Miaka 10 ya Ali Nabwa, ndoto zake zingali hai

Mohammed Ali Nabwa

Muktasari:

  • Huyu ni mwandishi ambaye tangia mwanzoni mwa miaka ya 1970 hadi alipoiaga dunia Februari 2007, aliandika kuwa suluhisho la kile kinachosikika mara nyingi kama kero za Muungano, ni mfumo wa serikali tatu.

Miaka 10 iliyopita fani ya uwandishi wa habari Zanzibar na Tanzania kwa jumla ilipata msiba wa kuondokewa na mwandishi habari mahiri na jabari, Ali Mohammed Ali Nabwa.

Huyu ni mwandishi ambaye tangia mwanzoni mwa miaka ya 1970 hadi alipoiaga dunia Februari 2007, aliandika kuwa suluhisho la kile kinachosikika mara nyingi kama kero za Muungano, ni mfumo wa serikali tatu.

Katika moja ya makala zake za mwisho za ukurasa ulioitwa “ Ipo Sku itakuwa Kweli” kabla ya gazeti la Dira aliolitumikia kama Mhariri Mtendaji, aliandika:” Tukitaka tusitake ipo siku itakuwa kweli kwa Tanzania kuwa na Katiba itayoridhiwa na wananchi. Hili litakuwa na mjadala mkali, lakini mwisho wa siku ni kuwepo muungano wa serikali tatu.

Kuzungumzia kuvunja muungano ni wenda wazimu na kuendelea na vuta nikuvute na kukataa ukweli, nayo haingii akilini.”

Alisema kama atakuwa ameiaga dunia walio hai wamkumbuke kwa kauli yake hiyo.

Naona leo vyema nimkumbuke rafiki na swahiba wangu huyu niliyefanya naye kazi sehemu mbali mbali kwa miaka mingi, ukiachilia mbali kucheza naye nikiwa mdogo, lakini yeye akiwa amenizidi umri kwa miaka saba.

Nabwa alisema unachoweza kufanya ni kuchelewesha na si kuzuia mabadiliko kwani hata maisha ya binadamu hurefushwa kwa kutumia mashine, lakini hatimaye kila nafsi itakabiliana na mauti.

Wakati Watanzania hivi sasa ni mara chache wanazungumzia kiporo cha Katiba Mpya, nimeona vyema nimkumbuke na kuikumbusha jamii kuwahi kuwapo mtu huyu aliyetumia kalamu bila ya woga.

Marehemu Nabwa hakuwa na kigugumizi katika kuuleza ukweli licha ya kuelewa athari na hatari zake wakati ule ambapo kuilaumu Serikali ilikuwa

nongwa na aliyejaribu alizushiwa balaa na hata kutangazwa si raia kama alivyofanyiwa yeye.

Mara baada ya Nabwa kuiaga dunia, nilisema marehemu atakumbukwa kwa mengi, lakini zaidi kwa kuwa mkweli na jabari wa kufichua maovu ambayo wengine waliogopa hata kuyasikia, seuze kuyaandikia.

Kwa zaidi ya miaka 40 niliyofanya naye kazi, Nabwa nitamkumbuka kama mwandishi aliyechukia dhuluma na hasa mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, iwe nyumbani au nje ya mipaka yetu.

Hakuwa na muhali kufichua ubakaji uliofanyika Zanzibar zamani.

Siku moja alikabiliana uso kwa uso na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume na kumwambia kuwa kuwanyang’anya

uraia Wangazija ni uonevu.

Yeye alikuwa katika orodha ya waliotangazwa si raia licha ya kuzaliwa, kukulia na kuishi Zanzibar, ijapokuwa kwa vipindi alikwenda

nje kwa masomo au kufanya kazi Bara, Kenya, Comoro, Uingereza na kwengineko.

Nabwa, kwa kuandika mambo yaliyowaudhi wakubwa alikuja kunyang’anywa uraia kwa mara ya pili mwaka 2003.

