MAONI YA MHARIRI: Mkakati uandaliwe kuhamia Dodoma

Muktasari:

Mpango huo ulitangazwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza mwaka 1973, wakati ambao viongozi wengi wa nchi za Afrika walitaka kujenga Afrika mpya yenye serikali zinazojiendesha kwa kuangalia maslahi mapana ya nchi kuliko ya kibiashara zaidi kama walivyokuwa wakoloni.

Katika toleo la gazeti hili la Julai 16 mwaka huu tuliandika maoni ya kupongeza uamuzi wa Rais John Magufuli kufufua mpango wa kuhamishia makao makuu ya Serikali mkoani Dodoma ulioanzishwa miaka takriban 42 iliyopita.

Mpango huo ulitangazwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza mwaka 1973, wakati ambao viongozi wengi wa nchi za Afrika walitaka kujenga Afrika mpya yenye serikali zinazojiendesha kwa kuangalia maslahi mapana ya nchi kuliko ya kibiashara zaidi kama walivyokuwa wakoloni.

Serikali ya Awamu ya Kwanza ilianza rasmi kutekeleza mpango huo baada ya kukamilishwa kwa ramani ya mpango mji mwaka 1976, lakini safari hiyo ya kuhamia Dodoma ilikumbana na vikwazo vingi vilivyosababisha isitekelezwe kwa kadri ya matarajio.

Vikwazo hivyo ni pamoja na vita vya Kagera vilivyofuatiwa na kipindi cha kujifunga mkanda kubana matumizi, bei ya mafuta kupanda na kuyumba kwa uchumi wa dunia.

Vikwazo hivyo pamoja na vingine vingi ilisababisha Serikali ishindwe kujipanga kuweka takribani Sh300 milioni kila mwaka kukamilisha safari hiyo ya miaka kumi.

Lakini baada ya kuondokana na vikwazo hivyo, safari ya Dodoma haikufufuliwa licha ya kutajwatajwa kwenye vikao vya Serikali na Bunge kuwa mpango wa kuhamia Dodoma uko palepale.

Pamoja na kutoa pongezi hizo, tumeona ni vizuri pia kutoa tahadhari ili kutekelezwa kwa mpango huo kufanyike kwa njia ambayo itakuwa safi na salama.

Rais ametangaza kuwa katika kipindi cha miaka minne na miezi minne, Serikali yake itakuwa imeshahamia Dodoma, na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akaongeza kuwa atahamia Dodoma ifikapo mwezi Septemba.

Ni uamuzi thabiti kuwa katika kipindi hicho kifupi, Serikali iwe imeshahamishia makao yake mjini Dodoma, lakini uwezo wa kutekeleza hilo upo au utekelezwaji wake utafanywa kwa nguvu zote bila ya kujali athari zitakazotokana na mpango huo.

Katika kipindi hiki ambacho bajeti ya Serikali haijajumuisha suala hilo, ni dhahiri kuwa utekelezwaji wa mpango huo unaweza kuwa wa kuzuia shughuli fulanifulani zilizokwishapangwa kwenye bajeti hii na kuhamishia fedha kwenye mpango huo.

Kama mpango wa maendeleo wa miaka mitano haujajumuisha suala hilo, ni dhahiri kuwa utekelezwaji wake utaumiza baadhi ya sekta ambazo viongozi wakuu wa Serikali watadhani kuwa si muhimu katika kipindi hicho kilichobaki cha miaka minne na miezi minne.

Pia katika kipindi hiki mkoa wa Dodoma umejiandaa vipi kupokea ugeni wa wafanyakazi watakaolazimika kuhamia Dodoma. Maandalizi hayo ni kama miundombinu ya huduma za jamii kama barabara, maji, mawasiliano, shule, nishati na hospitali.

Ni kwa kiasi gani mkoa umejiandaa kwa makazi, majengo ya ofisi na masuala mengine yanayotakiwa kwa ajili ya makao makuu ya Serikali.

Hivi sasa, Serikali imeshaanza kuziandikia taasisi zake kuhusu utekelezwaji wa mpango aliotangaza Rais. Kuna mpango gani wa kutekeleza agizo hilo? Kwamba wizara zote ziwe zimeshahamia Dodoma ifikapo Septemba au utatekelezwa kwa awamu?

Hakuna shaka kuwa mpango wa kuhamia Dodoma ni mzuri kwa kuwa sababu zilizosababisha kufikia uamuzi huo bado zipo palepale na umuhimu ni uleule kuwa utasaidia kusogeza huduma za Serikali kwa wananchi wengi.

Pamoja na umuhimu huo, tunashauri kuwa tamko la Rais la kutaka Serikali iwe imehamia Dodoma ifikapo mwaka 2020, litengenezewe mkakati thabiti wa utekelezaji ambao hautaathiri baadhi ya sekta na wananchi kwa ujumla.