Mimba zinavyowatesa wanafunzi wa kike Bahi

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Chikopelo wilayani Bahi, Mkoa wa Dodoma wakipata mlo wa mchana katika chumba walichopanga mtaani. Wanafunzi hawa wanakabiliwa na vishawishi vingi vya kupata mimba kutoka kwa wanaume wakware. Picha zote na Tumaini Msowoya

Muktasari:

TAKWIMU ZA MIMBA

  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiahirisha kikao cha Bunge mjini Dodoma Julai 5, 2017 alisema takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2015, wanafunzi 3,637 waliacha masomo kutokana na tatizo hilo.

Katika Wilaya ya  Bahi, mkoani Dodoma kipo kijiji maarufu kinachoitwa Bahi Sokoni.

Ni sehemu iliyochangamka kiasi kutokana na shughuli za biashara za maduka ambazo zimeshamiri, huku wakazi wake wengine wakijishughulisha na kilimo.

Ni saa 12 na dakika kadhaa jioni, jua likielekea kuzama; naingia katika mitaa ya kijiji hiki. Katika mtaa mmoja,  nakutana na mashine ya kusaga nafaka. Nyuma ya mashine ipo nyumba kuukuu.

Naitazama nyumba hii, nagundua kwamba hapa ndipo mahali nilipoelekezwa. Ni makazi ya Mzee Ally Mohamed mwenye umri wa miaka 60.

Baada ya kubisha hodi, ilisikika sauti ikiitikia “karibu” huku mlango wa nyumba ukifunguliwa. Alijitokeza binti ambaye baadaye alijitambulisha kwa jina la Mariam Ally. Uso wake umekunjamana na anaonekana kama amezama kwenye lindi la mawazo.

Baada ya kunikaribisha na kuketi kwenye kiti kilichokuwapo katika uwanja ulio mbele ya nyumba, napata hisia kwamba huyu ni binti ambaye nilipata taarifa kwamba ameachishwa shule kutokana na kupata ujauzito. Baadaye nilithibitisha kwamba hisia hizi zilikuwa kweli.

Mariam (17) alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Bahi. Wakati nafika kijijini kwake Agosti 15, 2017, ilikuwa imepita siku moja tu tangu aache masomo kwa sababu ya ujauzito. Hili ndilo lilimfanya aonekane mwenye huzuni.

Huenda alikuwa akitafakari namna ya kuyakabili majukumu mapya na mazito ya kulea mimba na baadaye ulezi wa  mtoto. Hii ni  tofauti kabisa na malengo yake ya  kusoma.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bahi, Stellah Selemani anakiri kupata taarifa za Mariam kuwa mjamzito na anaeleza kwamba wapo kwenye hatua za awali za kumfuta kabisa masomo, ili aendelee kulea mimba yake.

“Ni vigumu kwangu kama mzazi kumfukuza mtoto shule, lakini kiutendaji sina jinsi, ni lazima arudishwe nyumbani kwa sababu hawezi kusoma na wenzake akiwa mjamzito au amejifungua,” anasema.

Anasema walipopata taarifa za ujauzito wa mwanafunzi huyo, walienda kumpima na alipogundulika walitoa taarifa kwa uongozi wa juu ikiwamo ofisi ya kata na polisi.

Mtendaji wa Kata ya Bahi, Juma Idd naye anakiri kupokea taarifa hiyo na kwamba wanachofanya  sasa ni msako wa mwanaume aliyempa mimba msichana huyo ili sheria ichukue mkondo wake.

Kanuni Namba 4 ya Kanuni za Elimu Toleo la 2002, inaelekeza kufukuzwa shule kwa mwanafunzi yeyote wa kike na au wa kiume ambaye anajihusisha na vitendo vya ngono.

Mimba imekuwa ikitumika kama uthibitisho kwamba mwanafunzi husika amejihusisha na vitendo hivyo.

Simulizi ya Mariam

Mariam anaanza kusimulia kuhusu mkasa wake huku akitokwa na machozi.

“Shemeji yangu ndiye aliyenipa hii mimba, nilimkatalia lakini alinilazimisha na mimi sikujua kama nitapata mimba. Natamani kuendelea na masomo yangu.”

Anasema ilikuwa likizo ya Desemba 2016, wakati alipokutana na shemeji yake ambaye alimlazimisha kufanya mapenzi. “Shemeji yangu hajui kama nina mimba, sijamwambia kwa kuwa sina mawasiliano naye. Yeye anaishi Dar es Salaam na mimi nilienda kule likizo,” anasema.

Anasema wakati anasoma aliweza kupambana na kushinda vishawishi alivyokuwa akikutana navyo, kwani alikuwa akitembea zaidi ya kilometa tano kwenda na kurudi shuleni kila siku.

Anavitaja vishawishi hivyo kuwa ni pamoja na lifti za waendesha pikipiki, lakini anaumia kwamba ameangukia katika mikono ya mtu aliyepaswa kumlinda ambaye ni shemeji yake, mume wa dada yake.

