Mjue Mnangagwa na yaliyo nyuma ya pazia la Mugabe

Muktasari:

  • Pamoja na Mugabe kugoma kujiuzulu wala kugusia hilo kupitia hotuba yake kwa Taifa Jumapili iliyopita, ni dhahiri kuwa kiongozi huyo mkongwe Afrika yupo ukingoni. Jumapili mchana, chama tawala cha Zanu-PF kilimuondoa Mugabe kwenye uongozi.

Wapenda demokrasia wengi wanaamini Zimbabwe mpya inakuja. Novemba 15, mwaka huu Jeshi la Zimbabwe lilimweka katika kizuizi cha nyumbani Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe na kufanya hivyo kwa siku mbili mfululizo, huku wakidai hawajafanya mapinduzi na usalama wa kiongozi wa nchi uko vizuri.

Pamoja na Mugabe kugoma kujiuzulu wala kugusia hilo kupitia hotuba yake kwa Taifa Jumapili iliyopita, ni dhahiri kuwa kiongozi huyo mkongwe Afrika yupo ukingoni. Jumapili mchana, chama tawala cha Zanu-PF kilimuondoa Mugabe kwenye uongozi.

Uamuzi wa Zanu-PF kumuondoa Mugabe katika uongozi wa chama, ulifanywa na Kamati Kuu, ikiwa ni hatua ya kuelekea kumnyofoa kwenye urais wa nchi kupitia Bunge.

Zaidi Kamati Kuu ya Zanu-PF ilimtangaza Emmerson Mnangagwa kuwa kiongozi wake.

Kitu ambacho watu wanapaswa kufahamu ni kwamba hata Mugabe akiondoka, Zimbabwe inayokuja itaendelea kuwa ya hovyo kwa sababu mipango ya kumuondoa Mugabe madarakani imesukwa na tabaka ambalo limehusika kuiharibu nchi hiyo.

Mambo matatu ya kuzingatia, mosi; viongozi wa Jeshi la Zimbabwe hawana tatizo hata robo na Mugabe. Hata taarifa yao ya Novemba 15, mwaka huu, ilieleza kuwa shida yao ni wahalifu ambao wamemzunguka Mugabe.

Kauli hiyo ilikwenda pamoja na kumtambua Mugabe kuwa ni Rais wa Zimbabwe, Mkuu wa Nchi na Mkuu wa Serikali, vilevile Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama Zimbabwe.

Haitoshi, Novemba 17, mwaka huu, ikiwa ni siku mbili baada ya kumweka chini ya ulinzi, Mugabe akiwa na timu yake kamili ya ulinzi kama Rais wa nchi, alihudhuria mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Harare.

Nyongeza ya hapo ni kwamba Novemba 19 usiku, Mugabe alihutubia taifa akiwa amezungukwa na wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama vya Zimbabwe.

Badala ya kutangaza kujiuzulu kwa sababu ndicho kilichosubiriwa kwa hamu zaidi, aliahidi kuhutubia Mkutano Mkuu wa chama chake, Zanu-PF mwezi ujao, ingawa alikiri kutambua hisia za watu wengi.

Jambo la pili kufahamu ni kuwa mipango ya kumuondoa madarakani Mugabe siyo ukombozi, kwamba Jeshi liliona nchi inakwenda vibaya, hivyo kuchukua hatua za kuinusuru, bali kiini ni mgogoro wa nani anastahili kumrithi Mugabe.

Maofisa waandamizi wa Jeshi la Zimbabwe wamechagua hatma yao zaidi kuliko ya wananchi. Wametazama ni upande gani wenye kuwapa nafuu baada ya Mugabe kukabidhi nchi, hivyo kuchukua hatua ambayo imeonekana.

Jambo la tatu ni uzee wa Mugabe. Wameona kuwa kwa umri wa miaka 93 wa Mugabe hivi sasa, ni dhahiri yupo ukingoni, hivyo watu wengi, kwa wazi na siri, wamekuwa wakisuka mipango ya kumrithi, ndiyo maana Jeshi limeshika mpini ili kuzuia wale ambao watapunguza au kuondoa masilahi yao.

Jambo la nne ambalo ndilo msingi wa tatizo ni mke wa Mugabe, Grace Mugabe kuonekana kuwa hatari kwa masilahi ya watu wazito ambao wamekuwa wanufaika wakuu wa mfumo mbaya wa kugawana rasilimali za Zimbabwe.

Grace amekuwa kipenzi cha vijana wa chama tawala, Zanu-PF na nchi kwa jumla. Vijana ambao wanaona fursa zimebanwa na wazee wenye kujipambanua kama wanamapinduzi waliolikomboa taifa hilo.

