Miaka 17 ya Tamasha la Pasaka

Muktasari:

Tangu kuwa jukwaa linalowapa nafasi wasanii nane tu mpaka kufikia 25 haikuwa kazi rahisi. Wasanii mahiri Afrika wamewahi kutumbuiza katika tamasha hilo akiwamo Rebecca Malope, Solly Mahlangu na Sipho Makabane   wa Afrika Kusini, Ephraem Sekeleti  wa Zambia, Annastazia Mukabwa, Solomoni Mukubwa  wa Kenya, Kwetu Pazuri (Rwanda) na Faraja Ntaboba  wa DR Congo.

Kwa mara ya kwanza mwaka 2000 Tamasha la Pasaka liliburudisha ‘wapendwa’ jijini Dar es Salaam. Mbele ya watu  700,  waimbaji nane tu walitumbuiza kwa zaidi ya saa tano . Baadhi ya waimbaji waliotumbuiza ni Marehemu Vuyo Makohera, Faustine Munishi, Mzungu Soo na Kwaya Nuru Mtoni.

Miaka 17 baadaye Tamasha la Pasaka limejijengea heshima na kuwa  miongoni mwa yale ambayo husubiriwa kwa hamu kila mwaka. Zaidi ya wahudhuriaji 40,000 hushuhudia tamasha hilo kila mwaka katika kipindi cha miaka 10.

Tangu kuwa jukwaa linalowapa nafasi wasanii nane tu mpaka kufikia 25 haikuwa kazi rahisi. Wasanii mahiri Afrika wamewahi kutumbuiza katika tamasha hilo akiwamo Rebecca Malope, Solly Mahlangu na Sipho Makabane   wa Afrika Kusini, Ephraem Sekeleti  wa Zambia, Annastazia Mukabwa, Solomoni Mukubwa  wa Kenya, Kwetu Pazuri (Rwanda) na Faraja Ntaboba  wa DR Congo.

Mwanzilishi wa Tamasha hilo, Alex Msama anazungumzia safari hiyo alipokutana katika mahojiano na mwandishi wa Gazeti hili Julieth Kulangwa.

Kwa maneno machache unawezaje kuielezea safari ya miaka 17 ya Tamasha la Pasaka?

Haikuwa rahisi na kama isingekuwa wito huenda ningeishia njiani. Namshukuru Mungu ndoto yangu imetimia kwani unapozungumzia muziki wa Injili unamzungumzia Alex Msama.

Ni kwa kiasi gani Tamasha linachangia kukuza ajira nchini?

Mchango wake ni mkubwa kwa sababu kwa wastani kila mwaka huwa linatoa ajira za muda kwa watu wasiopungua 500. Kumbuka hawa ni vibarua tu kwa sababu wapo wale ambao nimewaajiri.

 Tamasha linatoa ajira kwa watengenezaji wa majukwaa, wenye vyombo vya muziki, taa, magari na wenye mapambo.  Mbali na kutoa ajira za muda lakini huwanufaisha wajasiriamali  wenye mahoteli, migahawa, usafiri ambao hunufaika unapofika msimu wa pasaka.

Mchango wa  Tamasha kwenye sanaa?

Sanaa imewaajiri wanamuziki wengi. Kama siyo muziki kwa ujumla huenda vijana wasio na kazi wangekuwa wengi mtaani. Muziki wa Injili umeajiri watu wengi pia. Tamasha linawapa jukwaa wasanii hasa wale wasiofahamika na kuwaingiza katika mfumo wa ajira za sanaa. Kwa mfano Bonny Mwaitege, Christina Shusho, Rose Muhando umaarufu wao umekuja katika jukwaa la Tamasha hili. Siyo tu linawapa umaarufu lakini linawaongezea mapato kwani baada ya hapo mashabiki wanazitafuta kazi zao hasa albamu na kuzinunua.

Mchango wa tamasha katika kukuza pato la Taifa?

Ni mkubwa. Kumbuka pale patauzwa maji ya kunywa, soda, vitafunwa, albamu za wasanii, vitabu na vitu vingine vingi. Hivi vyote vinazalishwa katika viwanda vyetu maana yake watu wanaponunua Serikali inapata kodi yake. Lakini viwanja tunakofanyia matamasha tunakodi. Tunatoa karibu shilingi milioni 20 kwa Dar es Salaam peke yake maana yake kodi inayoingia ni kubwa. Kuna wageni kutoka nje wanaingia nchini. Hapa Serikali inaanza kupata fedha kuanzia kwenye viza na vibali vya kufanya kazi nchini katika msimu wa Tamasha.

Basata wananufaika vipi na Tamasha hili?           

Kwa kifupi kazi tunayoifanya ni kuisadia Basata. Wao ndio wenye jukumu la kuwatafutia majukwaa wasanii na kuwatangaza, lakini sisi tunawafanyia kazi hiyo. Bila uwepo wa matamasha kama haya unalifanya Baraza lipate kazi ya kufanya. Tunawasaidia kuibua vipaji kazi ambayo ilibidi waifanye.

