Miamba 16 ya Ligi Kuu Tanzania Bara hii hapa

Muktasari:

Makala hii inakuletea uchambuzi wa vikosi vya timu 16 zitakazoshiriki Ligi Kuu msimu ujao wa 2016/2017.

Dirisha la usajili kwa timu za Ligi Kuu, limefungwa rasmi Agosti 6 baada ya mchakamchaka wa hapa na pale kwa wachezaji kutoka eneo moja kwenda lingine.

Baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu msimu wa 2015/16 wapo wachezaji waliotimka timu zao na kuhamia nyingine, waliostaafu, waliobaki na wapo wachezaji pamoja na kusajiliwa wamejihakikishia namba.

Makala hii inakuletea uchambuzi wa vikosi vya timu 16 zitakazoshiriki Ligi Kuu msimu ujao wa 2016/2017.

 

1.Azam FC

Baada ya kushika nafasi ya pili msimu uliopita, Azam ilifanya mabadiliko kwenye benchi lake la ufundi kwa kumleta kocha, Zeben Hernandez kutoka Hispania aliyerithi mikoba ya Stewart Hall aliyeondoka.

Hall amekuwa akiingia na kutoka mara zote Azam, na humchukua inapotokea mambo yameharibika. Timu hiyo imewaacha wachezaji kadhaa akiwemo kipa, Ivo Mapunda, Khalid Mahadhi, Said Morad, Racine Diouf, Didier Kavumbagu, Joseph Kimwaga na Allan Wanga.

Katika kujiweka sawa na msimu wa 2016/17, Azam imeimarisha kikosi chake kwa kuwasajili wachezaji wanne wa kigeni, Daniel Yeboah, Enock Agyei, Daniel Amoah na Julius Kangwa.

Lengo kuu ni kutwaa ubingwa utakaowawezesha kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2018.

Hernandez anasema anataka kuona Azam inafanya vizuri, si katika Ligi Kuu, bali hata mashindano mengine ngazi ya klabu Afrika.

 

2.African Lyon

Imepanda Ligi Kuu msimu huu baada ya kupambana kwa misimu minne mfululizo kwenye Ligi Daraja la Kwanza. Timu hiyo ilishuka daraja msimu wa 2013/14.

Pamoja na hayo, Lyon imeingia na mguu wa bahati kwenye Ligi Kuu baada ya kupata udhamini wa kituo cha redio cha Choice FM.

Imewasajili wachezaji wachache tu ambao ni kiungo Abdulhalim Humud, Hamadi Manzi, Jerry Tegete na Adam Kingwande. Msimu ujao timu hiyo itanolewa na kocha wa zamani wa Simba, Dragan Popadic ambaye aliiongoza Simba kufanya vema katika michuano ya Afrika Mashariki na Kati mwishoni mwa miaka ya 90.

 

3.Ndanda FC

Ilimaliza ligi msimu uliopita ikiwa nafasi ya tisa, lakini imeondokewa na wachezaji wake tegemeo wa kikosi cha kwanza walioipa mafanikio.

Baadhi ya wachezaji hao ni Atupele Green, Cassian Ponela na William Lucian ‘Gallas’.

Katika harakati zake za kujiimarisha imeinasa saini ya kiungo wa zamani wa Yanga, Salum Telela lakini ina kazi kubwa ya kufanya msimu ujao ili iweze kubakia kwenye Ligi Kuu kwani mpaka sasa haina kocha baada ya kocha mkuu, Malale Hamsini kutimkia JKT Ruvu.

 

4. JKT Ruvu

Baada ya kuponea chupuchupu kushuka daraja msimu uliopita, timu imeongeza nguvu kwenye benchi lake la ufundi kwa kumchukua kocha Malale Hamsini aliyekuwa akiinoa Ndanda FC.

Timu hiyo iliyomaliza ikiwa ya 11, imeimarisha safu yake ya ushambuliaji kwa kumsajili mchezaji Atupele Green kutoka Ndanda FC.

Pia, imewaacha wachezaji Gaudence Mwaikimba, Mussa Kidu na Abdulrahman Musa. Ni dhahiri malengo yao makubwa ni kuhakikisha inafanya vizuri msimu ujao.

 

5. Ruvu Shooting

Baada ya kushuka daraja msimu wa 2014/2015, timu hiyo imepambana na kufanikiwa kurudi Ligi Kuu kwa kishindo ikishinda mechi 12 kati ya 15 ilizocheza kwenye ligi daraja la kwanza.