Hivyo, Grace amemponza Mugabe kwa sababu aliamua kuchuana waziwazi na Mnangagwa ambaye ni Makamu wa Rais aliyeondolewa na Mugabe.

Upande wa pili, Mnangagwa kwa sababu za umri, ushawishi na kwa vile naye ni mmoja wapigania uhuru, jeshi na chama (Zanu-PF) wameona bora Mnangagwa kuliko Grace.

Hali hiyo inakwenda na matokeo ya Mnangagwa kuteuliwa kuwa kiongozi wa Zanu-PF, wakati Mugabe amevuliwa uongozi, kisha Grace na watu ambao iliaminika walikuwa nyuma yake kufutwa uanachama.

Sanaa ya mapinduzi

Jeshi la Zimbabwe linataka lisionekane limempindua Mugabe, isipokuwa “linashughulika na wahalifu wanaomzunguka”, upande wa pili likachukua uongozi wa nchi na kukamata viongozi ambao wameonekana kuwa wenye kumuunga mkono Grace.

Tayari Waziri wa Fedha, Ignatius Chombo ambaye alikuwa nyuma ya harakati za Grace, ameshawekwa chini ya ulinzi. Bila shaka Chombo ni mmoja wa walioitwa “wahalifu waliomzunguka Mugabe”, kama Msemaji wa Jeshi, Meja Jenerali Sibusiso Moyo, alivyosema Novemba 15. Vilevile Chombo ni mmoja wa waliofukuzwa uanachama Zanu-PF.

Sura halisi baada ya Jeshi kuchukua uongozi wa nchi ilikuwa kulazimisha mazungumzo kufanyika kati ya Mugabe, viongozi wa dini, Makamu wa Pili wa Rais, Phelekezela Mphoko pamoja na Mnangagwa ili Mugabe akabidhi nchi lakini msisitizo ni kumkabidhi Mnangagwa.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zimbabwe, nchi inakuwa na Makamu wa Rais wawili, wa kwanza na wa pili. Nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ndiyo inatolewa macho zaidi, kwani mwenye cheo hicho ndiye anakuwa na hadhi ya kumrithi Rais aliye madarakani.

Kitendo cha Mugabe kumwondoa kazini Mnangagwa kisha kuanzisha mchakato wa kumsimika Grace kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, huku vijana wa Zanu-PF wakimpigia debe mama, kilimaanisha nchi inakwenda kuwa keki ya kizazi kipya, hivyo kuwatisha wakongwe waliopigania uhuru.

Utaona sasa, Jeshi la Zimbabwe linataka lionekane lenyewe halikuwa na dhamira ya kuingilia siasa za nchi, wakati tayari limeshaingilia. Linajifanya kumheshimu Mugabe wakati tayari limeingilia utawala wake na kuzuia matakwa ya Mugabe kumteua Grace kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais ili aje kumrithi.

Jeshi la Zimbabwe lilianza kumtisha Mugabe mara tu alipomwondoa Mnangagwa na kukaribisha mchakato wa kumpitisha Grace kuwa Makamu wa Rais kupitia Zanu-PF. Mkuu wa Majeshi, Jenerali Constantino Chiwenga alitishia kuwa kuendelea kwa misuguano kwenye chama kungesababisha jeshi liingilie.

Kweli Jeshi likaingilia kati na kudhibiti nchi. Mnangagwa na Chiwenga ni marafiki, kwa hiyo Jeshi la Zimbabwe liliamua kudhibiti nchi kwa malengo mawili kwa mpigo. Mosi ni kumtetea rafiki wa mkuu wa majeshi, pili ni kulinda masilahi ya mabosi wa jeshi pamoja na maveterani wake, maana ni tabaka la wala nchi (wapigania uhuru).

Zimbabwe na uhuru

Katika ufafanuzi wa Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere kuhusu mantiki ya kutungwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1967 ni baada ya kuona baadhi ya viongozi wakianza kujinufaisha kwa mali za umma kwa kigezo cha kuwa tabaka la wapigania uhuru.

Hiyo kansa aliyoikataa Mwalimu Nyerere kupitia Azimio la Arusha, ya watu ambao wamepigania uhuru wa nchi kujiona wao ni tabaka maalumu sana na kutaka kujilimbikizia mali na kupata upendeleo mkubwa kwenye nchi ndiyo ambayo imeiharibu Zimbabwe.

