Migogoro ya mipaka ya hifadhi imalizwe kuimarisha utalii nchini

Muktasari:

Wakati Serikali ikitekeleza mipango mbalimbali iliyojiwekea, viongozi wanapaswa kuzingatia siasa safi hasa kwenye matumizi ya ardhi huku wananchi nao wakijisimamia kuleta maendeleo kwa kutumia rasilimali hiyo na kujikwamua kutoka kwenye lindi la umaskini.

Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema ili tuendelee tunahitaji vitu vinne; ardhi, siasa safi, uongozi bora na watu. Mwalimu alimaanisha sambamba na mambo mengine, ardhi ni miongoni mwa misingi madhubuti ya maendeleo.

Wakati Serikali ikitekeleza mipango mbalimbali iliyojiwekea, viongozi wanapaswa kuzingatia siasa safi hasa kwenye matumizi ya ardhi huku wananchi nao wakijisimamia kuleta maendeleo kwa kutumia rasilimali hiyo na kujikwamua kutoka kwenye lindi la umaskini.

Kutokana na sababu tofauti, kuna migogoro mingi nchini ambayo inajitokeza kati ya wananchi na mwekezaji, halmashauri na hifadhi ya taifa, wakulima na wafugaji, halmashauri na halmashauri, kijiji na kijiji au mkoa na mkoa.

Wengi wanagombea mipaka, baadhi rasilimali kama vile maji na malisho. Haya yote yanatokea kipindi ambacho Serikali inasisitiza wananchi kufanya kazi ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa na huduma.

Machi mwaka jana, akiwa kwenye ziara ya siku tano, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwatuma mawaziri watatu mkoani Simiyu na kuwataka wakae na uongozi wa kila wilaya pamoja na wananchi ili kubaini tatizo la mipaka baina ya halmashauri za mkoa huo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Majaliwa alitoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na wakazi wa vijiji vya Mwakaluba na Mwandoya na kubainisha kwamba amekuwa akipokea malalamiko ya mipaka kila alipopita kabla hajawataka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi; Waziri wa Maliasili ua Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene kuchukua hatua.

Taarifa zilieleza kwamba kuna zuio linalowakata wananchi kufanya shughuli zozote ndani ya mita 60 kutoka kwenye kingo za Mto Simiyu bila kushirikishwa wala kuelezwa chochote zaidi ya kuona bango la matangazo tu.

Ili kukabiliana na migogoro ya ardhi nchini, Waziri Mkuu alisema Serikali ina mpango wa kuunda mabaraza 100 ya ardhi ambayo yatakuwa na jukumu la kutatua migogoro ya ardhi kwa wakati. Lukuvi pia, aliziagiza halmashauri kumaliza migogoro hiyo mpaka Desemba 31, mwaka jana.

Siyo huko pekee, wilayani Mbarali, Mbeya kuna mgogoro wa mpaka kati ya wananchi na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 sasa kutokana na upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Mgogoro huo unatokana na tangazo lililotolewa kwenye gazeti la Serikali namba 28 la mwaka 2007 ambalo linaainisha mipaka ya hifadhi hiyo ambayo wananchi hao wanaipinga kwa madai imeingia kwenye makazi na mashamba yao.

Haya yanatokea wakati Serikali ikiwa na mkakati wa kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini mpaka milioni 3 kwa mwaka kutoka 1.2 waliokuwepo mwaka juzi. Mkakati huo unatekelezwa ndani ya miaka mitatu, 2016/2018.

Ni jukumu ambalo zimepewa taasisi na mamlaka zenye dhamana ya kuutangaza utalii wa Tanzania. Bodi ya Utalii nchini (TTB) na Tanapa ni wahusika wa kwanza kwenye utekelezaji wa mpango huu ingawa wadau wengi wanakaribishwa kushiriki.

Profesa Maghembe hivi karibuni alizindua Bodi ya Wadhamini wa Tanapa ambayo itadumu kwa miaka mitatu ijayo ikitarajiwa kuishauri menejimenti ya shirika kuweka mikakati ili kufikia malengo. Katika kuufanya utalii unakua, mchango wa wananchi ni muhimu kuanzia kwenye kukabiliana na ujangili, utunzaji wa mazingira na kulinda hifadhi na wanyama waliopo kwenye maeneo yanayotambulika kisheria.