Katika kuimarisha kikosi chake, imewatema wachezaji Ally Khan, Yahaya Tumbo, Juma Mpakala, Rashid Gumbo, Kulwa Mobi, Gideon Sepo, George Osei na Chagu Chagula.

Nafasi za wachezaji hao zimezibwa na wachezaji Chande Magoja, Fuluzuru Maganga, Shaibu Nayopa, Abdulrahman Musa, Renatus Kisasa, Jabir Aziz, Peter Richard, Clider Loita na Elias Emannuel.

Pia, iliachana na kocha wake wa muda mrefu, Tom Olaba na kumteua mzawa, Selemani Mtingwe kurithi mikoba yake. Timu hiyo inaonekana kuja kivingine msimu ujao kwa kuchukua wachezaji wengi zaidi raia tofauti na zamani ilikuwa ikiwatumiwa wanajeshi pekee.

 

6.Toto Africans

Imepata pigo kubwa baada ya kuondokewa na nusu ya nyota wake wa kikosi cha kwanza waliotimkia timu nyingine kusaka maslahi bora zaidi.

Baadhi ya nyota waliotimka ni Hassan Hatib, Musa Kirungi, Yassin Mpilipili, Abdallah Seseme, Edward Christopher na Carlos Protas.

Kutokana na hali ya ukata inayoikabili, timu hiyo imemsajili mchezaji mmoja tu wa maana ambaye ni Frank Sekule kutoka Majimaji.

Kwenye msimu ujao wa ligi itaongozwa na kocha Rogasian Kaijage aliyerithi mikoba ya John Tegete aliyetimka timu hiyo tangu alipochukua mikoba 2013.

 

7. Prisons

Ilifanya vizuri msimu uliopita baada ya kumaliza Ligi Kuu ikiwa kwenye nafasi ya nne na pointi 51.

Ina kazi kubwa ya kuweza kumaliza zaidi ya nafasi ya nne msimu ujao. Pamoja na mafanikio hayo, timu hiyo imemeguka baada ya kuondokewa na kocha wake, Salum Mayanga aliyekwenda Mtibwa huku pia ikiondokewa na mchezaji wao tegemeo, Mohammed Mkopi aliyesajiliwa Mbeya City.

Katika kujiimarisha, wamemchukua kocha Abdul Mingange na wachezaji Kazungu Nchinjayi na Mohammed Samatta.

Wamefanikiwa kumbakiza beki tegemeo, Salum Kimenya ambaye alikuwa anawindwa na Simba.

 

8.Mwadui FC

Wakiwa chini ya kocha mwenye maneno mengi, Jamhuri Kihwelo Mwadui wameweka malengo ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu msimu ujao. Imefanya uamuzi mgumu wa kuwatema wachezaji Jerry Tegete, Athuman Idd ‘Chuji’, Jabir Aziz, Razack Khalfan na Nizar Khalfan.

Nafasi zao zimezibwa na Abdallah Seseme, Abdallah Mfuko, Yassin Mustafa, William Lucian, Salum Kanoni na Said Nassor ‘Chollo’

 

9. Majimaji

Inatakiwa ifanye kazi ya ziada msimu ujao ili iweze kubakia kwenye Ligi Kuu vinginevyo itakwenda na maji.

Majimaji inaingia kwenye msimu mpya wa ligi bila kocha wake, Kally Ongalla ambaye aliisaidia kutoshuka daraja msimu uliopita.

Kocha huyo amemaliza mkataba wake, lakini baada ya kutoa masharti ya yeye kurudi, timu hiyo iliyakataa.

Mbali na kocha, timu hiyo imeondokewa na wachezaji Frank Sekule, Dan Mrwanda, David Burhan, Godfrey Taita na Kazungu Nchinjayi na imewasajili beki Ernest Mwalupwani na ikiwaongezea mikataba wachezaji Alex Kondo na Marcel Kaheza.

 

10. Mtibwa Sugar

Lengo lao kila mwaka ni kumaliza wakiwa kwenye nafasi nne za juu ingawa msimu uliopita hawakutimiza na walimaliza wakiwa nafasi ya tano.

Wamemrudisha kocha wa zamani, Salum Mayanga anayeziba pengo lililoachwa na Mecky Mexime aliyekwenda Kagera Sugar.

Kama inavyosifika kwa kuzizalishia timu za Simba na Yanga wachezaji, safari hii Mtibwa imeondokewa na wachezaji Andrew Vincent, Shiza Kichuya, Muzamiru Yassin na Mohammed Ibrahim waliosajiliwa na timu hizo.