Alirudishiwa miezi michache kabla ya kuiaga dunia, lakini hata alipotangazwa si raia aliendelea kufichua maovu mpaka siku chache kabla ya mauti kumfika.

Akiandika kwa lugha mwanana iliyokuwa na mafumbo, marehemu aliiambia Serikali ya Zanzibar ilipotaka kulifungia gazeti Dira kwa kukerwa na makala zake kuwa ilikuwa

inafunga banda wakati farasi ameshatoka.

Alisema kama aliyoyaandika hayakuwa ya kweli apelekwe mahakamani na huko atafungua kawa ili watu wakijue chakula kilichofunikwa badala ya kukihisi kwa harufu inayotoka kwenye sahani iliyofunikwa kawa.

Nabwa alifichua mambo ambayo serikali ilitaka yafichwe bila ya kujali gharama zake kwa maisha yake. Hakumuogopa mtu, iwe kwa kuwa na mdaraka serikalini, fedha zinazompa jeuri au nguvu za mwili licha ya kuwa na umbo hafifu.

Alitegemea kalamu ambayo iliwafunua macho maelfu ya watu na kuwatoa tongotongo wale ambao walipoambiwa lami ni rangi nyekundu au nyeupe walikubali kutokana na hofu.

Marehemu aliniambia ukweli lazima usemwe na kama hukuusema wengine watauweka hadharani na mwandishi anayeufumbia macho hatasamehewa na jamii hata akiwa kaburini.

Wakati gazeti la Dira ambalo mimi na yeye tulikuwa miongoni mwa wamiliki lilipofungiwa, aliniambia, “Salim, ukweli hauozi na ukiuficha wengine wataufichua na utakuja kukuumbua. Watafunga gazeti, lakini hawataweza kufunga midomo ya Watanzania juu ya mfumo wa Muungano wanaoutaka.”

Siku zote alisitiza kuwa Muungano unaitwa ni wa Serikali mbili au wa nchi mbili, bali ukweli ni wa watu wa pande mbili, Bara na Visiwani na wao ndio wamiliki na viongozi wamepewa uwakala wa kusimamia utendaji.

Sasa wakati Katiba mpya ya Tanzania imetiwa kapuni, kama vile hapakuwepo juhudi ya kufanya hivyo, nimelazimika kumbuka Marehemu Nabwa.

Kama alivyosema Nabwa, nami nawaambia Watanzania kwamba Katiba mpya ina umuhimu mkubwa na kuiahirisha zaidi ni kusababisha malumbano.

Miongoni mwa mambo ambayo marehemu Nabwa alitaka Serikali ifanye, ni jambo la kawaida katika utawala bora, ni kueleza kilichotokea katika masuala mbalimbali visiwani, ikiwa pamoja na lile alilosikitikia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere la kutoweka baadhi ya wanasiasa alipowaleta Zanzibar kutoka Bara kujibu tuhuma mbalimbali.

Vilevile alielezea simulizi za kusikitisha za watu mashuhuri nchini kama Bibi Titi Mohamed katika kesi ya uhaini iliyosikilizwa na aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, P. T. Georges.

Nabwa alitaka watu waliodaiwa kumdhalilisha Bibi Titi ambao walikuwa hai waulizwe nini kilitokea na kama wangeonekana kuwa na hatia wawajibishwe kisheria.

Nusra atiwe kitanzi

Maisha ya Nabwa yalikuwa na misukosuko, lakini hakutetereka, hata pale alipohukumiwa kifo nchini Comoro kwa kesi ya kubuni ya uhaini.

Alinusurika kuuawa baada ya Serikali ya Rais Ali Saleh aliyetawala Comoro kwa mkono wa chuma kupinduliwa siku moja kabla ya siku ambayo angenyongwa. Katika mazungumzo yetu siku moja juu ya yaliomkuta Comoro, Nabwa aliniambia, “Nilipokea hukumu ile kama majaliwa yangu, lakini sikuacha kumuomba Mungu na nilimshukuru aliponusuru maisha yangu. Hakuna wakati niliojuta kwa ajili ya kusema kweli na sitajuta duniani wala kaburini.”

