Mijadala ya Bungeni tuna jambo la kujifunza?

Muktasari:

  • Kiu hii ya Watanzania ya kutaka kuona na kusikia yale ambayo wabunge wao wanayajadili bungeni ni vigumu kuipima faida yake. Ingawa ni wazi, ni haki yetu sisi wapiga kura kusikiliza na kuyaona yale tuliyowatuma, kama kweli tunawatuma wabunge wetu.

        Asilimia kubwa ya Watanzania bado wanatamani Bunge kuonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni. Tafiti nyingi zilizofanywa na hasa ule wa Twaweza zilionyesha kwa takwimu ukweli huu. Ukizingatia ukweli kwamba Serikali imefanikiwa kusambaza umeme vijijini na hivyo maeneo mengi hapa Tanzania yana umeme, watu wanaweza kuona televisheni majumbani kwao au vijiweni.

Kiu hii ya Watanzania ya kutaka kuona na kusikia yale ambayo wabunge wao wanayajadili bungeni ni vigumu kuipima faida yake. Ingawa ni wazi, ni haki yetu sisi wapiga kura kusikiliza na kuyaona yale tuliyowatuma, kama kweli tunawatuma wabunge wetu.

Swali la msingi hapa ni je, mijadala hiyo ina maana yoyote? Serikali inafuatilia mijadala hiyo? Inawasikiliza wabunge wetu? Inayafanyia kazi yale yanayotolewa na wabunge wetu? Tunajifunza kutokana na mijadala ya Bunge au tunaendeleza mipasho na ushabiki?

Majuma mawili yaliyopita, kulikuwa na mjadala mkali bungeni juu ya mpango wa maendeleo uliotolewa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango.

Mmoja wa wabunge walioshiriki katika mjadala huo ni aliyekuwa waziri wa habari, vijana na michezo,Nape Nnauye, ambaye alielezea juu ya hatari ya Tanzania kupoteza sifa ya kukopa ikiwa itatekeleza miradi yake mitatu mikubwa ya maendeleo.

Nape iliitaja miradi hiyo kama ujenzi wa umeme wa kutumia nguvu za maji katika Stiegler’s Gorge katika pori la akiba la Selous, ununuzi wa ndege sita ili kufufua shirika la ndege na ujenzi wa reli ya standard gauge.

Kufuatana na maelezo ya Nape, ufufuaji wa shirika la ndege utaigharimu serikali dola za kimarekani billion moja, mradi wa umeme utagharimu Serikali dola bilioni tano na ujenzi wa reli ya kati katika kiwango cha kisasa utaigharimu Serikali dola 15bilioni.

Nape alidai kuwa mpaka sasa deni la taifa ni dola za Marekani 26 bilioni. Na kwamba ili Tanzania ipoteze sifa ya kukopa, deni lake la taifa linatakiwa lisifikie dola za Marekani 45 billion.

Ukijumlisha dola bilioni moja za ufufuaji wa shirika la ndege, dola bilioni tano za ujenzi wa bwawa la umeme na dola 15bilioni za ujenzi wa reli ya kati katika kiwango cha kisasa, utapata jumla ya dola 21 bilioni ambazo ukijumlisha na deni la taifa la dola bilioni 26, unapata dola 47 bilioni ambazo ni zaidi ya ukomo, kwa dola bilioni mbili.

Akijibu hoja ya Nape, Waziri Mpango alisema hakuna kitu kama ukomo wa kukopa na akatoa mifano ya nchi kama Uingereza na Marekani ambazo zimepita ukomo huo, lakini bado zinakopesheka.

Hata hivyo, pamoja na majibu ya Dk Mpango, tuna mifano ya nchi kama Ugiriki ambazo si tu zimefikia mwisho ya ukomo wa kukopa, bali zimeshindwa kulipa madeni kiasi ya uhuru wa nchi hiyo kama kuingiliwa na wakopeshaji kama vile Serikali ya Ujerumani.

Kwa hiyo, si ukweli kwamba hakuna ukomo wa kukopa kwa nchi, ukomo upo na si busara kwa nchi kuendelea tu kukopa, kwa ajili ya ujenzi wa miradi ambayo uwezo wa miradi hiyo kurudisha madeni ni mdogo.

Hapa, ni kujitahidi kuzitoa hoja hizi kwa uangalifu mkubwa. Wakati watu wana mpango wa kwenda kwa kasi, hoja kama hizi hazifurahishi.

Kwa vile Tanzania ni yetu sote, madeni haya yatatugusa wote, sisi na vizazi vyetu, ni muhimu kujadiliana hadi kufikia maelewano. Hakuna asiyependa maendeleo, lakini tusitake maendeleo kwa kuangamiza vitu vingine muhimu kwetu na kwa taifa letu.

Tukiangalia miradi hii mitatu, ni muhimu tujiulize maswali muhimu na ya msingi, je ni miradi ipi ina uwezo wa kurudisha madeni hayo. Kwa harakaharaka tunaweza kusema ni mradi wa ufufuaji tu wa shirika la ndege la Tanzania ambao si tu una faida kwa taifa, bali pia una uwezo wa kurudisha deni lake la dola bilioni moja za marekani. Hoja hii inatolewa kwa kuzingatia upepo wa biashara hii ambayo kwa upande mwingine ni ngumu maana tunashuhudia makampuni makubwa ya ndege na ya miaka mingi yakishindwa biashara hii na kuifunga.

Mungu, atubariki tuiendeshe biashara hii kwa ufanisi na kwa faida.

Uwezo wa mradi huu wa ndege kurudisha deni hili unatokana na ukweli kwamba mradi huu una nia ya kuboresha biashara ya utalii nchini ambayo kwa sasa inaliingizia taifa dola bilioni mbili za kimarekani kwa mwaka.

