Migogoro ishughulikiwe kwa wakati kuimarisha sekta ya utalii nchini

wanawake  kutoka vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakiandamana kupinga kumegwa kwa eneo la pori tengefu  katika mji wa Wasso uliopo Loliondo,mkoani Arusha. Picha na Mussa Juma

Muktasari:

  • Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe anasema katika kipindi cha mwaka 2015, idadi ya watalii waliongia nchini ilikuwa 1,376,182 ambao walichangia Dola 1.9 bilioni za Marekani katika pato la Taifa.

Sekta ya Utalii inachangia zaidi ya asilimia 25 ya mapato ya Taifa ya kigeni, lakini hatua za makusudi zisipochukuliwa huenda migogoro ikapunguza ufanisi ulionza kujitokeza. Mapato hayo yanatokana na malipo kwa huduma mbalimbali ambazo watalii wanalipa wanapoingia nchini yanayotarajiwa kuongezeka kutokana na kuimarika kwa idadi ya watalii wanaoingia kila mwaka.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe anasema katika kipindi cha mwaka 2015, idadi ya watalii waliongia nchini ilikuwa 1,376,182 ambao walichangia Dola 1.9 bilioni za Marekani katika pato la Taifa.

Kutokana na kazi nzuri ya Serikali na wadau katika kutangaza vivutio vilivyopo nchini, idadi inaendelea kuongezeka na katika kipindi cha Julai hadi Agosti, 2016 waliongezeka kwa asilimia 11.

Waziri huyo anasema watalii wengi wanaofika nchini wanatembelea zaidi hifadhi za Taifa, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Zanzibar, wawindaji wa kitalii na wapiga picha.

Hata hivyo, anasema katika kuongeza siku za watalii kukaa nchini, bidhaa mbalimbali zinaendelea kuongezwa kwenye sekta hii ikiwamo utalii wa utamaduni na maeneo mengine yaliyohifadhiwa.

Uwekezaji

Utalii ni miongoni mwa sekta ambazo zimewavutiwa wawekezaji kutumia fursa nyingi kama vile mapori ya akiba, mapori tengefu, maeneo ya hifadhi za jamii (WMA) na mengineyo.

Karibu wilaya zote ambazo zimebahatika kuwa na vivutio vya utalii, kuna wawekezaji tofauti zikiwamo hoteli, kampuni za uwindaji na utalii wa picha. Arusha ni miongoni mwa mikoa zenye wawekezaji wengi wa utalii huku ikipewa hadhi ya kuwa kitovu cha sekta hiyo nchini.

Wawekezaji hawa, wa ndani na nje wametoa zaidi ya ajira 400,000 kwenye hoteli, magari ya kusafirisha watalii, kambi za uwindaji wa kitalii, utalii wa picha na kutembeza watalii.

Migogoro

Hata hivyo, licha ya faida kubwa ambayo inatokana na wawekezaji katika sekta ya utalii, bado kuna changamoto ya migogoro inayochangiwa na uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa, mgongano wa kisheria na ongezeko la watu na mifugo katika maeneo hayo.

Katika Wilaya ya Ngorongoro kuna mgogoro unaosababishwa na kukinzana kwa hoja ya uhifadhi wa ikolojia ya Serengeti ambayo ni mazalia ya wanyamapori na kuwapo kwa ardhi mseto katika eneo hilo.

Migogoro sasa imesababisha wawekezaji kuanza kupungua katika eneo hilo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kutoka kampuni 12 mpaka nne zilizopo sasa. Sababu kubwa ya migogoro hiyo ni kukosekana kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi, kutosimamiwa kwa sheria na mwingiliano wa matumizi ya ardhi kwa shughuli za ufugaji, utalii, kilimo na uhifadhi.

Ofisa Utalii wa Wilaya ya Ngorongoro, Elibariki Bajuta anasema kutokana na hali hiyo baadhi ya wawekezaji waliokuwa wakitoa misaada ya afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara na ajira katika Tarafa ya Loliondo wamefungasha virago na kuondoka.

Anazitaja kampuni zilizobaki kuwa ni Thomson Safari and Beyond Klein’s Camp, Ottelo Business Corporation (OBC) na Buffalo Camp ambazo kwa pamoja, katika miaka mitatu iliyopita zimechangia zaidi ya Sh11.3 bilioni.

