ELIMU NA MALEZI : Michezo inavyokuza uwezo wa mtoto kiakili-1

Muktasari:

Katika kuhakikisha kwamba watoto wanaelekeza nguvu zao katika masomo, zipo shule huamua kupunguza au kuondoa kabisa michezo.

        Imeanza kuaminika kuwa michezo na masomo haviwezi kwenda pamoja. Wazazi na walimu wanaichukulia michezo si tu kama upotevu wa muda wa mtoto, lakini pia inaathiri uzingatiaji katika masomo.

Katika kuhakikisha kwamba watoto wanaelekeza nguvu zao katika masomo, zipo shule huamua kupunguza au kuondoa kabisa michezo.

Itakumbukwa miaka ya nyuma kiongozi fulani, aliamua kufuta mashindano ya michezo katika ngazi za shule ya msingi na sekondari, kwa hoja kwamba michezo inawapotezea muda wanafunzi.

Vuguguvu hilo la kufuta michezo lilienda sambamba na msisitizo wa shule za msingi na sekondari kuongeza ufaulu. Ndio kusema wakubwa wa elimu waliamini kuwa kufuta mashindano hayo ya michezo shuleni kungepandisha taaluma katika shule zetu. Hata hivyo, baadaye uamuzi huo ulibatilishwa.

Michezo na ujifunzaji

Katika malezi na makuzi ya mtoto, umri wa mpaka miaka 12 hauwezi kutenganishwa na michezo. Karibu kila anachojifunza mtoto kuhusu mazingira yake, kinategemea na aina ya michezo anayoshiriki.

Ni kwa sababu hiyo, walimu wa ngazi za awali za elimu, wanafundishwa mbinu za kubuni michezo ya aina mbalimbali kuwasaidia watoto kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu.

Katika makala haya, tunaichukulia michezo kama vitendo vinavyoshughulisha viungo vya mtoto kwa lengo la kumburudisha, kushindana na kujifunza mambo mapya.

Kwa mfano, mtoto anapotumia mikono na vidole vyake kurusha na kuudaka mdako, tunaweza kusema anashiriki michezo kwa sababu kwanza anashughulisha viungo vyake na pili analenga kufikia lengo la kumshinda mwenzake.

Mbali na kuboresha afya ya mtoto, tutazame namna michezo isivyoweza kutenganishwa na ujifunzaji wa mtoto.

Umakini

Michezo inaongeza umakini wa mtoto katika kufuatilia kile anachokifanya. Umakini ni ubora wa mawasiliano kati ya viungo vya mwili wake katika kufikia malengo ya mchezo husika.

Kwa mfano, mtoto anayecheza mchezo wa ‘rede’ inambidi kuwa na uwezo mzuri wa kuona na kufuatilia mwenzake mwenye mpira ataurusha wapi.

Bila uwezo mzuri wa kubashiri mwelekeo wa mpira, itakuwa vigumu kwake kuukwepa wakati huohuo akiendelea kujaza mchanga kwenye chupa inayotakiwa kujaa ili kumpa ushindi.

Umakini ni sifa muhimu katika masomo. Ili mwanafunzi afanikiwe lazima awe na uwezo wa kufuatilia kwa makini kile kinachosemwa na mwalimu; awe na uwezo wa kutumia macho na masikio yake kuchunguza wakati anapohitajika kufanya majaribio.

Kwa hiyo, utaona, mtoto anayepewa muda wa kucheza michezo inayokuza umakini wake anakuwa na nafasi ya kuwa makini darasani kuliko mwenzake asiyeshiriki michezo.

Ushirikiano

Michezo mingi inafanyika kwa ushirikiano wa watoto wengine. Mara nyingi lengo linakuwa kushindana kwa maana ya kujua nani anaweza kufanya vizuri zaidi ya mwingine.

