Mkataba tata wa EPA unavyoiadhibu nchi ya Kenya

Viongozi wakuu wa nchi za Afrika ya Mashariki wakisimama wakati wimbo wa umoja wa nchi hizo ukipigwa katika mkutano wa 17 wa EAC uliofanyika mkoani Arusha, Machi 2, 2017. Picha na Maktaba

Muktasari:

EPA NI KITU GANI?

Huu ni mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Umoja wa Ulaya (EU) na nchi wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaolenga kufungua masoko hapa Afrika Mashariki kwa bidhaa za viwanda vya Ulaya na bidhaa Afrika Mashariki kupata masoko Ulaya.

Mkataba huu unatakiwa kuridhiwa na nchi zote wanachama wa EAC ili uanze kutumika rasmi kwa kufungua masoko katika pande zote. Nchi za Afrika Mashariki zinazotakiwa kutia saini ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini.

Kwa kuwa Ulaya imeendelea kiviwanda, mkataba huo unaonekana utawanufaisha wao zaidi kwa kuleta bidhaa zao Afrika Mashariki bila kutozwa kodi. Nchi za Afrika Mashariki bado hazijaendelea kiviwanda hivyo hazina bidhaa nyingi za kupeleka Ulaya.

Tanzania imebainisha wazi kwamba haitatia saini mkataba huo kwa sababu unatishia maslahi katika mpango wake wa kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025.

Ikikubali kusaini mkataba huo, bidhaa za Tanzania zitashindwa kuhimili ushindani na bidhaa kutoka Ulaya.

Kenya ambayo tayari imetia saini mkataba huo, inanufaika na soko la Ulaya kwa kuuza bidhaa za maua na mbogamboga. Hata hivyo, manufaa kwao yatakuwa kidogo kwa sababu wanazalisha bidhaa kidogo kuliko nchi za Ulaya.

Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (Epa) kati ya Umoja wa Ulaya (EU) na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaendelea kuwa kaa la moto kwa wakuu wa nchi hizo kushindwa kuafikiana.

Mkataba huo ambao mchakato wake ulianza mwaka 2010, ulitakiwa kusainiwa Oktoba, 2016 lakini wakuu wa nchi za EAC wakajipa muda zaidi wa kutafakari suala hilo na kukubaliana kukutana tena Januari, mwaka huu wakiwa na majibu.

Hata hivyo, ilipofika Januari nchi hizo ziliendelea kushikilia misimamo tofauti, huku kila moja ikiangalia masilahi yake binafsi. Pengine hilo ndilo jambo pekee linalosababisha ugumu wa kuwa na msimamo wa pamoja na kuzifanya Kenya na Rwanda kuwa pekee zilizotia saini mkataba huo.

Tanzania imeweka wazi kwamba vipengele vya mkataba wa Epa vitaikwamisha kufikia azma yake ya kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025 kwa sababu moja ya vipengele vya mkataba huo kinataka bidhaa zote kutoka Ulaya ziruhusiwe kuingia katika nchi yoyote ya Afrika Mashariki.

Burundi nayo haitaki kusaini mkataba huo kwa sababu tayari imewekewa vikwazo na EU kutokana na mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini humo. Kama ilivyo kwa nchi za EAC, Burundi inataka Umoja wa Ulaya uondoe vikwazo vyake kwanza ndipo suala la Epa lijadiliwe.

Kenya ambayo tayari imesaini mkataba huo sasa inaadhibiwa na EU kwa bidhaa zake za mbogamboga na maua kutozwa kodi ambayo awali haikuwapo.

Lengo la EU ni kutaka nchi hiyo ambayo ndiyo yenye uchumi mkubwa Afrika Mashariki kushinikiza mataifa mengine kusaini mkataba wa Epa.

 

Mkataba huo hauwezi kutumika mpaka nchi zote wanachama wa EAC watakapotia saini kwa pamoja kukubali kufungua masoko. Kenya iko tayari kwa sababu inanufaika kwa kuuza bidhaa zake nchi za Ulaya.

Nchi za Uganda na Sudani Kusini bado hazijasaini lakini ziko tayari kujadiliana ili kuona manufaa ya mkataba huo kabla ya kufanya uamuzi. Kwa upande wa Rwanda, tayari imesaini mkataba huo lakini iko tayari kwa majadiliano zaidi.

Kauli za wakuu wa nchi

Moja ya ajenda za mkutano wa kawaida wa 18 wa EAC uliowakutanisha wakuu wa nchi wiki iliyopita jijini Dar es Salaam ilikuwa kujadili suala la Epa. Hata hivyo hawakuweza kufikia mwafaka kwa sababu zilezile zinazowatofautisha.

Mwenyekiti wa EAC aliyemaliza muda wake, Rais John Magufuli anasema suala la Epa limekuwa gumu kwa sababu lina vipengele vinavyozibana nchi za Afrika Mashariki na pia wanachama wa EU hawapo pamoja ndiyo maana Uingereza imejitoa.

“Mkataka huu una masharti mengi, tunahitaji muda wa kuyasoma na kufanyia mabadiliko ili yasituumize. Pia Jumuiya ya Ulaya wameiwekea embargo (vikwazo) Burundi wakati Burundi nayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuna mambo mengi ya kuangalia hapa,” anasema Rais Magufuli.

