Miaka mitano haiwatoshi mnatafuta balaa

Muktasari:

  • Katika mifumo ya demokrasia za juu (High Democracy) suala la kiongozi kukaa madarakani huzua hisia kali sana na halichezewi.

Hivi karibuni mbunge wa jimbo la Chemba na mwanahabari wa siku nyingi, Juma Nkamia, alitoa notisi kwa uongozi wa Bunge la Tanzania ili kukamilisha mpango wake wa kuwasilisha muswada binafsi wa sheria ambao utapelekea Katiba ya Tanzania ifanyiwe marekebisho ili kuwapa wanasiasa (madiwani, wabunge na rais) fursa ya kuongoza kwa miaka saba tofauti na utaratibu wa sasa ambapo wanasiasa hao wanakaa madarakani kwa miaka mitano tu.

Natambua Nkamia ameandika barua nyingine au amezungumza na vyombo vya habari akionyesha nia ya kuachana na hoja yake kwa maelezo kuwa ameelekezwa na viongozi wake wa juu, hili nalo linahitaji mjadala siku za mbele, maana hoja au masuala ya kufikiri kubadili au kutobadili Katiba kulingana na wakati huhitaji shauku na msukumo wa wananchi kwanza na wenye mamlaka juu ya Katiba yao ni wananchi, nilipata kujiuliza, hao viongozi wakuu wa Nkamia waliomshawishi ni “Watanzania” au ni viongozi wa CCM?

Wabunge wanajua majukumu yao?

Ubunge si kazi ya utani utani au ya mchezo mchezo, au ya kufanyia propaganda. Hii ni kazi maalumu ya kuwawakilisha wananchi na kamwe si kujiwakilisha wewe mwenyewe. Nilipoisikia hoja ile nilijiuliza mwenzetu ametumwa na wana jimbo wake, chama chake au marafiki zake? Nikajiuliza mbona yako masuala makubwa ya kikatiba ya kushughulikia kuliko kujaribu masuala yatakayoizamisha nchi kwenye utumwa mpya?

Nikajiuliza tena kwa nini mbunge ajaribu kutoa mawazo ambayo hayaendani na wakati wa sasa na tena asijali athari za mawazo yake? Kwa nchi zenye demokrasia kubwa kutushinda, unapoleta mawazo ya kulimbikiza muda na madaraka kwa wanasiasa, utapata mbinyo wa kijamii hadi ujiuzulu, unakuwa umepoteza mamlaka ya kimaadili ya kuwawakilisha wananchi wengi na wanaopenda wawe na viongozi wanaotumia muda wao vizuri madarakani katika kipindi kidogo watakachopewa.

Kitendo cha mbunge kupendekeza masuala ambayo yanajenga viashiria vya kujilimbikizia madaraka, tamaa ya kukaa madarakani muda mrefu na mawazo ya kuwa muda wa wabunge hautoshi ni cha kushtusha. Na kama Nkamia alikuwa anatania ajue kuwa ubunge si kazi ya kutania na kupitia kwake wabunge wengine wajifunze kutoibua masuala ya ajabu ajabu ambayo hayana tija kwa Taifa.

Miaka saba ni dalili za uimla

Kukaa miaka saba madarakani ni dalili za uimla na udikteta uliopitiliza, ni kujenga milki ya kifalme na kimalikia au kichifu katika mfumo wa kidemokrasia. Ni kuondoa fursa ya kuleta mawazo mapya yanayotoka kwa mabadishano ya vizazi katika utawala na uongozi wa nchi na ni kujenga Taifa litakalopitwa na wakati kwa kuendelea kufanya mambo yale yale kupitia watu wale wale kwa muda mrefu, hoja za namna hiyo zinapaswa kuwekwa ndani ya taasisi za hiyari tu kama vyama vya siasa na hao nao wataingia kwenye matatizo makubwa ikiwa hakuna chaguzi za mara kwa mara za kuwafanya waamue ikiwa viongozi waliopo waendelee au la!

Katika mifumo ya demokrasia za juu (High Democracy) suala la kiongozi kukaa madarakani huzua hisia kali sana na halichezewi.

Suala la unaingia madarakani lini na kutoka lini liko katikati na tena kwa wenzetu miaka michache sana ya kukaa madarakani ina maana kubwa. Nakumbuka Barack Obama aliingia madarakani mwaka 2008 na kumaliza kipindi chake cha miaka minne mwaka 2012, alikuwa tayari amezeeka na kuchoka kweli kweli.

Uchokaji wa Obama unatokana na ukubwa wa majukumu ya uwakilishi wa wananchi ambayo hayana muda maalumu. Na hata Obama alipostaafu baada ya kuhitimu miaka minne mara mbili amenukuliwa akisema kazi ya uwakilishi si ya kukimbilia.

Obama anaeleza ni namna gani kuwa mbali na familia yake ambayo iko kwake kulikuwa kunampa shida kubwa lakini hakuwa na namna.

Kifalsafa hapa anatueleza kuwa muda wa miaka minne kuiongoza Marekani kwake ulikuwa ni karne nne. Ndipo unastaajabu sana ukija Afrika na Dodoma ambako Juma Nkamia anataka wabunge na marais waongoze walau mara mbili ya muda ambao Obama ameukimbia wa awamu moja ya miaka minne. Hii miaka saba ya Nkamia kama ndiyo ingelikuwa kwenye uongozi wa Marekani basi nadhani mtu kama Obama asingelijaribu kuomba mingine saba ya pili!

