Mourinho: Nitaleta Picha ya Ferguson

Kocha mpya wa Manchester United,Jose Mourinho

Muktasari:

Kocha huyo alisema wiki iliyopita kuwa mpango atakaoanza nao ni kufanya usajili wa kufa mtu, utakaoibeba klabu hiyo akifananisha na mvinyo bora. “Kama ukipanda mbegu bora za zabibu, utapata divai bora, ninachotaka mashabiki wawe wastahimilivu.

LONDON, England .Kocha mpya wa Manchester United, amerudia kusema msimu ujao, utakuwa mwendo wa ushindi sanjari na falsafa mbalimbali zilizotumiwa na kocha Sir Alex Ferguson kuipa vikombe timu yake.

Kocha huyo alisema wiki iliyopita kuwa mpango atakaoanza nao ni kufanya usajili wa kufa mtu, utakaoibeba klabu hiyo akifananisha na mvinyo bora. “Kama ukipanda mbegu bora za zabibu, utapata divai bora, ninachotaka mashabiki wawe wastahimilivu.

Anasema kupanda zabibu hadi kuvuna na kupata divai, kunahitaji muda kwa hiyo kinachotakiwa ni kutulia kukanyaga alimopita Ferguson hasa kwa kuangalia vijana pamoja na kusajili wakali.

Kuna mpaka wa nadharia ya mafanikio katika michezo na Mourinho alisema anataka kusimamia hapa.

Kocha huyo aliyesaini mkataba wa Pauni 4milioni, alisema anataka kuirudisha Manchester United kama ilivyokuwa siku za nyuma kwa kutumia staili ya ushambuliaji iliyokuwa ikitumiwa na kocha aliyeondoka na mafanikio lukuki, Sir Alex Ferguson.

Mourinho alisema kuwa Old Trafford ina heshima yake na kwamba ilifika hatua mashabiki walichanganyikiwa kutokana na matokeo na staili ya Louis van Gaal.

“Msimu uliopita kocha van Gaal aliwachanganya sana mashabiki, na mimi ni Mourinho ninataka kuirudisha filosofia ya ushambuliajialiyoitumia Ferguson,” alisema.

Kocha huyo alikuwa na mazungumzo na wachezaji wa timu hiyo akiwamo; Wayne Rooney, David De Gea na Michael Carrick na katika mazungumzo, alielezea mkakati wa klabu msimu ujao wa ligi.

Aliweka wazi kuwa mfumo mgumu wa Van Gaal utakuwa historia na sasa anataka kuibadilisha timu, alisema wakati alipohojiwa na gazeti la Mirror.

Mourinho hufundisha soka na kuchezwa kwa taratibu na staili ya aina yake, na kwa hali ilivyo, anataka kuisoma falsafa na utamaduni wa Manchester United.

Akiwa na washambuliaji kama; Zlatan Ibrahimovic na Henrikh Mkhitaryan waliokamilisha usajili, huo unaweza kusema ni msimu wa aina yake kwa mashabiki wa Manchester United.