Kisa cha Mariamu kinaakisi hali halisi ya elimu kwa watoto wa kike ilivyo wilayani Bahi. Kwa mfano, katika  shule ya Sekondari ya Chikopelo wilayani humo, kati ya wanafunzi  67 walioanza kidato cha kwanza 2014, wamebaki wanafunzi 26 wanaotarajiwa kumaliza kidato cha nne mwaka huu.

Mwalimu wa Taaluma wa shule hiyo, Ahadi Mgando anasema walianza wasichana 31 lakini waliobaki ni 12 tu huku wengi wakiacha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwamo kupata ujauzito.

Mkurugenzi wa Shirika la Marafiki wa Elimu Dodoma, David Makundi anasema katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Babayu, wasichana sita kati ya wanane waliokuwa kidato cha nne walipata mimba na kuacha shule mwaka 2015.

Kilio cha mzazi 

Baba yake Mariam, Ally Mohamed (60) anasema hajui afanye nini kwani suala la mwanawe kuwa mjamzito limemchanganya kiasi cha kuhisi kupata ugonjwa wa moyo.

“Nilijua binti yangu atamaliza masomo bila bugudha yoyote, kwa kweli naumia sana, nimechanganyikiwa mno,” anasema  na kuongeza: ‘‘Umekuja wakati tayari binti yangu ameshaharibikiwa? Kwa nini huwa hamuwasaidii kabla hawajafikia hatua hii? Inaniuma sana.”

Mzee Ally ambaye ndiye mlezi pekee wa Mariam, kama ilivyo kwa binti yake huyo, anatamani mwanawe apate nafasi ya kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Hata hivyo, suala hilo haliwezekani kwani mbali na kikwazo cha Sheria ya Elimu ya 1978 na Waraka wa Kanuni za Elimu wa 2002, Rais John Magufulu ameweka msimamo kwamba hilo haliwezekani asilani katika uongozi wake.

 Tatizo la wanafunzi wasichana wanaoacha shule kwa sababu ya mimba pia ni kubwa katika mtazamo wa kitaifa.Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiahirisha kikao cha Bunge mjini Dodoma Julai 5, 2017 alisema takwimu zinaonyesha kuwa 2015, wanafunzi 3,637 waliacha masomo kutokana na tatizo hilo.

Vichocheo vya mimba

Uchunguzi wa Mwananchi katika Wilaya ya Bahi, umebaini vichocheo vya wanafunzi kupata mimba ni pamoja na mmomonyoko wa maadili, baadhi ya wazazi kutotimiza wajibu wao, umasikini, mazingira duni ya kujifunzia pamoja na mila na desturi zinazomgandamiza mtoto wa kike.

Makundi anasema wasichana wengi wanajilea wenyewe katika vyumba wanavyopanga kutokana na makazi yao kuwa mbali na shule wanazosoma.

“Pia, kuna suala la mila na desturi za kutojali watoto wa kike, kwamba wao ni wa kuolewa tu, hivyo kuna wakati wazazi wanaona mimba za watoto hawa ni kitu cha kawaida,” anasema.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Matolee   Festo Matonya anasema: “Wasichana wengi wanaishi peke yao na wale wanaoishi kwa wazazi wanatembea umbali mrefu. Unadhani nini kitakachotokea hapo? Ni vishawishi na mimba tu”.

 Anaongeza: “Mfano shule yetu ya Bahi, tatizo kubwa ni gharama za kukaa bwenini, inabidi watembee umbali mrefu na njiani wanakutana vishawishi ikiwamo bodaboda wanaowarubuni kwa chipsi.”

Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Magaga, Laurent John anasema ili kupunguza tatizo hilo, lazima watoto wapewe malezi ya kimaadili na ujenzi wa mazingira mazuri ya kusomea kwa wanafunzi.

Hatua za kudhibiti

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Elizabeth Kitundu anasema Serikali haitamfumbia macho mwanaume yeyote atakayebainika kumpa mimba mwanafunzi na kwamba, amewaelekeza wenyeviti wa vijiji kuwachukulia hatua, pia wazazi watakaobainika kuwaficha wanaume waliowapa mimba watoto wao.

 “Mimba ni changamoto kwa watoto wetu, nimeshapita huko kote kuwasihi wanafunzi waachane na tamaa, hayo yote watakayakuta huko mbele, wasome kwanza,” anasema.

Katika Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali namba mbili ya 2016, Bunge liliridhia adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa mwanaume atakayethibitika kujamiiana na mtoto wa kike mwenye umri wa chini ya miaka 18 akiwamo mwanafunzi.

Ofisa Elimu Sekondari wa Bahi, Hassan Mohamed anasema wamewaagiza watendaji wa kata na vijiji kuwakamata wahusika wa mimba za wanafunzi ili sheria ichukue mkondo wake.

 “Sisi tunachofanya ni kusimamia sheria, hata hivyo mimba kwenye wilaya yetu imepungua kwa kiasi kikubwa, mwaka huu tumepata kesi chache tu,” anasema.

Katika shule aliyosoma Mariam, Mwalimu Stellah anasema ili kukabiliana na tatizo hilo, wamekuwa wakizungumza na watoto wa kike na kuwaambia ukweli kuhusu maisha na umuhimu wa kujitunza.