Mkakati wa kupambana na mbumbumbu Ruvuma

Baadhi ya walimu mkoani Ruvuma wakiwa katika mafunzo ya kufundisha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu. Na Mpiga picha wetu.

Muktasari:

  • Walimu wapewa mbinu mpya za kufundisha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu

Tatizo la wanafunzi wa shule za msingi, wakiwamo wahitimu wa darasa la saba kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu, linazidi kushika kasi kiasi cha kuwashughulisha wadau wengi wa elimu nchini.

Ni changamoto ya kitaifa kwa kuwa kila kona ya nchi, habari ya wanafunzi kutojua stadi hizi muhimu katika maisha zimetamalaki.

Kwa mfano, Aprili mwaka 2012, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ilibaini kuwepo kwa wanafunzi 5200 waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari wakiwa hawajui kusoma wala kuandika.Baada ya tukio hilo, Serikali ikaagiza wakuu wa shule kuendesha mitihani ya mchujo kwa wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanzam, kwa minajili ya kuwaengua wanafunzi mbumbumbu.

Pamoja na jitihada za Serikali na hata wadau wengine, utafiti unaonyesha tatizo la wanafunzi kutojua stadi hizi maarufu kwa kifupi cha KKK, linaendelea kukua katika shule mbalimbali nchini.Miongoni mwa wadau wanaolifuatilia kwa karibu suala hili ni asasi ya kiraia ya Twaweza kupitia programu yake ya Uwezo.

Tangu mwaka 2010, asasi hiyo inayofanya kazi zake pia katika nchi za Kenya na Uganda, imekuwa ikifanya utafiti kila mwaka kubaini ukubwa wa tatizo. Kila mwaka Uwezo inapotoa ripoti zake, matokeo huwa sio mazuri kwa kiwango cha kuridhisha.

Hali ilivyo mkoani Ruvuma

Takwimu za Mkoa wa Ruvuma kwa mwaka 2015, zinaonyesha kuwapo kwa wanafunzi 7,339 wa darasa la kwanza ambao hawakujua kusoma kati ya wanafunzi 43,951 waliosajiliwa. Kwa wanafunzi wa darasa la pili waliobainika walikuwa 4373 kati ya 40, 717.

Mwaka 2016, wasiojua kusoma kwa darasa la kwanza walikuwa 6,392 na la pili wakiwa 4,563. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Ofisa Elimu wa mkoa huo, Kinderu Said.

Kwa sababu hii, shirika la Misaada la Marekani (USAID), limeanzisha mkakati uitwao Tusome Pamoja ambao pamoja na mambo mengine unalenga kutoa mafunzo kwa walimu wanaofundisha madarasa ya chini, msisitizo ukiwa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.

“Kupitia mafunzo haya tumeanza kuona mafanikio ya wanafunzi wanaoingia darasa la tatu, huku wakijua kusoma kuandika na hisabati kwa sababu ya uwingi wa vifaa vya kufundishia hasa vitabu pamoja na elimu waliyoipata walimu hawa,”anasema Kinderu na kuongeza:

“Changamoto kubwa ambayo itakuwepo ni ufaulu wa wanafunzi kuwa mkubwa, hapo sasa tatizo litakuwa ni madarasa ila ufumbuzi tayari umeanza kwa kuanza ujenzi wa madarasa ya sekondari.” Anasema mradi huo pia umeanzisha harakati za ushirikishwaji wa wazazi walimu na wanafunzi.

‘’Wazazi sasa wameanza kushirikiana na walimu katika kujua maendeleo ya watoto wao na kutokana na juhudi hii, watoto wanasoma sababu wanaelewa wazazi wao wapo karibu na wanafuatilia maendeleo yao shuleni,’’ anaongeza kusema.

Mshauri mkuu wa mradi Stevin John Msabaha anasema malengo makuu ya mradi ni kuunga mkono jitihada za Serikali ili kuweza kufikia lengo la kuondoa kabisa tatizo la wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika kwa darasa la kwanza na la pili ifikapo mwaka 2021.

Ukiondoa Ruvuma, anasema mradi huu unafanyika pia katika mikoa ya Mtwara, Iringa, Morogoro na Zanzibar.

“Lengo jingine ni kuisaidia Serikali kwa kuwapatia walimu mbinu za ufundishaji pamoja na vifaa vya kujifunzia ili kuinua kiwango cha elimu nchini,’’ anasema.

Msabaha anaongeza kuwa programu hiyo itahakikisha kila mwanafunzi wa ngazi ya darasa la kwanza na la pili anajua kusoma kuandika na kufanya hesabu anapoingia darasa la tatu .

Wasemavyo walimu

Mwalimu Bosco Mapunda wa Shule ya Msingi Sabasaba, anasema tangu wapate mafunzo kumekuwapo mabadiliko ya usomaji kwa wanafunzi, huku kila siku hali ikiboreka.

“Wametufunza ufundishaji wa sauti, silabi neno na sentensi. Kwa mpangilio huu, mtoto lazima atajua sauti ya silabi na alphabeti na mwishowe kuzitumia hizo kupata sentensi,’’ anasema.