TUONGEE KILIMO: Mpango wa biashara ya kilimo kwa kaya

Herment Mrema

Muktasari:

Kaya au kikundi kimeamua kuwa na kumbukumbu ya kila shughuli inayofanyika katika kutekeleza biashara zao na kumbukumbu ya gharama zinazotumika katika biashara. Kaya au kikundi kinaelewa kuwa hata ile kazi anayofanya mkulima kusimamia kilimo chake ina gharama na lazima iwe kwenye kumbukumbu na ajilipe kama angemlipa mtu mwingine kwa kazi hiyo.

Kaya au kikundi cha wakulima kuwa na mpango wa biashara ni ishara kuwa wameamua kufanya kilimo cha kibiashara na kuachana na cha mazoea.

Kaya au kikundi kimeamua kuwa na kumbukumbu ya kila shughuli inayofanyika katika kutekeleza biashara zao na kumbukumbu ya gharama zinazotumika katika biashara. Kaya au kikundi kinaelewa kuwa hata ile kazi anayofanya mkulima kusimamia kilimo chake ina gharama na lazima iwe kwenye kumbukumbu na ajilipe kama angemlipa mtu mwingine kwa kazi hiyo.

Mpango biashara wa kilimo kwa kila kaya au kikundi kwa kuanzia inaanza na zao moja ambayo inaorodhesha shughuli zote ambazo zinatakiwa zifanyike ile biashara ya kilimo iwe na uhakika.

Katika shughuli hizo ni pamoja na kuchagua eneo la ardhi ambalo litatumika kwa kilimo, kupima eneo hilo kujua lina ukubwa gani. Kufahamu ukubwa wa ardhi ni muhimu kuelewa kuwa utahitaji maji, mbegu, mbolea, dawa, nguvu kazi, muda wa mashini za kulimia na gharama mbalimbali ili kujua itagharimu kiasi gani kuhudumia shamba

Mpango biashara unaokubalika benki utajenga hoja ya kuwa na mazungumzo na wanunuzi ili kuweka mazingira ya kaya au kikundi kuingia mkataba na msindikaji, na mnunuzi wa bidhaa mara zitakapokuwa tayari.

Mkataba wa biashara na mnunuzi ni muhimu sana kujenga hoja na watoa vitendea kazi kwa mikopo kwa sababu watakuwa na uhakika wa masoko ya vitendea kazi na masoko ya bidhaa zitakazozalishwa. Mpango biashara ni muhimu vilevile kuweza kupata bima ya mazao kwani unaeleza kwa ufasaha ukubwa wa biashara yenyewe na kiasi ya kinga kinachotakiwa kukatiwa bima. Wakulima wenye bima ya mazao wanakuwa na uhakika wa kulipa madeni yao kwani ikiwa majanga yametokea kama kuwa na ukame au mafuriko bima italipa kiasi fulani cha thamani ya biashara iliyoathrika ambayo itaweza kulipa gharama zote zilizotumika.

Mpango biashara vilevile ni ramani ya kuonyesha hatua kwa hatua njia ambayo mkulima akishirikiana na meneja wa mnyororo wa ongezeko la thamani watapitia kupata mafanikio kibiashara.

Mpango biashara unaongeza umakini na unahakikisha kila gharama itakayotumika inatokana na mpango na kila juhudi iliyofanyika itawekewa kumbukumbu.

Mpango biashara unampa mkulima au kikundi nidhamu ya kuweka kumbukumbu na baada ya msimu kutengeneza mahesabu ya mapato na matumizi pamoja na mizania ya hesabu ambayo inampa taarifa juu ya ufanisi wa biashara zake.

Taarifa za utekelezaji wa mpango biashara kwa mkulima na kikundi zinaonyesha ni kiasi gani cha faida iliyopatikana kwa nini faida imekuwa kubwa au ndogo na ni kitu gani kifanyike kuongeza faida kwa msimu ujao.

Taarifa ya mahesabu ya biashara yanampa mkulima au kikundi aina ya kodi na kiasi gani atakachotakiwa kulipa kwa usahihi badala ya kutumia makisio hivyo kufanya biashara kuwa na uhakika zaidi.

Mpango biashara unampa mkulima au kikundi fursa ya kujua kiasi cha raslimali atakazohitaji, mpangilio na muda wa matumizi ya raslimali hizi, na vilevile kujipanga jinsi ya kuzipata, kama ni kukopa benki au kuzipata kwa mkopo kutoka kwa watoa huduma.

Mkulima au kikundi kikiwa na mipango mizuri ya biashara inakuwa rahisi kuingia mikataba na wadau mbali mbali kwa kutumia mipango hiyo na kuwa na uhakika zaidi ya kutekeleza biashara ya kilimo badala ya kufanya ubabaishaji.

Mipango biashara inampa fursa mkulima kumwajibisha mtoa huduma na vitendea kazi ikiwa matokeo ya biashara yatakuwa tofauti na walivyokubaliana hapo awali. Mpango biashara vilevile unajenga hoja ya kupanua au kupunguza kiasi cha biashara kutokana na matokeo na mahesabu ya biashara zenyewe hivyo ni muhimu sana kwa kila kaya na kikundi kuwa na mpango biashara.