Miaka 56 ya kupambana na ujinga, maradhi na umaskini

Muktasari:

  • Mwalimu Nyerere alianzisha vita dhidi ya maadui watatu; ujinga, maradhi na umaskini. Alikuwa na maana kwamba ikiwa Tanganyika na baadaye Tanzania itaweza kupigana na maadui hao watatu kwa mafanikio, ingeligeuka kuwa kisiwa cha maendeleo na maisha ya hadhi ya juu sana duniani. Katika uchambuzi huu, tunapitia kwa pamoja ikiwa Taifa letu limefanikiwa kuenzi wito na malengo ya muasisi wa Taifa letu katika vita dhidi ya maadui hao watatu.

Kuna deni ambalo Taifa letu linahitaji kulifanyia tafakuri kubwa wakati huu wa kusherehekea miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika, deni hilo ni lile la masuala makuu ambayo Mwalimu Nyerere, muasisi wa taifa la Tanganyika na baadaye mmoja wa waasisi wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar, alitupatia miaka michache tu baada ya uhuru wa Tanganyika.

Mwalimu Nyerere alianzisha vita dhidi ya maadui watatu; ujinga, maradhi na umaskini. Alikuwa na maana kwamba ikiwa Tanganyika na baadaye Tanzania itaweza kupigana na maadui hao watatu kwa mafanikio, ingeligeuka kuwa kisiwa cha maendeleo na maisha ya hadhi ya juu sana duniani. Katika uchambuzi huu, tunapitia kwa pamoja ikiwa Taifa letu limefanikiwa kuenzi wito na malengo ya muasisi wa Taifa letu katika vita dhidi ya maadui hao watatu.

Utekelezaji baada ya Nyerere

Katika kipindi cha mwaka 1985 hadi 2017 (miaka 32) wakati Mwalimu Nyerere hakuwa madarakani, ziko juhudi mbalimbali zimefanywa katika kupambana na ujinga, maradhi na umaskini. Juhudi hizo zimelenga kuongeza taasisi za utoaji wa elimu, wataalamu, vifaa na miundombinu ili kupambana na ujinga, kuongeza idadi ya zahanati, vituo vya afya, hospitali za kawaida na hospitali za rufaa sambamba na kuongeza wataalamu na vifaa vya utabibu ili kupambana na madhara ya maradhi.

Sambamba na hilo, kumekuwa na njia mbalimbali ambazo zimetumiwa ili kuzuia maradhi na hasa kwa kutoa elimu ya afya, usafishaji wa mazingira na elimu ya kutibu dalili za magonjwa badala ya magonjwa yenyewe. Na kumekuwa na hatua mbalimbali za kiuchumi zimekuwa zikichukuliwa ili kuondoa umaskini – hatua hizo zinahusisha kuwekeza katika uzalishaji wa watu binafsi na kuwafanya wajijengee uwezo wa kiuchumi. Ziko njia nyingi sana zimetumika kuhakikisha kwamba uchumi wa Taifa unakwenda juu.

Pamoja na hatua hizo za muda mrefu na tangu Nyerere aondoke madarakani, Tanganyika (Tanzania Bara) jana ilisherehekea miaka 56 ya uhuru wake huku bado mapambano dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini yakiwa yanalegalega, kwa mtu anayetokea nje ya Tanzania akifika nchini kwetu anaweza kudhani kuwa ndiyo kwanza Taifa linaanza kupambana na maadui hao watatu miaka hii ya 2000.

Kumbe ni kinyume chake, vita dhidi ya maadui hao watatu imepiganwa miaka yote 25 ya utawala wa Mwalimu Nyerere kupitia Tanu na CCM na kisha imeendelea kupiganwa kwa miaka yote 32 ya tawala za Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na sasa John Magufuli wakifanya hivyo kupitia CCM.

Mapambano magumu

Ziko sababu kadhaa zinazosababisha mapambano kuendelea hadi leo na tena kwa mafanikio ya kusuasua. Sababu ya kwanza ni uwekezaji usio na mwendelezo katika mipango na utekelezaji wa hatua za kupambana na ujinga, maradhi na umaskini. Katika kila kipengele kwa miaka 56 tumekuwa tukiwekeza nguvu isiyo na uwiano wa wakati na mahitaji.

Unakuta tunajenga shule nyingi na zinakaa miaka 10 hazina walimu, vifaa wala miundombinu mahsusi. Siku tukipata walimu unagundua kuwa shule zilishachoka na kuchakaa kwa sababu hazikuwa na matunzo.

Ndiyo maana hata mwaka huu, pamoja na juhudi zote zilizofanyika tunaambiwa watoto zaidi ya 12,000 waliofaulu hawakuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza nchi nzima. Hizi siyo dalili nzuri ukilinganisha na hali halisi ya mahitaji ya elimu ili kupambana na ujinga ndani ya nchi yetu.

Vivyo hivyo katika uchumi, hadi leo tumeshindwa kubaini na kuwekeza kwenye eneo ambalo linaweza kuwa chachu ya uchumi wa jumla wa Taifa. Wakati wa Mwalimu Nyerere, kilimo kilikuwa ni uti wa mgongo wa Taifa na Mwalimu alikipigania sana. Awamu zilizofuatia za uongozi wa nchi kila moja iliwekeza kwenye mipango mipya, Mwinyi akafungua soko la nje na biashara huria, Mkapa akajiwekeza kwenye uwekezaji. Kikwete kwenye mahusiano ya kimataifa na kampeni za kuimarisha kilimo na Magufuli kwenye mapambano dhidi ya rushwa na ujenzi wa viwanda.