Mkurugenzi wa OBC, Isack Mollel anasema kampuni yake inachangia zaidi ya Sh4.5 bilioni kwa halmashauri ya wilaya hiyo kutokana na uwindaji unaofanywa. OBC inamiliki kitalu cha uwindaji katika eneo la Loliondo chenye kilomita 4,000 za mraba ingawa ni kilomita 1,500 ndizo zinazotumika kwa shughuli hiyo.

Anasema kwa miaka 10 iliyopita kampuni yake imetoa mchango wa moja kwa moja kwa halmashauri ambao ni zaidi ya Sh2.26 bilioni licha ya asilimia 25 itokanayo na mapato ya uwindaji ambazo ni zaidi ya Sh2.5 bilioni.

Akifafanua mapato hayo kwa miaka mitano iliyopita, anasema kampuni ilitoa gawio la Dola 80,660 za Marekani mwaka 2012 na Dola 91,354 mwaka 2013. Kiasi hicho kiliongezeka mpaka Dola 93,556 mwaka 2014 na kufuatiwa na Dola 101,600 mwaka 2015. Mwaka jana ililipa Dola 100,009 za Marekani.

Licha ya fedha, kampuni hiyo imeshiriki kuchimba visima katika vijiji vinavyozunguka eneo la uwindaji huku ikitoa misaada mbalimbali ikiwamo ya afya na elimu.

“Kati ya mwaka 1991 hadi 2006 tumechangia kiasi cha Dola 1.6 milioni (zaidi ya Sh3.2 bilioni) katika uhifadhi pamoja na ununuzi wa magari zaidi ya 30 na silaha ili kusaidia vita dhidi ya ujangili,” anasema Mollel.

Migogoro

Serikali ya Awamu ya Tano, imekuwa na mikakati kadhaa ya kutatua migogoro kwenye maeneo ya uwekezaji, hususan sekta ya utalii kwa kuanzisha mazungumzo inayozishirikisha pande zinazokinzana kusaka suluhu, kusimamia sheria na taratibu.

Katika kutekeleza hilo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hivi karibuni alifanya ziara katika Wilaya ya Ngorongoro na kuagiza kumalizwa migogoro iliyopo na sasa vikao vya suluhu vinaendelea.

Baada ya ziara ya Loliondo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alitoa agizo la kutengwa kwa eneo la kilomita 1,500 za mraba ndani ya pori tengefu kwa ajili ya uhifadhi wa ikolojia ya Serengeti kutokana na umuhimu wake kwa masilahi ya Taifa katika uhifadhi na utalii wa maliasili.

Anasema kuliacha eneo hilo liendelee kuvamiwa ni kuiua Hifadhi ya Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambazo zina mazalia ya wanyamapori na vyanzo vya maji kwa ajili yao na wananchi wa maeneo jirani.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo anasema katika kupata suluhu, hatua waliyofikia ni nzuri kwani kamati maalumu ya wahifadhi, wataalamu wa ardhi, wawekezaji na wananchi wa vijiji husika imeundwa na kuwajumuisha katika kuhakikisha suluhu ya Loliondo inapatikana.

Anasema kuwa kuna mapendekezo mawili ambayo yamefikiwa hadi sasa. Mosi ni kutengwa kwa pori tengefu lenye ukubwa wa kilomita 1,500 za mraba na kuanzishwa kwa hifadhi ya jamii (WMA), ingawa uamuzi wa mwisho unatarajiwa kutolewa na Rais John Magufuli.

Loliondo siyo pekee yake inayokabiliwa na migogoro inayoleta athari kwa sekta ya utalii. Hifadhi ya Ruaha imekuwa kwenye ‘rabsha’ na wananchi wanaoizunguka baada ya kutangaza mipaka mipya ambayo inafika kwenye makazi ya wananchi.

Umakini unahitajika kuhakikisha njia sahihi zinatumika kutafuta suluhu kwa masilahi ya Taifa, wawekezaji na wananchi bila kuathiri shughuli muhimu hasa za kiuchumi.

Endapo migogoro iliyopo haitashughulikiwa kwa wakati, wadau wanatahadharisha kwamba huenda ikawakatisha tamaa wawekezaji wanaovutiwa na fursa zilizopo nchini.