Mizuka ilipanda mashabiki mechi za mahasimu

Muktasari:

  • Simba na Yanga zimegawanya Watanzania katika makundi mawili, yanayokinzana kishabiki na kulazimisha wengine wasipende kutumia vitu vyenye rangi za kijani au nyekundu.

KILA linapofika pambano la mahasimu, mizuka ya mashabiki hupanda. Tambo za kila aina zitasikika kila mmoja akimtambia mwenzake.

Simba na Yanga zimegawanya Watanzania katika makundi mawili, yanayokinzana kishabiki na kulazimisha wengine wasipende kutumia vitu vyenye rangi za kijani au nyekundu.

Simba na Yanga, zinapokuwa zinajiandaa kukutana, kunakuwa na shamra shamra za aina yake, mfano tambo za mashabiki kila mtu akivutia ushindi kwa timu yake, zinaibua mastaa na kushusha thamani ya baadhi ya wachezaji, kambi zinakuwa na ulinzi mkali na wakati mwingine makocha, viongozi kutimuliwa.

Kambi za klabu hizo kwa msimu huu, ziliwekwa katika mkoa wa Morogoro au Pemba na Unguja, huku baadhi ya wakazi wakisimamisha shuguli zao kwa muda, ili kwenda kushuhudia jinsi ambavyo timu zao zinajifua.

Lakini kabla ya mechi, utasikia mashabiki wanapigana vikumbo kulinda uwanja usiku kucha. Hilo lkinafanyika sasa ole wako uonekane unakatiza katikati ya uwanja usiku...

Katika msimu huu Simba ndio ilionekana kujiamini zaidi kutokana na usajili walioufanya kilichofanya mashabiki wake kutamba mitaani kuona hawawezi kusumbuliwa na Yanga.

Unaweza kuona hawa wamebeba jeneza na bendera ya timu husika.

Mechi ya kwanza iliyokuwa na tambo za kutosha, hakuna aliyetoka mbabe dhidi ya mwingine, baada ya dakika 90 kuamua sare ya bao 1-1, Obrey Chirwa akiwa ameifungia Yanga kipindi cha kwanza na winga machachari wa Simba, Shiza Kichuya akijibu mapigo kipindi cha pili, hivyo mashabiki wa pande zote wakitoka roho kwatu katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.

Kabla ya mechi hiyo, matokeo ya mechi zao mwisho yalifanana, Simba wakiifunga Majimaji ya Songea, mabao 4-0 Uwanja wa Taifa, huku Yanga wakiibuka kidedea katika ardhi ya Shinyanga kwa kuwashushia kipigo wenyeji wao, Stand United ‘Chama la Wana’ cha mabao 4-0.

Matokeo hayo ni kama yalijenga ujasiri kwa timu zote , kuona zipo vizuri kushindana kiuwezo na pia kuwafanya mashabiki wao kutambia, huku waliokuwa mikoani kupata ujasiri wa kutua jiji la Dar es Salaam, kushuhudia mtanange huo.

Kwa mechi ya mzunguko wa pili, Simba ilionekana kuwa imara zaidi kutokana na mfululizo wa ushindi waliokuwa wanaupata, ukiachana na mechi yao ya mwisho na Lipuli ya Iringa ambayo walitoka sare ya bao 1-1.

Mashabiki wa Yanga, hawakuwa na msisimko mkubwa wala amsha amsha, kwani ilitokana na aliyekuwa kocha wao, George Lwandamina kurejea nchini kwao Zambia na kikosi kubaki kwa makocha wasaidizi na mechi yao ya mwisho kabla ya kukutana na Simba, walicheza na Mbeya City na matokeo yake yakawa sare ya bao 1-1.

Katika mechi ya mzunguko wa pili, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga na kufanya kumaliza msimu kishujaa kwa kuchukua ubingwa na kuweka historia ya kuwafunga mahasimu wao Yanga.