Takwimu za sasa bado zinaonyesha kuwa asilimia zaidi ya 70 ya wananchi wa Tanzania wanategemea kilimo kuendesha maisha yao. Serikali mkakati yoyote duniani ilipaswa kuona kuwa kilimo ndiyo chachu au injini ya kuamsha maendeleo ya Tanzania na nguvu zingeliwekezwa huko, kwa bahati mbaya sana hilo halijafanyika na halijawahi kuwa na mwendelezo. Tangu Nyerere aondoke madarakani na kampeni ya Kilimo na Viwanda, ambayo kwa kweli ilipaswa kuwa kampeni ya kudumu na yenye kuongoza dira ya Taifa, viongozi wote waliofuata kila mmoja wao ameshuhudia ongezeko kubwa la idadi ya watu ambao wanakuta Taifa halina miundombinu ya kuwahimili.

Msukumo wa kisheria

Tanzania haina msukumo wa kisheria ambao umeiweka Serikali katika jukumu la lazima la kupambana na umaskini, maradhi na ujinga. Masuala ya kupambana na maadui hao watatu yameguswa kwenye Katiba, tena kwa kutajwa kama “haki” za wananchi. Lakini, aina ya haki hizo haiwezi kusababisha Serikali ikafunguliwa mashtaka pale inapokosekana. Tuzungumzavyo katika Tanzania ya leo, maradhi mbalimbali mepesi kabisa yanaua maelfu ya watu na hawana uwezo wa kupata matibabu. Katiba yetu imeishia kusema kuwa kila raia anayo haki ya kuishi, lakini haijafafanua ikiwa Serikali imeshindwa kulinda maisha ya mwananchi huyo, mathalani mwananchi amekosa matibabu na kufariki dunia kwa sababu Serikali haijamwekea hospitali, mwananchi huyo atafanya nini?

Mtizamo huru unaweza kutuhitimishia kwamba kama tangu huko nyuma tungelikuwa na nguvu ya kisheria ambayo inaibana Serikali na kuipa masharti ya namna ya kupambana na maadui hao watatu, leo hii Tanzania ingelikuwa inasherehekea miaka 56 ya kushinda vita dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini. Lakini, kwa sababu maadui hao wakuu hatukuwahi kuweka mfumo thabiti utakaolazimisha kila Serikali iingiayo madarakani ipambane nao kwa kiwango mahsusi, ndiyo maana kila Serikali ikija madarakani inajiwekea vipaumbele vyake ambayo nyakati nyingi havilisaidii Taifa kupambana na maadui hao.

Ndiyo kusema kuwa, baada ya miaka 56 ya uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara), wananchi hawawezi kuishtaki Serikali kokote, ikiwa imeshindwa kuwawekea miundombinu ya kuinua uchumi wao, kupambana na maradhi na kupambana na ujinga.

Takwimu za kimataifa

Mara kadhaa, takwimu za kimataifa zimekuwa propaganda ya kusaidia mataifa masikini kama Tanzania, kukwepa wajibu wake wa kupambana na maradhi, umaskini na ujinga.

Mfano mmoja rahisi ambao sote tunaufahamu ni takwimu za mashirika makubwa ya kimataifa ambayo kwa kiasi kikubwa huwa na mgongano mkubwa wa kimasilahi na nchi maskini. Tazama kwa mfano, takwimu za kimataifa juu ya ukuaji wa uchumi wa nchi za Kiafrika na namna takwimu hizo zinavyopikwa nje ya hali halisi.

Shirika la kimataifa kama IMF, linapokuwa linafadhili makampuni ya uchimbaji mafuta, au madini au rasilimali zingine kwenye nchi ya Afrika, uchimbaji huo unapokuwa wa uhakika, takwimu za IMF kwa nchi hiyo hugeuka na kuwa za kuwahadaa wananchi kuwa uchumi wao unakua sana na hali hiyo inasababishwa na ukuaji wa sekta ya mafuta, madini au nyinginezo.

Mbinu za namna hiyo zinaifanya Afrika isiishi kwenye uhalisia na ndiyo maana miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika imekuwa ikishuhudia propaganda hizo badala ya masuluhisho sahihi ya kupambana na maadui ambao kwa hakika wanatafuna mifupa ya kila nchi ya Afrika.

Nyakati ambazo mzunguko wa fedha unasuasua mitaani, utasikia IMF au taasisi za tafiti zikisema Tanzania ina fedha za ndani na za nje za kutosha na Serikali hukimbilia kujilinda ndani ya takwimu hizo ili kuwaridhisha wananchi.

Michezo ya namna hiyo ni mwiba kwa mapambano halisi ya maadui wakuu watatu wa Taifa ambao tuliyarithi kutoka kwa wakoloni, na kupitia katika mikono ya miaka 56 ya awamu mbalimbali za uongozi wa CCM.

(Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Mfuatiliaji wa Utendaji wa Serikali barani Afrika; ni Mtafiti, Mwanasheria, mwanaharakati na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi CUF. Simu; +255787536759 (Whatsup, Meseji na Kupiga)/ Barua Pepe; [email protected])