Mkulima Market: mkombozi mwingine wa wakulima, wafugaji nchini

Baadhi ya wajasiriamali walioshiriki katika soko la wazi la kilimo (Mkulima Market), liliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

Uzoefu unaonyesha mazao mengi yamekuwa yakiozea shambani na hata yanayobahatika kufika sokoni yanakosa wanunuzi au yanauzwa kwa bei ndogo isiyokuwa na masilahi kwa wakulima.

Miongoni mwa changamoto nyingi ambazo kwa kipindi kirefu zimekuwa zikiwakabili wakulima ni namna ya kupata masoko ya bidhaa zao.

Uzoefu unaonyesha mazao mengi yamekuwa yakiozea shambani na hata yanayobahatika kufika sokoni yanakosa wanunuzi au yanauzwa kwa bei ndogo isiyokuwa na masilahi kwa wakulima.

Uko mfano wa kuelekea mwishoni mwa mwaka jana, baada ya mitandao mingi ya kijamii kuonyesha picha za marundo ya nyanya zikiwa zimetelekezwa na wakulima baada ya kukosa wanunuzi.

Katika kuhakikisha wakulima wanakuwa na sehemu ya kutatua changamoto za ukosefu wa masoko hasa kwa wakulima, asasi isiyo ya kiserikali ya Mkulima Market imeandaa soko la wazi kwa wakulima wadogo, jambo linalotoa fursa kwa wazalishaji kutangaza bidhaa zao.

Akizungumza soko hilo litakalokuwa liki fanyika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwandaaji na msimamizi wa soko hilo, Vicensia Shule anasema ni endelevu, linalenga kumsaidia mkulima wa chini kupata soko la kuuza bidhaa zake na hatimaye kujikwamua kiuchumi.

Shule anasema nafasi kama hii ni muhimu kwani ina mchango mkubwa kwa wakulima wasio na uwezo kutangazia nembo zao (brands) jambo ambalo litawawezesha kufahamika kibiashara.

“Tunachokifanya ni kuhakikisha kila mjasiriamali anapata nafasi kushiriki soko hilo ili aweze kukutana na wanunuzi wake kulingana na bajeti tulioiandaa. Hii ina nguvu kwani bidhaa zao zinaweza kupata wateja wa kudumu” anasema.

Anaongeza kuwa uhaba wa masoko kwa wakulima wadogo utapunguzwa kwa uwepo wa soko hili, kwani litakuwa endelevu hadi pale shida ya masoko kwa bidhaa za kilimo itakapoisha au kupungua kwa kiasi kikubwa.

Mmoja wa waandaaji wa soko hilo ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kilimo na mazingira, Dk Pamba Siajali,

anasema wamebuni wazo hilo ili kusaidia wakulima kufanya kilimo chao kwa manufaa mapana zaidi.

“Sisi ni kama kiwanda cha kuandaa wataalamu katika mambo mbalimbali yanayohusu kilimo na ufugaji. Tuna nafasi katika soko ya kuwapa elimu na ushauri kuhusu namna ya kuboresha bidhaa zao au kufanya ufugaji uwe wa kisasa ili kuwawezesha kupata faida zaidi,” anasema.

Aidha, anasema soko hilo litahusisha mafunzo kwa wakulima kuelimishwa namna ya kupata vibali kutoka Shirika la Viwango (TBS) kwa ajili ya kuwezesha bidhaa zao kutambulika rasmi.

Soko la kwanza

Desemba 21 hadi 24 mwaka jana, soko hilo lilianza katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kushirikisha makundi 73 ya wakulima na wajasiriamali kutoka mikoa ya Tanga, Arusha, Pwani, Morogoro na Dar es Salaam.

Akizungumzia mapokeo ya soko hilo, Dk Shule anasema tamasha hilo lilikuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa biashara zilifana huku asilimia kubwa ya wafanyabiashara wakitengeneza faida ya kutosha.

Anasema japo ni mara ya kwanza, mwitiko wa wajasiriamali na hata wanunuzi ulikuwa mkubwa.

“Wafanyabiashara walifurahi na kila siku napokea simu za pongezi, huku wakisema wapo tayari kurudi hata kesho,” anasema.

Anasema kufuatia matokeo chanya, wameamua kufanya soko hilo mara nne kwa mwaka badala ya mara moja. Soko la kwanza kwa mwaka huu anasema litafanyika Aprili 4.

Aidha, anaeleza kuwa soko hilo litakuwa likizunguka mikoani kwa lengo la kuwawezesha wakulima zaidi kutangaza bidhaa zao. “Kuanzia Aprili 3 hadi 9 tutakuwa na soko mkoani Simiyu, hivyo ni wazi kuwa idadi kubwa ya wafanyabiashara watapata nafasi ya kujitangaza,” anasema.

Changamoto

Kuhusu changamoto za kuandaa tukio hilo la aina yake kwa mara ya kwanza anasema: “Hakuna changamoto isipokuwa ushamba wetu tu. Sisi tulioandaa soko siyo wakulima wala wafugaji, lakini tunaamini kuwa masoko yajayo kila kitu kitakaa sawa.”

Wasemavyo washiriki

Valelia Mark ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara wa asasi ya Nzua inayojishughulisha na ufugaji wa kuku wa kienyeji anasema:

“Kutafuta soko la kuuza bidhaa zako si jambo rahisi, hivyo nimefurahia soko hili kwani biashara inaenda vizuri na wateja wanafurahia kununua kuku wetu.”

Mfanyabiashara wa matunda Mwanaidi issa anasema kinachosababisha wafanyabiashara na wakulima wadogo kushindwa kujikwamua kiuchumi ni kutokana na kukosekana kwa masoko ya uhakika, jambo ambalo kwa kipindi kirefu limekuwa likiwavunja moyo wakulima.

“Mkulima Market ni msaada mkubwa kwa wakulima wadogo ambao hawawezi kuzitangaza bidhaa zao na kutanua soko lao, lakini kwa sasa wateja wamefurahia bidhaa zangu na wamechukua namba zangu kwa ajili ya mawasiliano,’’ anaeleza.

Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Godluck Mwanyika, anayejihusisha na utengenezaji wa bidhaa kama viatu, mashati ya batiki anasema ni vizuri tamasha hilo likawa endelevu kwani limewawezesha wajasiriamali wapya kupata nafasi ya kutangaza bidhaa zao.

“Ili wajasiriamali wapya waweze kunufaika na kazi zao wanahitaji misaada ya kuwawezesha kujitangazia kazi zao au bidhaa na soko hili limetuwezesha kufanya hivyo,” anasema.

Wasemavyo wanunuzi

Maria Mpulule anasema soko lilikuwa zuri na waandaaji wameliweka sehemu ambayo ni salama.

“Nimenunua vitu mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, pia nimepata elimu ya namna ya kutunza kuandaa na kutengeneza bidhaa, hivyo nimejua kuwa mimi naweza kutengeneza na kupata faida,” anasema.

Anasema ni jambo zuri kama Serikali itaanzisha matamasha kama hayo yatakayokuwa na mchango mkubwa wa kuwainua wakulima wadogo na wajasiriamali kutangaza bidhaa zao.