe. Kile tunachokiishi kina nguvu kuliko maneno tunayowaambia.

Huwezi kumfundisha mtoto ukomavu wa hisia kama wewe mwenyewe unaonyesha uchanga wa hisia. Mtu mchanga wa hisia ana tabia ya kulipuka, kusema mambo bila kufikiri na kuhukumu kirahisi.

Mtoto anakutazama kama mwalimu wake wa kwanza. Kuwa mfano kwa kudhibiti hisia zako. Mtoto anapokukasirisha, usiwe mwepesi kukimbilia kutoa adhabu. Jifunze kutulia hata kama ni kweli umekasirika. Kama ni lazima, basi mwadhibu ukiwa huna hasira.

Lakini pia, onyesha mfano wa namna unavyoweza kupita nyakati ngumu na bado ukawa imara. Usiwe mwepesi wa kuwalaumu watu wengine mambo yanapokuwa magumu.

Mtoto anapokusikia ukirusha lawama kwa watu wengine, anajifunza kuwalaumu wengine hasa mambo yanapokuwa magumu.

Blogu: http://bwaya.blogspot.com