Miaka 56 ya watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora

Muktasari:

  • Mwalimu alikuwa na maana kwamba vitu hivyo vinne vinategemeana sana na kimoja kikikosekana huenda vingine hushindwa kufanya kazi. Nimeona kuwa kwa sababu wiki iliyopita Tanganyika imeadhimisha uhuru wake, makala yangu ya leo iwape wasomaji nafasi ya kutafakari falsafa ya maendeleo ya taifa kwa mujibu wa fikra za Mwalimu.

Moja ya falsafa muhimu zitakazodumu, ambazo ziliwekwa na Mwalimu Nyerere ni ile imani yake juu ya uwepo wa maendeleo na sababu za maendeleo hayo. Mwalimu alisema ili nchi iendelee na ipate maendeleo inahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Mwalimu alikuwa na maana kwamba vitu hivyo vinne vinategemeana sana na kimoja kikikosekana huenda vingine hushindwa kufanya kazi. Nimeona kuwa kwa sababu wiki iliyopita Tanganyika imeadhimisha uhuru wake, makala yangu ya leo iwape wasomaji nafasi ya kutafakari falsafa ya maendeleo ya taifa kwa mujibu wa fikra za Mwalimu.

Na ifahamike kwamba mambo manne aliyoyataja Mwalimu hakuyataja kwa kubahatisha wala hakuyataja kirahisi – kiuhalisia Mwalimu aliyataja kwa uzito wa kipekee na alitaka viongozi wote watakaofuata wajipime kimaendeleo kwa kuzingatia masuala hayo. Katika makala ya leo tunazungumzia mambo mawili; watu na ardhi.

WATU

Watu ndiyo kila kitu kuhusu dunia na unapowataja unazungumzia watu ambao watakuwapo kudhibiti dunia na kuifanya dunia iwe vile wanavyotaka. Kukiwa na watu ambao watataka kuiharibu dunia basi itaharibika, kukiwa na watu watakaotaka kuitengeneza dunia basi itatengenezeka. Mwalimu aliamini watu ndiyo msingi wa kila kifanyikacho na kwa hiyo Taifa kama Tanzania linayo sababu ya kutengeneza watu watakaoifanya Tanzania iwe mahali salama pa kuishi. Kwa hiyo ili utengeneze Tanzania salama unahitaji kuwa na watu salama na hao ndiyo kipimo cha maendeleo ya Taifa.

Kwa miaka 56 ya uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) tunaweza kujiuliza ni kwa kiasi gani tumetengeneza taifa salama na watu salama. Sifa za watu salama ambazo zinaweza kuwa kipimo cha watu ni utu, uadilifu, uzalendo, umoja, uchapakazi, kujituma, kujitolea na mambo kama hayo. Kwa kiasi kikubwa Mwalimu Nyerere alitusaidia kujenga sehemu kubwa ya masuala hayo, watu waliojengwa chini ya Mwalimu walikuwa watu wanaopaswa kujua kuwa taifa linahitaji kuwa moja, lisilo na ubaguzi wala utengano, lenye umoja na mshikamano na lisiloamini katika ukabila, dini, utajiri, umasikini na hali yoyote ile iwayo.

Mwalimu alituachia kazi ya kuendelea kuwajenga watu, wawe watu wa kisasa lakini watakaozingatia kanuni muhimu za utu wema. Leo tunaweza kujipima juu ya aina ya watu tulionao, wakoje? Maana, kimsingi lazima tukubaliane kuwa Mwalimu alisema ili taifa letu liendelee linahitaji watu kama kitu cha kwanza. Basi mbona watu tunao, wako zaidi ya Milioni 55, kwa nini taifa letu halina maendeleo ya kuridhisha huku limekamilisha hitaji la kwanza la maendeleo ambalo ni “watu?” Jibu la swali hili ni rahisi, watu tunao lakini hawafuati kanuni na mahitaji ya utu wa mtu kwa ajili ya maendeleo ya mtu.