Kiongozi akikaa miaka saba madarakani anakuwa mfalme au malkia, anakuwa amewamiliki wananchi wake na anakuwa na muda mrefu wa kulala na kula raha kuliko kuwahudumia wananchi. Wabunge na wawakilishi ukiwapa miaka saba ya kukaa madarakani watu wataingia tu na kuchuma kisha waondoke, hakutakuwa na siasa wala demokrasia katika nchi yetu.

Wapo watu wanatetea msimamo wa Nkamia kwa kulinganisha na utaratibu wa kukaa madarakani nchini Rwanda ambapo uchaguzi wa Rais unafanyika kila baada ya miaka saba. Rwanda ni Taifa ambalo hatupaswi kulitolea mifano wakati tunazungumzia demokrasia, Rwanda ni nchi ambayo demokrasia ni adui na ukuu wa Rais wa nchi yao ndiyo kipaumbele.

Unapotaka kuilinganisha Tanzania katika demokrasia kwenye uwanda wa dunia lazima uzitizame nchi za magharibi ambako tumekuwa tukijifunza mifumo hiyo au utizame nchi za Afrika zilizopiga hatua ikiwemo Afrika Kusini, Nigeria, Ghana, Kenya.

Tukiichoka amani tunatafuta balaa

Hoja ya ukomo wa madaraka ya wanasiasa kuwa miaka saba ni kulilia balaa na ni kuziweka nchi za Afrika katika rehani ya wanasiasa wachache na kuzitoa kwenye mamlaka ya wananchi japo tunafahamu kuwa nchi nyingi kati ya hizo zinapigania ukuu wa wananchi hata katika Katiba za sasa za chaguzi za kila baada ya miaka mitano.

Mabalaa tunayoyatafuta yatakuwa yanahusisha pia kujiingiza kwenye vita za wenyewe kwa wenyewe, majaribio ya kupindua Serikali na chuki za hali ya juu kati ya wanasiasa na wananchi. Kwa kawaida na kisaikolojia, wananchi hufikia wakati fulani wakawachoka twawakilishi wao na wanapomchoka mwakilishi wanaingia kwenye matatizo makubwa ya kimahusiano na kimaendeleo hususani kwa nchi zenye maeneo makubwa na zinazohitaji uchumi mkubwa kama Tanzania.

Hoja ya wanasiasa wa Tanzania kuongoza miaka saba inapaswa kuonywa na isidharauliwe. Nkamia ni mwana CCM mzuri na huwezi kujua ametumwa na nani kuishadidia kwa siku kadhaa kabla ya kusema kuwa anaiondoa.

Huenda tayari ni mashauriano ambayo anayafanya na wabunge wenzake wa CCM na hatujui hoja hiyo kama ilikuwa ni utani ni wa namna gani na kiwango kipi; jambo la msingi hapa ni kuendelea kuonya kuwa nchi yetu ina vipindi vya kukaa madarakani ambavyo vinatosha kwa sasa, kuviongeza ni kuleta shida.

Nusu ya wabunge huchokwa ndani ya miaka miwili

Uzoefu wangu wa kuzungumza na wananchi unaonyesha kuwa huwa wanamchoka mwakilishi wao ikiwa hatimizi wajibu wake ndani ya mwaka mmoja hadi miwili. Ndiyo maana wakati wabunge wetu wanatimiza miaka miwili mwaka huu 2017 tunafahamu kuwa yapo majimbo mengi tu ambayo wananchi wanatamani kurudi kwenye uchaguzi hata leo ili wawatupe nje wawakilishi wao ambao hawajitambui.

Viongozi wa CCM wenyewe wamewahi kuzunguka nchi wakihubiri kuwa Baraza la Mawaziri chini ya Rais Jakaya Kikwete lilijaa mizigo, walikuwa wanajuta kuwa na viongozi wa namna hiyo kwenye utawala wa nchi. Kwa mujibu wa Katiba yetu mawaziri wanatokana na wabunge na sasa kama mawaziri ni mizigo kiasi hiki vipi ule uzao wao, bunge? Kwa nadharia hiyo rahisi tukubaliane kuwa tuna wabunge wengi mizigo na ndiyo maana kila baada ya uchaguzi mmoja walau nusu yao huwa hawarudi tena bungeni, mizigo hiyo ndiyo huhitaji kukalishwa madarakani miaka? Si inakuwa ni kutafuta mateso kwa wananchi?

Ikiwa tutajenga fikra za uongozi wa miaka saba wananchi watakuwa wanashinda makanisani na misikitini wakiombea mbunge fulani afe haraka! Tutajenga nchi ya chuki na kukosa ridhiko. Kwa Rais wa nchi ndiyo usiseme, atachokwa si tu na wananchi, bali mihimili mingine ya dola inayofanya kazi naye, vyombo vya ulinzi na usalama vitaanza kugawanyika.

Ndiyo maana huko nchini Rwanda kila kukicha wapo majenerali wa kijeshi ambao wanakimbilia uhamishoni kwa kukosana na Kagame na wengine anawawinda hadi wawapo nje ya Rwanda. Kumweka mtu kwenye ngazi ya utendaji wa nchi kwa miaka saba ni kutafuta balaa, tena balaa kubwa!

(Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Mfuatiliaji wa Utendaji wa Serikali barani Afrika; ni Mtafiti, Mwanasheria, mwanaharakati na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi CUF. Simu; +255787536759 (Whatsup, Meseji na Kupiga)/ Barua Pepe; [email protected])