Kupitia  Tamasha waimbaji wametambulika nje ya mipaka kiasi cha kupata mialiko ya kutumbuiza huko. Rose Muhando ni mfano kwani ameshawahi kupata mkataba wa Sony na hivi karibuni atakwenda Marekani kufanya kazi.  Zote ni jukumu la Tamasha.

Katika Tamasha la mwaka huu watatumbuiza wangapi?

Tunatarajia waimbaji zaidi ya 25 kwa sababu wapo wengi wanaochipukia tunaotaka kuwapa nafasi.

Vipi kuhusu kusaidia wasiojiweza?

Kwenye kutoa misaada hatuchagui dini isipokuwa uhitaji. Tumesaidia yatima, wajane , wazee na wengine wenye uhitaji. Na siyo kwamba misaada yote ninatoa kutokana na mapato ya tamasha.

Ndugu yetu Reginald Mengi ametusaidia sana. Tukimwomba pale kunapokuwa na uhitaji wa kuwasaidia hawa wenye uhitaji anatusikia na kutusaidia. Wakati mwingine huwa anatupa matangazo bure katika media zake.

Mwingine aliyekuwa msaada mkubwa kwetu ni Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ambaye alikuwa karibu na sisi baada ya kugundua kuwa tuna nia njema ya kuwasaidia Watanzania wenzetu. Ninaamini Rais wetu John Magufuli atatuunga mkono.

Kumbukumbu nzuri kuhusu Tamasha la Pasaka?

Kubwa ambalo siwezi kuisahau ni pale tulipomwalika Rais Jakaya Kikwete mwaka 2011. Baada ya kumwandikia barua na kukubali kuna watu walitubeza kuwa hatakuja bali atamtuma mwakilishi.

Alitushangaza alipokuja na tulipomlilia kuhusu vibali vya wasanii kutoka nje kuwa ghali na tangu hapo tumeanza kulipa nusu.

Naweza kusema yeye ndiye aliyebadilisha upepo wa Tamasha la  Pasaka kwa kuwa nakumbuka kabla ya hapo tulikuwa tukilifanyia Diamond Jubilee ikabidi sasa tulihamishie Uwanja wa Taifa kutokana na mwamko wa watu kuhudhuria.

Kumbukumbu mbaya uliyokuwa nayo?

Sitasahau mwaka 2013 tulipata changamoto ya kukutana na mvua kila tulipokwenda kufanya Tamasha.  Maeneo tuliyotembelea watu walishindwa kutoka kwa kuwa mvua ilinyesha sana. Iringa tulipata watu 11, Songea tulipata watu kama 100 na Shinyanga watu 20. Tuliishiwa hela, tukakopa mpaka ikabidi tumuweke mtu rehani. Huyo mtu alikaa wiki ikabidi atoroke.

Kwa mara ya kwanza nilikopa mpaka nikawa na madeni yasiyolipika. Kuna wakati magari yaliishiwa mafuta ikabidi mpaka waimbaji na wao wachangie.

Kitu gani kilikusukuma kwenye muziki wa Injili?

Niliamua kutoa huduma hii kumshukuru Mungu kwa aliponitoa katika maisha yangu. Ukweli kabisa kutoka moyoni mwangu ni kwamba sipati faida yoyote katika kuendesha Tamasha, lakini nimejitoa kuhudumia. Najua Mungu ananishushia  baraka kutokana na huduma hii ninayoitoa.

Wizi wa kazi za sanaa ni kilio cha muda mrefu, nini mtazamo wako katika hili?

Serikali haijalivalia njuga suala hili. Ni jukumu la Serikali kulivalia njuga kwa sababu leo hii Rais magufuli akisema sitaki kuona cd feki mtaani zitapotea. Leo hii kila mtu anauza tu kwa sababu anajua hawezi kufanywa chochote.

Kuhusu Tamasha la mwaka huu

Tamasha la mwaka huu litazinduliwa  Aprili 16 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kuhusu maandalizi Msama anasema yamekamilika kwa asilimia 90 kwani baadhi ya waimbaji wamethibitisha kushiriki.

Waliothibitisha kushiriki ni pamoja na  Christina Shusho, Martha Mwaipaja, Jesca ‘BM’ na Goodluck Gosbert.

Wengine ni  Kwaya ya Ulyankuru Tabora, maarufu kama Kwa Viumbe Vyote iliyowahi kutikisa vilivyo katika miaka ya 1990.

Kwaya nyingine ni Kinondoni Revival Choir ambayo italitumia tamasha hilo kuzindua albamu yake mpya huku malkia wa muziki wa Injili nchini, Rose Muhando naye akitarajiwa kuzindua albamu yake ya Ruth.

Kiingilio

Kiingilio katika viwanja vyote litakapofanyika tamasha hilo, viti maalumu ni Sh10,000 na wakubwa ni Sh5,000 na watoto ni Sh3,000.