Mapengo yao yamezibwa na wachezaji Rashid Mandawa, Haruna Chanongo, Cassian Ponela na Benedictor Tinoco.

 

11. Stand United

Imekuwa na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe ambayo inatoa taswira mbaya kwa timu hiyo kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu.

Kuna uongozi wa timu hiyo wa aina mbili, kuna waasisi na wajaji. Waasisi wametaka kubakia na timu wakati wajaji wamekuwa wakijitangaza kuwa wao pia wana sauti ndani ya klabu.

Pia wamemtimua kocha Patrick Liewig kwa kilichoelezwa kushindwa kuivusha timu ambayo ilimaliza msimu uliopita ikishika nafasi ya saba na pointi 40.

Viongozi kwa mgawanyiko wao, wameimarisha kikosi chao kwa kuwasajili wachezaji, Yusuph Mpilipili, Adeyum Ahmed na Chidiebere Abasilim huku wakiondokewa na Haruna Chanongo. Iwapo watamaliza migogoro, wanaweza kufanya vizuri msimu ujao hasa wakichagizwa na udhamini mnono kutoka kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia.

 

12. Kagera Sugar

Ikionekana kujifunza kutokana na makosa yaliyojitokeza msimu uliopita ambapo iliponea kwenye tundu la sindano, Kagera Sugar imefanya maboresho makubwa kwenye kikosi chake.

Kwanza imeimarisha benchi la ufundi kwa kumchukua kocha Mecky Maxime atakayesaidiwa na Ally Jangalu na Musa Mbaya ‘Moloto’

Kikosi chake kimeongezwa sura nyingi mpya ambazo ni wachezaji; Hussein Sharrif, Themi Felix, Edward Christopher, Hassan Hatib, Anthony Matogolo, Dan Mrwanda, David Burhan na Godfrey Taita.

 

13. Mbeya City

Lengo lao ni kurudi kwenye nafasi nne za juu kama walivyofanya msimu wa 2013/2014.

Wamewabakiza nyota wao wote muhimu huku wakiwaongeza Ayoub Semtawa, Mohammed Mkopi na Rajab Zahir.

Wataendelea kuwa chini ya kocha Mmalawi Kinnah Phiri ambaye aliifanikiwa kuifanyia mabadiliko makubwa timu hiyo ndani ya muda mfupi.

 

14. Yanga

Tofauti na nyakati zilizopita, mwaka huu hawakusajili kundi kubwa la wachezaji kama ilivyozoeleka. Imewaongeza wachezaji wanne ambao ni Hassan Kessy, Andrew Vincent, Juma Mahadh na Obrey Chirwa.

Pia, haijaacha wachezaji wengi kwani walioondoka ni watatu tu ambao ni Paul Nonga, Salum Telela na Benedictor Tinoco.

Lengo lao kuu kutetea ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya tatu mfululizo.

 

15.Simba

Baada ya kuhaha kwa misimu minne mfululizo bila mafanikio, safari hii Simba inaonekana imepania kuutwaa ubingwa kwa kuwa na hamu hiyo baada ya misimu minne.

Imefanya usajili wa aina yake ambao pengine unaweza kumaliza kiu yao ya kutotwaa ubingwa kwa muda mrefu.

Simba ambayo haijashiriki hata Kombe la Kagame kwa muda mrefu, imeimarisha benchi la ufundi kwa kumleta kocha Joseph Omog akisaidiwa na Jackson Mayanja huku ikisajili wachezaji Shiza Kichuya, Moussa Ndusha, Frederick Blagnon, Method Mwanjali, Mohammed Ibrahim, Muzamiru Yassin, Jamal Mnyate, Emannuel Semwanza, Hamad Juma na Laudit Mavugo. Wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri msimu ujao iwapo kutakuwa utulivu kwa viongozi, wanachama na mashabiki wake ambao mara nyingi wamekuwa wakikosa uvumilivu pindi inapofanya vibaya.

 

16. Mbao FC

Haijafanya usajili mkubwa na imeamua kutumia wachezaji wake wengi ambao waliiwezesha timu hiyo kupanda Ligi Kuu kwa ajili ya msimu ujao. Mchezaji wa maana aliyesajiliwa ni kipa wa zamani wa Toto Africans, Erick Ngwegwe.

Pia wameimarisha benchi la ufundi kwa kumuajiri kocha kutoka Burundi, Ndairagije Etienne.