Mourinho mchecheto tayari

Muktasari:

Hakuwa akiiwazia mechi hiyo na wala hakuwa akimuwazia Wayne Rooney na sakata lake, akili na mawazo yake ni mechi ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Chelsea itakayopigwa Machi 13.


Mawazo mengine! Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho katoa mpya, jana Jumapili timu yake ilikuwa inacheza na Southampton mechi ya fainali ya Kombe la Ligi, lakini mawazo yake hayapo.

Hakuwa akiiwazia mechi hiyo na wala hakuwa akimuwazia Wayne Rooney na sakata lake, akili na mawazo yake ni mechi ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Chelsea itakayopigwa Machi 13.

Kocha huyo ameanza mchecheto na kusema ana wasiwasi na matokeo kwa kuwa ana msongamano wa mechi kabla ya mchezo huo na ratiba inaweza kuchangia timu yake ifanye vibaya.

Ushindi wake wa mabao 2-1 dhidi ya Blackburn haufikirii sana, lakini akasema kichwa chake kimejawa na ratiba ngumu kabla ya kuibukia kwa mpambano huo wa Stamford Bridge.

“Sina cha kujibu,” alisema. “Nimeanza mechi na St Etienne Jumatano, mechi ya Kombe la Ligi Jumapili (jana) halafu wanakuja Bournemouth Machi 4 kisha mechi ya Europa Raundi ya 16 dhidi ya FC Rostov Machi 9 halafu Chelsea Machi 13.”

Ninalazimika kucheza tu ikiwemo mechi hiyo ya Ulaya. Na papo hapo kucheza kuwania nafasi ya nne Ligi Kuu England.

“Chelsea wanalitaka Kombe la FA najua watakomaa tu, kwa kuwa wanataka ubingwa na sisi lazima tupambane.”

Alisema anajua Antonio Conte anataka kumuonyesha Mourinho ambaye timu yake ndiyo bingwa mwaka huu, kocha wa Chelsea anaitazama mechi ya United kwa kujiamini. “Kwanza hana presha ya mchezo na matokeo ya mwisho, Oktoba mwaka jana Chelsea iliifunga Man United 4-0 mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.”

Matokeo hayo yalimuumiza Mourinho kwani kilikuwa kipigo cha mwaka katika historia ya ligi kuu kwake.

Man United imekuwa ikisumbuka kwa Chelsea kwani ilishinda mara mbili Stamford Bridge miaka 15 iliyopita.

Mourinho aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya St Etienne katika Ligi ya Europa na akawataka kukomaa licha ya kuwa na ratiba ngumu.