Katika kucheza, mtoto atajifunza namna ya kupanga mikakati ya ushindi akiwa na wenzake. Katika kupanga mikakati, mtoto hujifunza mawazo mapya, hujifunza kukubali kwamba naye, kwa wakati mwingine, anahitaji kuachana na wazo lake na kufanyia kazi mawazo ya wengine.

Uwezo huu ni muhimu katika kujifunza. Ili mwanafunzi aelewe masomo yake vizuri, analazimika kusikiliza mawazo ya watu wengi. Bila uwezo wa kuvumilia mawazo asiyokubaliana nayo, itakuwa vigumu kwa mwanafunzi kufanya vizuri.

Lakini pia, katika kushindana na timu pinzani, mtoto hujifunza kwamba kuna kushinda na kushindwa. Maumivu ya kushindwa ni mtaji muhimu anaouhitaji mtoto katika maisha ya taaluma. Bila michezo, somo la kujifunza kushindwa linaweza kuwa gumu kueleweka.

Kufikiri kwa haraka

Kufikiri ni mtaji muhimu katika michezo. Ipo michezo mingi inayohitaji uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi kwa haraka na kwa wakati.

Kwa mfano, watoto wanapocheza mchezo wa mpira wa miguu, wanahitaji kufanya maamuzi muhimu kwa haraka. Lazima mtoto ajue mpinzani wake yuko wapi na anafikiri kufanya nini ili ajue cha kufanya kitakacholeta mafanikio kwa timu yake.

Vivyohivyo katika michezo mingine mingi. Bila uwezo wa kufanya maamuzi ya haraka, mtoto hawezi kushinda.

Uwezo huu wa kufikiri kwa haraka unatumika darasani. Mtoto anayeweza kufanya maamuzi muhimu kwa wakati, mara nyingi ndiye anayefanikiwa zaidi.

Ubunifu

Michezo inahitaji ubunifu mkubwa. Wakati mwingine mtoto atahitaji kutumia vifaa vinavyopatikana katika mazingira yake na kuvigeuza vikidhi mahitaji ya mchezo unaokusudiwa.

Mathalani, katika mazingira ambayo watoto hawapati mipira iliyotengenezwa, watoto wanaweza kutumia mchanganyiko wa vipande vya godoro, nguo kuukuu na kamba kutengeneza mpira unaoweza kuwasaidia kufikia malengo yao.

Pia, hata katika michezo mingine kama kuruka kamba, watoto wengi hutumia kamba za miti au zilizotengenezwa kwa kuunga vipande vya nguo kuukuu. Kazi hii ya kutengeneza kamba inakuza ubunifu kwa sababu mtoto anahitaji kutumia alichonacho kufikia lengo alilonalo.

Kwa hakika bila ubunifu, mtoto hawezi kufanya vizuri darasani. Mwalimu atampa maswali ambayo wakati mwingine hayana jibu linalofahamika waziwazi. Katika mazingira kama haya, mwanafunzi mwenye ubunifu anakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi.

Lugha na kuhesabu

Katika michezo, watoto hulazimika kuwasiliana ili waweze kukubaliana sheria za mchezo na hata kupanga mikakati ya ushindi.

Lugha kama nyenzo ya mawasiliano, ndio kiini cha mawasiliano katika michezo ya watoto. Lengo la kupata ushindi humfanya mtoto si tu ajifunze namna ya kusema mawazo yake kwa lugha inayoelewa, lakini pia kuelewa kile wanachojaribu kukisema wenzake.

Kwa namna hii watoto wanaoshiriki michezo wana nafasi kubwa ya kuwa na msamiati zaidi kuliko watoto wanaonyimwa fursa hiyo muhimu.

Aidha, kupitia michezo watoto kujifunza kuhesabu. Mchezo kama mdako, kwa mfano, unamlazimu mtoto kujua idadi ya kete anazotumia, kuhesabu mitupo ya kete anayotakiwa kuidaka. Haya yote kwa pamoja yanamjengea mtoto uwezo wa kuhesabu wakati mwingine kabla hajakwenda shule. Itaendelea