Mitandao ya kijamii fursa mpya ukuaji wa Kiswahili

Muktasari:

  • Kiswahili ni lugha inayokua na kuenea zaidi duniani ikiwa na asili ya Pwani ya Afrika Mashariki. Mbali na kuenezwa na shughuli za kijamii na kiuchumi, lugha hiyo ya Kiafrika yenye wazungumzaji wengi imetengenezewa taasisi kwa ajili ya kuikuza na kuieneza.

Lugha yoyote inakua na kuenea pale inapokuwa na watumiaji. Husambaa kwa jamii nyingine, kwa sababu ya mwingiliano unaotokana na shughuli za kijamii au kiuchumi kama vile ndoa, elimu au biashara.

Kiswahili ni lugha inayokua na kuenea zaidi duniani ikiwa na asili ya Pwani ya Afrika Mashariki. Mbali na kuenezwa na shughuli za kijamii na kiuchumi, lugha hiyo ya Kiafrika yenye wazungumzaji wengi imetengenezewa taasisi kwa ajili ya kuikuza na kuieneza.

Hapa Tanzania kuna vyombo vingi vinavyofanya kazi ya kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili. Pamoja na majukumu mengine, vyombo hivyo vina jukumu la kuhakikisha kwamba Kiswahili kinapata wazungumzaji wengi na kuongeza misamiati.

Baadhi ya vyombo vilivyopo ni Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki), Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita), Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (Ukuta) na Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania (Uwavita).

Habari njema kwa Kiswahili

Licha ya kuanzishwa kwa vyombo hivyo miaka ya 1960, kazi zao zimekuwa zikikwamishwa na teknolojia duni ya habari na mawasiliano. Machapisho yao mengi yako kwenye vitabu, jambo linalochelewesha lugha hiyo kwenda mbali zaidi.

Sasa ni habari njema kwa taasisi hizo baada ya mitandao ya kijamii kukitambua Kiswahili kama moja ya lugha ambazo zinaweza kutumika kwa mawasiliano.

Kama inavyofahamika, mitandao ya kijamii inatumiwa na watu wengi hasa vijana, hivyo ikitumika ipasavyo itasaidia kukuza lugha ya Kiswahili.

Rekodi ya Kiswahili mitandaoni ilianza kuwekwa na mtandao wa Facebook baada ya kuamua kukitumia Kiswahili kwenye orodha ya lugha zitakazotumika. Watumiaji wa Kiswahili wamepata fursa adhimu ya kutumia lugha yao.

Hata wakati Seneta John Kennedy alipokidhihaki Kiswahili hivi karibuni wakati mmiliki wa mtandao huo, Mark Zuckerberg akihojiwa na Bunge la Seneti la Marekani, watu wa mataifa mbalimbali walilaani matamshi yake aliposema Kiswahili ni “lugha yenye maandishi yasiyoeleweka.”

Hakuna lugha iliyo bora kuliko nyingine kwa sababu zote zinafanya kazi moja kama chombo cha mawasiliano. Tofauti zinazojitokeza ni mawanda ya kuenea kwa lugha yenyewe na wingi wa misamiati yake.

Tayari baadhi ya mitandao ya simu hapa nchini imeanza kuwawezesha wateja wao kutumia facebook kwa lugha ya Kiswahili, jambo ambalo ni hatua kubwa kwa watumiaji wa lugha hiyo inayozungumzwa zaidi Afrika Mashariki.

Zamu ya Twitter

Wiki chache zilizopita, mtandao wa kijamii wa Twitter nao ukakitambua rasmi Kiswahili kama lugha mojawapo itakayotumika kwenye mtandao huo, ili kuwapa watumiaji wake uhuru wa kuchagua lugha waitakayo.

Hatua hiyo ya kihistoria imekifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kufikia mafanikio hayo, ingawa bado haijaingizwa rasmi katika mipangilio ya lugha kwenye mtandao huo.

Mtandao huo sasa unatambua maneno ya Kiswahili na hutoa tafsiri ya maneno ya lugha hiyo ambayo yamesemwa na kuandikwa katika nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

Tangu wiki iliyopita, Twitter ilianza kutumia lugha hiyo katika twiti (tweet) na kisha kutoa tafsiri inayokaribia sana kama ilivyo katika lugha nyingi za kigeni.