Tangu Zimbabwe ilipopata uhuru mwaka 1980, ilihama kutoka kwa wakoloni wa Uingereza (Wazungu) na kuwa chini ya tabaka la Wazimbabwe wachache ambao walijiona wanastahili kuliko wananchi wengine kupitia jina la “wapigania uhuru”.

Mugabe akiwa Waziri Mkuu na Mkuu wa Serikali kuanzia mwaka 1980 mpaka 1987 kisha Mkuu wa Nchi, Amiri Jeshi Mkuu na Mkuu wa Serikali mwaka 1987 mpaka 2017, alilea mfumo huo wa Wazimbabwe wachache kunufaika kuliko walio wengi.

Watu hao, wakiwamo Mnangagwa na Chiwenga walitumika vizuri na Mugabe kukandamiza walio wengi na kutoa fursa nyingi kwa wachache. Hao ambao wamezoea kufaidi kuliko wengi, ndiyo ambao leo wanagombana ili kuulinda upendeleo waliozoea.

Hiyo inakupa tafsiri kuwa Zimbabwe mabadiliko ni vigumu kutokea kutokana na mazoea ambayo wamejitengenezea. Hawataki kutengeneza nchi iwe ya fursa sawa kwa kila mwananchi, wanahitaji taifa libaki kuwa la wakoloni weusi wenye jina la “wapigania uhuru”.

Ni kama ambavyo vijana wa Zanu-PF na wengine ambao walimtaka Grace, waliona bora nchi iwe kwenye hakimiliki ya familia ya Mugabe kuliko kukabidhiwa mtu ambaye ni jamii ileile ya maveterani waliopigania uhuru wa nchi. Kwao, utawala kuondoka kwenye tabaka hilo ni ukombozi wa mara ya pili.

Mnangagwa ni nani?

Akiwa na umri wa miaka 75 sasa, Mnangagwa alikuwa na siri ambayo ilidhihirika kuwa alikusudia kumrithi Mugabe ambaye bila kujua, alimwamini na kumteua nafasi nyeti serikalini mpaka kufikia hatua ya kumfanya kuwa Makamu wa Rais.

Kitabia Mnangagwa anatajwa ndani ya Zanu-PF kuwa ni mkorofi mno, hivyo watu wengi hawampendi. Hata hivyo, linapokuja suala la mnyukano na Grace, kisha kuona Jeshi kama lipo pamoja naye, wanaona bora huyohuyo Mnangagwa ili kutetea masilahi yao.

Mnangagwa ni mwanamapinduzi hasa, ni mwanajeshi na jasusi aliyepitia mafunzo Misri na China. Alikuwa mpiganaji wa mstari wa mbele katika vita ya ukombozi Zimbabwe miaka ya 1970 mpaka mwaka 1980, nchi ilipokabidhiwa uhuru wake.

Ni mtu wa jamii ya Karanga ambalo ni kundi dogo katika kabila la Washona. Kwa Wakaranga mamba huaminika ni mwenye nguvu kubwa kiimani. Hiyo ndiyo sababu Mnangagwa huitwa kwa utani Mamba. Kampuni ya mavazi ya Lacoste, nembo yake ni mamba, hivyo wafuasi wa Mnangagwa hujiita Lacoste.

Miaka ya 1970, Mnangagwa aliwahi kukamatwa na kuteswa na Waingereza chini ya Serikali ya Rhodesia Kusini, ambavyo ndivyo Zimbabwe ilitambulika hivyo wakati huo. Mnangagwa alikamatwa na kuteswa kwa sababu aliasisi kikosi alichokiita Crocodile Gang (Genge la Mamba) na kuliongoza kupambana na wakoloni.

Miaka 1980, Mnangagwa alikuwa sababu ya vifo vingi vya wafuasi wa chama cha Zapu waliopingana na Zanu-PF cha Mugabe katika vita ya kiraia Zimbabwe. Mnangagwa ndiye aliyekuwa gwiji la ushushushu na kuua watu wengi wasio na hatia. Vurugu nyingi za kudhibiti wapinzani, zilitekelezwa na Mnangagwa.

Mbunge wa Jimbo la Kwekwe Kati, Blessing Chebundo, alipata kusimulia kuhusu Mnangagwa: “Yule mtu siyo wa amani. Wakati wa kampeni za ubunge mwaka 2000, alipoona naelekea kumshinda alituma vijana wa Zanu-PF waniue kwa petroli, nikatoroka kimiujiza na baadaye nikamshinda.”

Huyo ndiye Mnangagwa, ambaye amesababisha nchi iingie kwenye misukosuko na hata kumuweka Mugabe katika mlango wa kutoka. Huyo ndiye Mnangagwa ambaye bila shaka anachukiwa mno na Grace.