MAONI YA MHARIRI: Mihimili ya dola iwe huru, iheshimiane

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Muktasari:

Utawala wa nchi umegawanywa katika mihimili mitatu na kila mmoja una majukumu yake yaliyoanishwa vizuri kikatiba ili kuhakikisha kuwa hakuna muingiliano kati yao. Lengo ni kuufanya kila mmoja kuwa huru.

Kwa siku kadhaa tumeshuhudia mihimili mitatu ya dola ikipata changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kuingiliana au mmoja kuulalamikia mwingine.

Utawala wa nchi umegawanywa katika mihimili mitatu na kila mmoja una majukumu yake yaliyoanishwa vizuri kikatiba ili kuhakikisha kuwa hakuna muingiliano kati yao. Lengo ni kuufanya kila mmoja kuwa huru.

Hata hivyo, wadadisi wa masuala ya kisiasa wamekuwa wakihoji kama hilo linawezekana katika nchi za dunia ya tatu kama Tanzania.

Mihimili hiyo ni Serikali, Bunge na Mahakama. Wajibu wa Serikali kwa ufupi ni kuendesha utawala na utekelezaji wa kila siku wa shughuli za umma. Bunge lina wajibu wa kuisimamia Serikali na kutunga sheria na Mahakama ina wajibu wa kusikiliza na kuamua kesi na pia kutoa tafsiri ya sheria na Katiba ya nchi.

Kwa hiyo kila mamlaka inaitwa mhimili wa dola na kila mmoja hufanya kazi zake kwa uhuru. Uhuru huu unamaanisha kuwa chombo kimoja kisiingilie kazi za chombo kingine.

Lakini, kwa siku za karibuni kumetokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wabunge kuwa Serikali imekuwa ikiwakamata baadhi yao bila kufuata taratibu yaani bila kupitia ofisi ya Spika.

Malalamiko hayo hayakuishia kwa wabunge kuilalamikia Serikali tu, waliigusa hata Mahakama kwamba imeshindwa kutoa dhamana kwa baadhi yao licha ya kuwa makosa wanayoshtakiwa nayo huwa na dhamana.

Wakati hayo yakiendelea, sasa kumezuka mgogoro mwingine kati ya wabunge na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Makonda, ambaye ametakiwa kwenda Dodoma kujieleza katika Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge anatuhumiwa kuwakashifu wabunge kuwa wakati mwingine hukosa cha kuzungumza na ndio maana husingizia bungeni.

Alikuwa akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kupata ufafanuzi wa mali zake baada ya kutuhumiwa bungeni na Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Msukuma’, aliyedai mkuu huyo wa mkoa anatumia gari aina ya Lexus lenye thamani ya Sh400 milioni, amekarabati ofisi yake kwa Sh400 milioni bila kufuata utaratibu wa ununuzi wa umma, ana gari aina ya Toyota V8 na amejenga maghorofa kwa mwaka mmoja tu.

Ukiangalia kwa makini, unaweza kudhani ni jambo dogo, lakini kama ukifuatilia majadiliano ya wabunge, utagundua kuwa suala hili si dogo na linahitaji suluhisho la haraka.

Licha ya kwamba mihimili hii hufanya majukumu yao kwa uhuru, hatudhani kama ni sahihi kudhalilishana, kuonyeshana umwamba au kunyoosheana vidole, ingawa kukosoana hatudhani kama ni jambo baya. Lengo kubwa la kuwa na mihimili hii ni kuhakikisha nchi inaongozwa kwa mfumo wa utawala bora, huku sheria, haki na demokrasia vikipewa kipaumbele kikubwa. Tunashauri mihimili hii iheshimiane, ijue mipaka ya kila mmoja, lakini ijue kuwa lengo ni moja tu kuhakikisha gurudumu la maendeleo linasonga mbele.

Kila mhimili unapaswa kujua maana ya kuwa huru kwa sababu wakati mwingine ni rahisi kuliona hilo kinadharia, lakini likawa gumu kwa vitendo na hasa kutokana na yote kutegemea bajeti kutoka serikalini.

Mivutano ya namna hii haiwezi kwisha moja kwa moja, lakini tunaamini busara za viongozi wake zinaweza kupunguza mihemko ili kila mhimili ujione upo huru na ufanye kazi bila kuingiliwa.