Thursday, September 14, 2017

Mipangomiji wakiwa makini migogoro ya ardhi itakuwa historia

By Joyce Joliga, Mwananchi jjoligamwananchi.co.tz

Songea. Akisitisha upimaji wa ardhi uliokuwa unaendelea katika Kata ya Mshangano, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dk Binilith Mahenge amewataka watumishi wa umma kuacha kupindisha sheria na kujali maslahi yao ili kupunguza migogoro ya ardhi.

Mkuu huyo amesema rushwa miongoni mwa watumishi wa idara ya ardhi imekuwa kichocheo kikubwa cha migogoro hiyo hasa baina ya wananchi na wafanyabiashara wanaotaka kuanzisha miradi ya aina tofauti.

Amesema hayo alipokuwa akisitisha upimaji wa ardhi unaofanywa na Kampuni ya Ardhi Plan kwa mwezi mmoja, kuanzia Agosti 22 hadi Septemba 22 na kumtaka Katibu Tawala (RAS) pamoja na halmashauri ya manispaa hiyo kuunda kamati za uchunguzi kufuatilia suala hilo ili haki itendeke. Tayari kampuni hiyo imeshapima zaidi ya viwanja 16,000 mpaka sasa.

“Nawaomba wananchi kuwa na subira. Kamati zifanye kazi kwa haraka ili kuujua undani wa mgogoro huu na kutenda haki. Nimeambiwa kampuni haina shida na upande wowote ila isiendelee na upimaji hadi suluhu itakapopatikana,” alisema Dk Mahenge.

Kwa muda mrefu, wananchi wa Mshangano wamekuwa na mgogoro na Paschal Msigwa, mfanyabiashara wa mjini hapa, mgogoro ambao umedumu muda mrefu bila kupata suluhu ya kudumu.

Wananchi hao wakiongozwa na diwani wao, Lother Mbawala wanagoma maeneo yao kupewa mfanyabiashara huyo ambaye ana nia ya kujenga shule wakisema waliyaacha kwa ajili ya ujenzi wa shule ya umma na si binafsi.

Diwani huyo anasema mgogoro uliopo unahusu kiwanja cha zaidi ya eka sita ambazo halmashauri kupitia kitengo cha ardhi ilimmilikisha bila kuwashirikisha wananchi wala uongozi wa kata hiyo. Lakini kutokana na kuongezeka kwa uelewa wa umuhimu wa kupima ardhi kwa kutumia kampuni binafsi zenye kibali cha wizara husika, wananchi walikubaliana na kampuni hiyo ambayo imekwama kutokana na agizo la mkuu wa mkoa.

“Kuizuia kampuni hii kuendelea kufanya kazi kumewaathiri wengi ambao wanategemea kuuza viwanja vyao ili kujiongezea kipato,” anasema Mbawala. Anasema makubaliano ya kupima ardhi ya wananchi hao kwa gharama zao ambazo wameshalipa yapo tangu mwaka 2011 na kushangazwa na uamuzi wa ofisi ya mkurugenzi kutoa kiwanjahicho bila kufanya mkutano na wananchi.

Anasema: “Mgogoro ulianza mwaka 2013 baada ya mfanyabiashara huyo kupewa kiwanja namba 1287 cha eka 7.6 kilichotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi. Wananchi walipinga uamuzi huo hivyo akanyang’anywa akapewa kingine namba 878 cha ukubwa wa eka saba, katika eneo ambalo lilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa sekondari.”

Anasema kwa mara ya pili wananchi wanapinga eneo lao kupewa mfanyabiashara huyo na kumtaka mkurugenzi kumtafutia jingine kwani ana viwanja vingi maeneo ya Namanditi na Shule ya Tanga ambayo yamepimwa badala ya kung’angania ya wananchi. “Jukumu langu ni kuwatetea wananchi wanyonge. Sitabadilika hadi nione haki ikitendeka. Mkurugenzi akae na Ofisa Mipango Miji kutafuta eneo jingine na si kunyang’anya maeneo ya wananchi. Wao walishindwa kupima viwanja, wananchi wajipimie ili kuendeleza makazi yao na kujiletea maendeleo,” Mbawala.

Akisisitiza kuachwa kwa eneo hilo ambalo wananchi wanalihitaji, diwani huyo ametoa pendekezo ambalo likiungwa mkono, mfanyabiashara huyo anaweza kufanikisha mradi wake.

Amesema yupo mwanakijiji mwenye eneo la eka 11 katika Mtaa wa Mitendewawa ambaye yupo tayari kulitoa endapo atalipwa fidia.

Msigwa anasema: “Nilishaanza ujenzi. Kuna madarasa mawili ambayo hayajakamilika, ujenzi ulikuwa unaendelea.”

Migogoro hii na mingine inayofanana na hii inaweza kuwa historia kama maofisa wa mipangomiji watakuwa makini.

-->