Sehemu kubwa ya hawa watu milioni 55 wanakosa sifa muhimu za kuendeleza taifa, huyu hana elimu nzuri, huyu hana uelewa, huyu hana maadili, huyu si mchapakazi, huyu si mzalendo, huyu hawezi kujitolea, huyu hawezi hiki na huyu hawezi kile. Naamini kuwa tungeliweza kutimiza ndoto za Mwalimu ikiwa tungeliweza kutengeneza watu watakaokuwa kwenye mchakato wa kulisaidia taifa kila dakika na sekunde, lakini leo tunalo taifa ambalo lina vijana wasio na matumaini, wasio na ajira, waliokata tamaa, wengine wanaopenda anasa kuliko kujishughulisha, walevi, watumiaji wa dawa za kulevya na sifa nyingine nyingi za kipuuzi.

Kama “watu” ni hitaji mojawapo la maendeleo, basi Tanzania inao watu wasiotumika kuleta maendeleo na wasioandaliwa mazingira ya kujiletea maendeleo – kwa hiyo tunaendelea kuwa taifa lenye “watu” jina na si “watu” kwa maana ya maendeleo.

ARDHI

Ardhi ni msingi wa maisha na kwa hiyo watu wanaitawala ardhi na kuifanya ilete matunda yatakayosaidia mustakabali mwema wa watu. Mwalimu Nyerere aliweka “ardhi” kama hitaji mojawapo la maendeleo kwa mantiki kwamba vizazi vyote vitaienzi ardhi na kuigeuza kuwa fursa ya kutengeneza mataifa salama na bora zaidi kwa vizazi vinavyofuatia.

Kwa miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika, ardhi imetelekezwa na haijaleta matunda yaliyokusudiwa na Mwalimu, hili haliigusi Tanzania tu bali Afrika nzima. Kaulimbiu ya Mwalimu Nyerere ya Kilimo ni uti wa mgongo inakosa uzito wake japokuwa bado kilimo ndiyo chanzo chanzo kikuu cha kipato cha takribani asilimia 70 – 75 ya Watanzania.

Takwimu za taasisi za wadau wa kilimo kwa mwenendo wa bajeti ya wizara ya (za) kilimo, mifugo na ufugaji kwa pamoja, zinaonyesha kuwa wastani wa bajeti ya wizara za sekta hizo kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita 2007 – 2016, ni chini ya asilimia 2.5 ya bajeti ya taifa. Hapo hatujafanya uchambuzi wa kibajeti wa mwaka 1961 tulipopata uhuru hadi mwaka 2006. Bajeti hii ni ndogo mno na inafifisha wosia wa mwalimu Nyerere kuwa ardhi ni moja ya nguzo nne za maendeleo.

Wakati tunatimiza miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika kwa kweli hatujafanikiwa kupandisha bajeti na uwezekezaji kwenye kilimo wala hadi kufika asilimia 10 ambayo iliridhiwa na Serikali kwenye ‘Azimio la Malabo’. Ikiwa kilimo, sekta ambayo inategemeza maisha ya asilimia 75 ya Watanzania wote inatengewa chini ya asilimia 2.5 ya bajeti ya taifa, taifa letu haliwezi kuwa linaelekea mahali sahihi!

Kilimo kilichokuwa kinazungumzwa na Mwalimu ni kile ambacho kitachangia pato la taifa kwa kiwango cha juu, kwa bahati mbaya hadi sasa pamoja na robo tatu ya Watanzania kukitegemea, bado kinachangia asilimia 28 katika pato la taifa kwa kujumuisha uvuvi na ufugaji. Baada ya kutimiza miaka 56 ya uhuru, ni wazi kuwa changamoto ya wazi iliyobakia mikononi mwetu ni kupandisha thamani na uwekezaji katika matumizi ya ardhi yenye tija.