Nabwa alitiwa katika kundi la watu zaidi ya 100 waliodaiwa kuhusika na mauaji ya Rais Abeid Amani Karume mwaka 1972 na kuwekwa gerezani katika chumba cha waliokuwa wanangojea kunyongwa.

Mimi pia nilikamatwa baadaye ili nisaidie kutoa ushahidi wa uwongo na nilipowaambia walionikamata waifanye wao kazi ile, walihamaki na kuniambia si mzalendo na baadaye nikaachiwa.

Alipotoka gerezani afya yake iliathirika na kupata maradhi ya moyo yaliomsumbua mpaka kufa kwake, lakini aliendelea kama aliyokuwa kabla, mkweli na asiyetetereka.

Alichosisitiza ni kuwa ipo siku mambo yatabadilika, na sasa Watazania, tofauti na ilivyo katika nchi nyingi za Afrika, wanaweza kukemea na kulaani yale ambayo wanaona Serikali inayakosea.

Siku moja tulipokuwa na gazeti la Dira walikuja watu kutuulizia wazee wao waliochukuliwa Nungwi na kupotea katika miaka ya 1960.

Nabwa alisema watu hawa walikuwa na haki ya kuelezwa kilichotoka na alihakikisha habari ile ilitoka licha ya kujua wakubwa wangelikasirika. Na kweli habari ile ilizusha balaa na vitisho.

Ubakaji ulimkera na alihakikisha wakati kila zilipopatikana habari za wakubwa kudaiwa kubaka hakusita kuwapa nafasi za waliodai kubakwa

binti zao kusikika na waliodaiwa kubaka kupewa nafasi ya kujieleza.

Siku moja katika mwaka 1969 aliponitembelea Arusha nikiwa mwandishi wa Tanganyika Standard (sasa Daily News), yeye akifanya kazi Nairobi,

Nabwa aliniambia alishangazwa kusikia Tanzania ikilaani ubaguzi uliofanyika Afrika Kusini wakati hali kama ile ilikuwapo nchini ingawa haikuwa ikipuliziwa tarumbeta katika majukwaa ya kimataifa.

Makala zake

Katika moja ya makala zake zilizofumbua macho na kuwatoa tongo vijana, Nabwa aliuliza, “Kwa nini Watanzania walisikitika alipouawa Steve Biko na makaburu wa Afrika Kusini, lakini hawasikitishwi na mauji ya akina Hanga?

Habari hii iliwaudhi wakubwa, hasa mmoja wa mawaziri aliyedai Dira lilitonesha kovu.

Akiwa Mhariri wa Dira, Nabwa alisakamwa baada ya gazeti kuandika kugunduliwa mafuta Zanzibar.

Serikali ilidai wakati ule kulikuwa hakujagunduliwa hata tone moja la mafuta Visiwani. Nabwa alisema ipo siku Serikali itasahau kwamba ilidangaya na kuamua kusema kweli.

Hii leo tumeuona ukweli na suala la mafuta lilitikisa nguzo za muungano mpaka Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alipotumia hekima na kulipatia suluhisho. Nawaachia wasomaji waulize nani alikuwa hasemi kweli, Nabwa au viongozi wa Zanzibar?

Hata alipotangazwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Omari Ramadhan Mapuri kuwa si raia, Nabwa aliendelea na msimamo wake wa kuandika ukweli na hata alipougua, aliandika akiwa kitandani.

Huyu ndiye Nabwa niliyemjua, muungwana asiye na shaka, jasiri na jabari, alikuwa hana muhali na alikataa kujifanya bwana na hakuwa tayari kugeuzwa mtwana kwa kutaka cheo au fedha.