Mkoa wa kilimo, mifugo, utalii

Muktasari:

  • Umepakana na mikoa ya Pwani na Lindi kwa upande wa Mashariki, Manyara na Tanga upande wa Kaskazini na kwa Magharibi, umepakana na mikoa ya Dodoma na Iringa. Kusini unapakana na Mkoa wa Ruvuma.

Morogoro ni mkoa wa pili kwa ukubwa nchini ukitanguliwa na Tabora. Mkoa una eneo la kilomita za mraba 73,039. Ni sawa na asilimia 7.7 ya eneo lote la Tanzania Bara, kati ya eneo hili, kilomita 22,240 ni eneo la maji.

Umepakana na mikoa ya Pwani na Lindi kwa upande wa Mashariki, Manyara na Tanga upande wa Kaskazini na kwa Magharibi, umepakana na mikoa ya Dodoma na Iringa. Kusini unapakana na Mkoa wa Ruvuma.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, idadi ya kaya za Mkoa wa Morogoro ni 489,688 zenye watu 2,218,492 na kati yao wanawake ni 1,125,190 na wanaume 1,093,302. Wastani wa idadi ya watu katika kaya ni 4.5.

Fursa zilizopo

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe anasema kuna fursa nyingi za kiuchumi katika kilimo cha mpunga, mahindi, maharagwe, alizeti, mbogamboga na matunda.

Anasema, pia mkoa wake una vivutio vya utalii vinavyoweza kuajiri vijana; Hifadhi ya Mikumi, Pori la Hifadhi la Selous, Milima Udzungwa, Maporomoko ya maji ya Kihululu na Kinole, lakini pia kuna chemchem ya maji moto ya Kisaki.

Anasema Morogoro ina uoto mzuri wa asili na misitu mingi. Pia wapo wajasiriamali waliowekeza kwenye ufugaji wa nyuki katika wilaya za Kilosa, Kilombero Ulanga na Mvomero. Katika kuhakikisha kuwa fursa hizo zinatangazwa na kuchangamkiwa, Dk Kebwe anasema: “Serikali mkoani hapa imeandaa kongamano la uwekezaji ambalo linatarajiwa kufanyika mwishoni mwa Septemba kuhamasisha uwekezaji. Tunatarajia washiriki kutoka zaidi ya nchi 20 ambao tutawaeleza kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo Morogoro.”

Kilimo

Morogoro ina fursa kubwa katika sekta ya kilimo na mikakati iliyopo kwa mujibu wa mpango kazi wa mkoa ni kuboresha na kuharakisha kupatikana kwa hali bora ya uchumi na maisha ya mwananchi kupitia mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) hasa ikizingatiwa kwamba una eneo la hekta 2,226,396 linalofaa kwa kilimo kati yake wastani wa hekta 789,007 sawa na asilimia 35.4 tu ndizo zinazolimwa.

Asilimia 76 ya wakazi wa Morogoro hujishughulisha na kilimo cha mazao mbalimbali yakiwamo mahindi, mpunga, migomba, uwele na mtama kwa ajili ya chakula na mazao ya biashara kama pamba, ufuta, alizeti, kahawa, korosho, viungo, mboga na matunda.

Ghala la chakula

Utekelezaji wa Mpango wa Fanya Morogoro kuwa Ghala la Taifa la chakula (Famogata), unazingatia nguzo kuu 10 za Kilimo Kwanza na mkoa uliandaa mkakati mahsusi mwaka 2009 ikiwa ni njia mojawapo ya kuanza utekelezaji wa kilimo kwa kuzingatia tija kwa kufuata sera na maelekezo ya Serikali pamoja na mikakati inayoongoza ukuaji wa sekta ya uchumi ambayo ni Dira ya Maendeleo 2025.

Tangu utekelezaji wa Famogata 2006/2007 ulipoanza, uzalishaji wa mazao ya chakula umekuwa ukiongezeka kutoka tani 957,661.00 zilizolimwa katika hekta 344,797.00 hadi kufikia tani 2,210,988.00 zilizolimwa katika hekta 659,660.00.

Katika Msimu wa mwaka 2014/2015 Mkoa umelenga kulima hekta 713,882 ili kuvuna tani 2, 691, 282.00 za mazao ya chakula na kwa upande wa mazao ya biashara lengo ni kulima hekta 174,887 ili kuvuna tani 3, 183, 072.00.