Katika kilimo tunawajibika kujenga miundombinu ya kutosha ya kilimo cha umwagiliaji ambacho kitasaidia kuepuka matatizo ya mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa isiyo rafiki kwa kilimo. Miundombinu hii inapaswa kwenda sambamba na utoaji taarifa na elimu ya kutosha kwa wakulima wa Tanzania. Ukisikiliza hata redio zetu na televisheni zetu za umma, zinatumia muda kidogo sana kutoa taarifa za kuelimisha wananchi na wakulima juu ya kilimo bora na cha kisasa. Vipindi vinavyohusu kilimo ni vichache mno, matangazo ya hamasa kuhusu kilimo bora hayajulikani na wakulima wameachwa wajilimie wajuavyo. Ikiwa hatutabadilisha mienendo yetu ya aina ya kilimo tunachofanya, ndoto za Mwalimu Nyerere kwamba ardhi ni nyenzo muhimu ya kuleta maendeleo itakosa maana.

Tunafahamu kwamba ardhi ni pamoja na maliasili, vivutio, madini, uvuvi, ufugaji na mambo kama hayo. Miaka 56 ya uhuru wa Tanganyika haya ni masuala tunayopaswa kuendelea kujiuliza tumeyatendea haki kwa kiasi gani. Mara kadhaa imeshasemwa, Mwalimu Nyerere alijua kuwa kwenye ardhi kuna madini mbalimbali na wakati wake akajua hakuwa na wataalamu wa kutosha wazawa na wazalendo wanaoweza kusimamia rasilimali hizo. Mwalimu akachelewesha michakato ya kufungulia wawekezaji wengi wa madini ili kuepuka nchi kuwa na mashimo kwa sababu wawekezaji wangeliweza kutumia faida ya Tanzania ya wakati huo kutokuwa na wataalamu wa kutosha na wangejichotea madini watakavyo.

Mfano huo wa Mwalimu unamaanisha kuwa ardhi ni kila kitu, ni uhai na ni utajiri. Mwalimu angelikuja leo hii, miaka 56 baada ya uhuru na kujionea mashimo yalivyotapakaa Mererani, Geita, Tarime, Buhemba na kwingineko wakati maeneo hayo yana hali mbaya sana kiuchumi na tena angeliulizia serikalini na kugundua kuwa hata Serikali haikuwa inakusanya kodi ya maana kutoka kwenye madini, angelisikitika sana na angeridhika kuwa hatukuwahi kuweka mipango sahihi ya kuifanya ardhi kuwa nguzo ya maendeleo.

Katika mazingira haya haya tunaweza kuiangalia sekta ya utalii ambayo pia inatokana na uwepo wa ardhi. Ni kwa kiasi gani taifa letu baada ya miaka 56 ya uhuru limeweza kufanya mapinduzi kwenye sekta ya utalii. Bado tuna safari ndefu kabisa, tumekuwa taifa la kupokea watalii wengi wasiochangia fedha za kutosha kwa sababu hatujaweka mikakati ya kutosha ya kuifanya sekta hiyo ilete utajiri na ajira za kutosha kwa vijana wetu. Amani na utulivu vilivyoko Tanzania vilikuwa ni tunu muhimu ya kutusaidia kuwekeza kwenye utalii na kupata mabilioni ya dola – miaka hii 56 inashuhudia kusuasua. Kwa hiyo bado ndoto ya Mwalimu ya kuitumia ardhi kama nyenzo muhimu ya maendeleo, haijafikiwa.

Jumapili ijayo tutagusa mambo mawili yaliyobakia; siasa safi na uongozi bora.

(Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Mfuatiliaji wa Utendaji wa Serikali barani Afrika; ni Mtafiti, Mwanasheria, mwanaharakati na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi CUF. Simu; +255787536759 (Whatsup, Meseji na Kupiga)/ Barua Pepe; [email protected])