Wizara ya Michezo na Urithi ya Kenya ilijiunga na watumiaji wa Twitter kusherehekea mafanikio hayo. Wizara hiyo iliandika twiti yake na kusema:

“Kiswahili ambacho hutumiwa sana Afrika Mashariki, ni lugha ya kitaifa ya Kenya na inaunganisha watu wa Kenya.”

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa lugha hiyo inazungumzwa na mamilioni ya watu duniani hasa Afrika. Kiswahili hutumiwa kama lugha ya Taifa kwa nchi za Tanzania na Kenya na huzungumzwa pia na watu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Uganda, Rwanda na Burundi.

Kwa bahati mbaya, vyombo vinavyofanya kazi ya kukuza na kueneza lugha hiyo adhimu, havina akaunti kwenye mitandao ya kijamii. Sasa ni wakati wao wa kugeukia mitandao hiyo ili kurahisisha kazi yao ya kukipa nafasi Kiswahili

Wadau wazungumza

Wakizungumzia hatua hiyo, wadau wa Kiswahili nchini wamesema kutambuliwa kwa Kiswahili, ni hatua kubwa kwa lugha hiyo kwa sababu itapata wigo mpana wa matumizi, kuongeza misamiati na idadi ya wazungumzaji.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki), Dk Ernesta Mosha anasema hatua hiyo ya Twitter ni fursa kwa vyombo vya ukuzaji wa lugha ya Kiswahili, kuangalia namna ya kutumia mitandao ya kijamii kufanya kazi zao za kukuza na kueneza Kiswahili.

Dk Mosha anasema Kiswahili sasa kimekuwa na wigo mpana wa matumizi, jambo litakalowezesha kuongezeka kwa misamiati, sambamba na kuongezeka kwa watumiaji wa lugha hiyo duniani.

“Hiyo ni fursa kwa vyombo vya kukuza Kiswahili; sasa tunatakiwa kufikiria namna ya kutumia mitandao ya kijamii kama Twitter kufundisha lugha ya Kiswahili kwa watu wa mataifa mengine,” anasema. Akiwa na mtazamo kama huo, mchunguzi lugha kutoka Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita), Anold Msoke, anasema kutambuliwa kwa Kiswahili, ni jambo zuri kwa watumiaji wake kwa sababu sasa wameondolewa ulazima wa kutumia lugha ya Kiingereza.

Hivyo, anasema watu wanaweza kutumia Kiswahili kwenye mitandao ya kijamii kutangaza biashara zao au shughuli nyingine wanazofanya na watu wakavutiwa kujifunza Kiswahili ili wapate bidhaa au kitu wanachokitaka.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Aldin Mutembei anabainisha hatua hiyo kama utambulisho wa Kiswahili duniani, licha ya matamshi makali ya Seneta wa Marekani, John Kennedy kukidhihaki Kiswahili.

Anawataka Watanzania kujivunia lugha yao ya Kiswahili kwa kuona fahari kuitumia kwenye mazungumzo ya kawaida na wanapoandika kwenye mitandao hiyo.

“Ningekuwa na mamlaka hapa kwetu, ningewataka wataalamu waandike makala moja moja ya Kiswahili katika fani zao, iwe ni sayansi au uhandisi ili tupate misamiati mipya na kukuza lugha yetu ya Kiswahili,” anasema Dk Mutembei.

Mkuu wa Idara ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Athuman Ponela, anasema kutambuliwa kwa Kiswahili ni mafanikio, kwa sababu kundi kubwa la vijana wa mataifa mbalimbali wanatumia mitandao hiyo.

Anasema jambo muhimu siyo tu kutambulika kwa Kiswahili bali watu wakitumie kwenye mitandao ya kijamii ili kuwavutia wengine ambao hawakizungumzi.

Anasema mazungumzo ya Kiswahili yakitamalaki kwenye mitandao ya kijamii yataongeza shauku ya wengine kujifunza. “Tunatakiwa kwenda mbele zaidi ya kutambuliwa, tutumie jukwaa la mitandao ya kijamii kujifunza Kiswahili na kufundisha wengine. Lugha inakua kila siku, kwa hiyo ni vizuri kujifunza mara kwa mara,” anasema Dk Ponela.

Lugha hiyo ni kielelezo cha utamaduni wa Mwafrika na inawakilisha watu wa Afrika Mashariki, hivyo ni wakati kwa kila Mswahili kujivunia lugha hiyo kwa kuitumia kwenye majukwaa na mitandao ya kijamii ili kuwavutia wengine.