Anasisitiza kuwa ana imani kuwa Rais wa Uganda, Yoweri Museven ambaye ndiye mwenyekiti mpya wa EAC ataendeleza mazungumza vizuri kwa sababu ana uzoefu wa muda mrefu na ni mmoja wa waasisi wa EAC iliyoanzishwa mwaka 2000 baada ya ile ya awali kuvunjika mwaka 1977.

Katika mazungumzo yao, mkutano huo uliowakutanisha wakuu wawili wa nchi wanachama (Rais Magufuli na Museveni),  Kenya iliwakilishwa na Naibu Rais William Ruto wakati Burundi ikiwakilishwa na Makamu wa kwanza wa Rais, Gaston Sindimwo.

Waziri wa Viwanda, Biashara na EAC, Francois Kanimba aliiwakilisha Rwanda katika mkutano huo wakati Mshauri wa Mambo ya Kiuchumi wa Rais wa Sudan Kusini, Dk Aggrey Tisa Sabuni aliiwakilisha nchi hiyo.

Waenda kuzitetea Kenya, Burundi

Makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano huo ni kwamba ndani ya mwezi mmoja, mwenyekiti wa EAC (Rais Museveni) pamoja na ujumbe kutoka sekretarieti ya EAC waende Brussels, Ubelgiji kuiambia EU iache kuiadhibu Kenya kwa sababu suala la Epa bado linajadiliwa.

Rais Museveni anasema kuendelea kuiadhibu Kenya kwa sababu ya ukubwa wao (kiuchumi) sio suluhisho la kuzifanya nchi nyingine zitie saini mkataba huo wenye utata.

Hata hivyo, anaonya kwamba EU ikiendelea na msimamo wake itakwamisha jitihada za mazungumzo kuhusu mkataba huo.

“Hatuwezi kuendelea na majadiliano wakati mwenzetu mmoja amebanwa. Nimeambiwa niende huko Brussels kuongea na hao wakubwa. Hili suala la Epa bado tunalifanyia kazi na tunahitaji kuzungumza nao tuone kama tunaweza kufanyia mabadiliko baadhi ya vifungu,” anasema mwenyekiti huyo wa EAC.

Suala jingine ni kuitaka EU kuiondolea vikwazo Burundi kwa sababu nayo ni mmoja wa nchi wanachama ambao wanatakiwa kutia saini mkataba huo. Vikwazo vya EU kwa Burundi ni moja ya vikwazo vinavyokwamisha mkataba huo kusainiwa.

“Burundi naye ni mwenzetu na anasema hawezi kujadili suala la Epa wakati tayari amewekewa vikwazo. Tunawataka EU waondoe vikwazo kwa Burundi, hili siyo suala la kuweka saini mara moja wakati bado hatuko pamoja,” anasema Rais Museven.

Magufuli akabidhi uenyekiti

Tanzania imekuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa miaka miwili mfululizo. Mara ya kwanza ilikuwa Februari 2015 wakati wa Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.

Rais Magufuli aliendelea kuwa mwenyekiti wa EAC baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 kabla ya kuongezewa mwaka mmoja na wakuu wa nchi wanachama ilipofika Machi, mwaka jana.

Mafanikio ya uongozi wake

Kabla ya kukabidhi madaraka hayo, Rais Magufuli anabainisha mafanikio mbalimbali yaliyopatikana wakati Tanzania ikiwa mwenyekiti ambayo ni ujenzi wa miundombinu, ukuzaji wa uchumi, amani na usalama wa jumuiya na kuundwa kwa Tume ya Usimamizi na Ufuatiliaji.

Jambo jingine anasema wamefanikiwa kupunguza matumizi kutoka Dola 12.6 milioni za Marekani kwa mwaka hadi kufikia Dola 9.1 milioni na kuokoa kiasi cha Dola 3.41 milioni ambazo zilikuwa zikitumika kwenye mambo yasiyo muhimu.

“Ninawapongeza sana sekretarieti ikiongozwa na Secretary General (Katibu Mkuu), Liberat Mfumukeko. Wamefanya kazi kubwa kuondoa matumizi yasiyo ya lazima lakini pia kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kimataifa,” anasema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Rais Museveni anasisitiza juu ya umuhimu wa ushirikiano ndani ya jumuiya na kwamba jumuiya hii ina maana kubwa tatu ambazo ni maendeleo (kiuchumi), usalama na undugu baina ya wananchi wa Afrika Mashariki.

Anasema waasisi wa jumuiya hii walizingatia mambo hayo matatu ambayo ndiyo msingi mkuu wa kuanzishwa kwake. Rais Museveni anasisitiza kwamba lazima mambo hayo yaendelezwe na kusimamiwa vizuri ili yawe na manufaa kwa taifa.

“Sisi wote ni ndugu hata makabila yetu ya kibantu yanafanana. Kuna historia ya wabantu wa kando ya ziwa, tunasikilizana katika baadhi ya matamshi ya maneno. Huu ndiyo undugu,” anasema kiongozi huyo mkongwe barani Afrika.