Ili kufanikisha ushirikiano huo, Tanapa ina wajibu wa kuboresha uhusiano wake na wananchi wanaozunguka hifadhi zake. Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya wananchi kuhusu shirika kupanua mipaka bila ushirikishwaji wa jamii husika.

Bodi hii inapaswa kujenga maelewano na jamii na kuielimisha umuhimu wa kutoa maeneo yao kwa ajili ya uhifadhi na utalii.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi iliyomaliza muda wake, Modestus Lilungulu, migogoro ya mipaka ambayo mingine ni ya muda mrefu inatokana na baadhi ya vijiji kutokubali alama za kudumu katika maeneo yaliyoongezwa hasa kwenye Hifadhi ya Ruaha.

Anasema kambi za uvuvi ya Kalilani kuendelea kuwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Milima ya Mahale, mpaka wa vijiji vya Ayamango, Gedamar na Gijedabong Wilaya ya Babati kuendelea kuishi ndani ya Hifadhi ya Tarangire baada ya kulipwa fidia na mgogoro kati ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani na vijiji vya Uvinje, Matipwili, Saadani na Kitame ni mambo yanayotakiwa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Profesa Maghembe anaitaka bodi hiyo na menejimenti ya Tanapa kudhibiti ujangili, kupunguza au kumaliza migogoro ya mipaka na kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato. Vilevile anawataka wateule kuisimamia sekta ya utalii ili kujenga uchumi wa nchi na kuwezesha uwekezaji.

“Ni jukumu la bodi kuhakikisha ujangili unamalizwa,” alisema Profesa Maghembe na kuiagiza bodi kuwashirikisha wananchi kwenye uhifadhi na kufanya maboresho kwenye programu ya ujirani mwema ili kuwajengea uwezo wa kiuchumi wananchi wanaozunguka hifadhi.

Waziri huyo alisema sekta ya utalii nchini inakadiriwa kuchangia asilimia 12 ya ajira na kuliingizia taifa kiasi cha Dola 2 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh4 trilioni) ambazo ni sawa na robo ya mauzo yote ya huduma na bidhaa nje ya nchi.

Kwa ukanda wa Afrika Mashariki, takwimu zinaonyesha Tanzania inaongoza kwa wastani siku ambazo watalii hukaa, kati ya 10 hadi 12 hivyo kuna haja kwa Tanapa kuboresha vivutio, masoko, huduma na miundombinu ya utalii kwa kuondoa migogoro iliyopo na kuepusha inayoweza kujitokeza.

Hilo linaweza kutekelezwa kutokana na bodi hiyo kujumuisha watu wenye uzoefu na maarifa mtambuka kutoka sekta mbalimbali kukabiliana na changamoto zilizopo.

Licha ya migogoro ya ardhi, bodi hiyo inapaswa kuweka mikakati ya uhakika itakayowazidi maarifa majangili wa tembo, faru na maliasili nyingine za misitu na hifadhi, ikiwamo uvunaji holela na usafirishaji wa magogo na mbao, uchomaji mkaa na kuni. Ujangili ni saratani ya utalii na hifadhi za taifa ambayo inahatarisha kutoweka kwa baadhi ya wanyama hasa wanaotafutwa kwa ajili ya biashara ya vipusa, wakiwamo faru na tembo na kitoweo inayofanywa zaidi na wananchi wanaozunguka hifadhi hizo.

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Jenerali mstaafu George Waitara na wajumbe wanane atakaoshirikiana nao kuishauri menejimenti ya Tanapa, wanalo jukumu la kutengeneza intelijensia itakayoutambua mtandao wa ujangili katika mapori ya akiba na hifadhi za taifa.

“Tutafungua ukurasa mpya kukabiliana na ujangili. Tutakamilisha uundaji wa jeshiusu na kutumia intelijensia na kuwashirikisha wananchi kutokomeza ujangili,” alisema Waitara