Ili ufufuaji wa shirika la ndege la Tanzania uwe na tija kwa taifa na kuweza kulipa deni hilo kwa muda mfupi, Tanzania inatakiwa kuboresha biashara ya utalii hasa katika pori la akiba la Selous, na hifadhi za Ruaha na Katavi.

Umuhimu wa kuboresha maeneo hayo matatu unatokana na ukweli kwamba mpaka sasa zaidi ya dola bilioni moja na nusu kati ya dola bilioni mbili zinazoingizwa na utalii hapa nchini zinatokana na utalii unaoletwa na vivutio vilivyoko kaskazini ya nchi kama vile Mlima Kilimanjaro, hifadhi za Serengeti, Tarangire na Ngongoro.

Hivyo, ili kuboresha utalii, Serikali inapaswa sasa kusimamia utalii kusini mwa nchi ambako kuna vivutio vizuri zaidi kuliko vile vilivyoko kaskazini mwa nchini.

Kwa mfano, Ruaha ni mbuga ya wanyama pori kubwa kuliko nyingine zote hapa nchini. kadhalika pori la akiba la Selous ni kubwa kuliko mapori yote ya akiba barani Africa na pori hilo lina wanyama wengi zaidi kuliko mapori mengine. kwa mfano tembo tu hivi sasa ni zaidi ya 15,000. Kabla ya ujangili wa miaka 40, Selous lilikuwa na tembo 110,000.

Kadhalika hifadhi ya Katavi ina twiga weupe, jambo ambalo ni kivutio kikubwa kwa utalii. Kuboreshwa kwa shirika la ndege la Tanzania na vivutio vya utalii kusini mwa Tanzania kunaweza kabisa kuongeza pato la utalii kutoka dola bilioni mbili hadi dola bilioni 12 na hivyo kushindana na Morocco.

Kwa hiyo badala ya kujenga bwawa la umeme Stiegler’s gorge na hivyo kuharibu mapitio ya wanyama pori, tunapaswa kuboresha pori la akiba la Selous na kuboresha pori hilo hatupaswi kujenga miundo mbinu itakayokaribisha watu wengi ambao wataendeleza ujangiri katika pori hilo la akiba la Selous.

Inapaswa kukumbukwa kuwa wakati Serikali inajenga hoja kwa Unesco kulifanya pori la akiba la Selous liwe urithi wa dunia mwaka 1976, pori hilo lilikuwa na tembo 110,000, vifaru zaidi ya 2,000 na mbwa mwitu wengi kuliko pori lolote barani Afrika.

Lakini, pia ikumbukwe kwamba ni wakati huohuo mwaka 1976, ambapo Reli ya Tazara yenye umbali wa kilomita 1,800 kutoka Dar es Salaam mpaka Kapiri Mposhi inayokatisha katika pori hilo ilikuwa inafunguliwa rasmi baada ya ujenzi wa reli hiyo kwa msaada wa Serikali ya China, na hivyo kufungua pori hilo kwa dunia. Na katika miaka 40 iliyopita mpaka mwaka 2014, pori hilo lilipoteza asilimia 90 ya tembo kutoka tembo 110,000 mpaka tembo 15,000. Idadi ya vifaru hivi sasa inasemekana kuwa chini ya 30.

Hayo ndiyo madhara ya kuweka miradi ya miundombinu katika maeneo yanayopaswa kuwa ya kulinda mazingira kwa faida ya utalii.

Kitu kimoja tunachopaswa kujiuliza ni kwamba mpaka sasa tuna mabwawa ya kufulia umeme makubwa matatu ya Kidatu, Mtera na Kihansi. tunapaswa sasa kujiuliza tumekidhi mahitaji yetu ya umeme?

Ili mabwawa haya ya kufulia umeme yawe na faida, tunapaswa kulinda vyanzo vya mito yetu. Je, tumefanikiwa katika hilo. Ijapokuwa ujenzi wa reli ya kati katika kiwango cha kisasa pia hauwezi kulipa haraka, lakini kwa nchi inayohudumia nchi zaidi ya sita zisizo na bandari kama vile Malawi, Zambia, Congo ya DRC, Burundi, Rwanda and Uganda, tunahitaji si reli tu, bali reli ambayo iko katika kiwango cha kisasa, ambayo ina uwezo wa kubeba mizigo mingi zaidi na inayokwenda nchi hizo kwa chini ya saa 12.

Kwa hiyo, hapa nieleweke kwamba, sipingi kwa sababu ya kupinga tu; natoa maoni hayo ili Serikali ifikirie mara mbili kabla ya kujiingiza katika mradi ambao unaweza kuigharimu na kutugharimu sote pia.

Kwa hiyo, kwa maoni yangu, ningeacha mradi wa stiegler’s hasa wakati huu ambapo tuna gesi zaidi ya mahitaji yetu.

Kwani kama mradi wa Kinyerezi II unaweza kuingiza megawati 600, hii ina maana miradi minne ya aina ya Kinyerezi inaweza kutupa megawati 2,400 ambazo ni zaidi ya umeme wa stiegler’s gorge ambao unataraajiwa kupata megawati 2,100.

Wito wangu ni kwa viongozi serikalini ambao wengi wao walikuwa waalimu vyuo vikuu kutumia elimu zao za juu, kufikiri namna ya kuipeleka nchi yetu juu. Hakuna faida ya kuwa na shahada ya uzamivu ambayo haiwezi kumsaidia rais katika kupanga maendeleo ya nchi.

Padre Privatus Karugendo

+255 754633122