Mpango wa pili wa maendeleo miaka mitano uandaliwe

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akiwasilisha mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka wa fedha 2016/17 kwenye mkutano wa wabunge uliofanyika jana, Dar es Salaam.  Picha ya Maktaba.

Muktasari:

Kichwa cha Mpango kinaeleza kuwa mpango huo unahusu Kujenga Uchumi wa Viwanda ili Kuchochea Mageuzi ya Kiuchumi na Maendeleo ya Watu - Nurturing Industrialisation for Economic Transformation and Human Development”.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango amewasilisha Bungeni Mpango wa Pili wa Miaka mitano ambao unapaswa kuwa mwongozo wa Serikali ya Rais John Magufuli kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Kichwa cha Mpango kinaeleza kuwa mpango huo unahusu Kujenga Uchumi wa Viwanda ili Kuchochea Mageuzi ya Kiuchumi na Maendeleo ya Watu - Nurturing Industrialisation for Economic Transformation and Human Development”.

Hata hivyo malengo ya sekta ya viwanda yaliyoainishwa katika jedwali la 4.1 la Mpango yanaonesha Serikali haiko makini kuendeleza viwanda. Mchango wa sekta ya viwanda katika pato la taifa umepangwa uongezeke kutoka asilimia 5.7 mwaka 2015 na kufikia asilimia 5.8 mwaka 2020 na asilimia 5.9 mwaka 2025. Ni wazi malengo hayo hayataleta mabadiliko ya mfumo wa uchumi. Ikiwa haya ndiyo malengo ya mpango wa pili Serikali inawafanyia mzaha Watanzania.

Wakati analizindua Bunge la 11, Rais Magufuli alieleza lengo lake ni kukuza sekta ya viwanda iweze kuajiri asilimia 40 ya nguvukazi mwaka 2020. Mpango wa miaka mitano hauchambui changamoto za kufikia lengo hili.

Lengo la ajira katika sekta ya viwanda haliko wazi. Hotuba ya Waziri haielezi lengo mahsusi la mpango kuhusu idadi au asilimia ya ajira inayotarajiwa kufikiwa ifikapo mwaka 2020.

Ni wazi lengo la Rais la asilimia 40 ya ajira ipatikane viwandani haliwezi kufikiwa ukizingatia sekta ya viwanda hivi sasa inaajiri asilimia 3.1 ya nguvu kazi.

Uingereza, nchi ya kwanza kuwa na mapinduzi ya viwanda ilifikia kilele cha asilimia 45 ya nguvu kazi iliyoajiriwa sekta ya viwanda kabla ya kuanza vita vya kwanza mwaka 1914.

Baada ya hapo mchango wa viwanda kwenye ajira ulipungua na kufikia asilimia 30. Kuanzia miaka ya 1970 Uingereza imepoteza ajira katika sekta ya viwanda na hivi sasa ni asilimia 10 tu ya nguvu kazi inaajiriwa viwandani. Nchini Marekani kilele cha ajira katika sekta ya viwanda kilikuwa asilimia 27 ya nguvu kazi mwishoni mwa vita ya pili baada ya hapo mchango wa ajira katika sekta ya viwanda umepungua.

Ujerumani ambayo ni maarufu kwa umahiri wake wa uhandisi na viwanda ilifikia kilele cha ajira katika sekta ya viwanda cha asilimia 40 mwanzoni mwa miaka ya 1970.

Nchi ya dunia ya tatu iliyofanikiwa mapinduzi ya viwanda ni Korea ya Kusini. Ajira viwandani iliongezeka toka asilimia nane mwaka 1963 mpaka kufikia kilele cha asilimia 28 mwaka 1989 na baada ya hapo imepungua mpaka kufikia asilimia 18.

Lengo la Rais la sekta ya viwanda kuajiri asilimia 40 ya nguvu kazi ni ndoto ya mchana yenye nia nzuri ya kuongeza ajira kwa vijana. Mpango wa pili hausaidii kufanikisha hata robo ya ndoto hii. Hotuba ya Rais alau ilieleza mwongozo mzuri wa viwanda vitakavyojengwa. Viwanda hivyo ni pamoja na vinavyotumia malighafi inayopatikana nchini, viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotumiwa na wananchi wengi, na viwanda vinavyoajiri watu wengi.

Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia ukiongozwa na Profesa Justin Lin wa China aliyekuwa Makamu wa Rais na Mchumi Mkuu wa Benki hiyo umechambua viwanda ambavyo Tanzania inaweza kuwa na ushindani mzuri.

Viwanda vilivyopendekezwa ni vya nguo na mavazi, viatu, bidhaa za ngozi, samani, bidhaa za mbao na za kusindika mazao ya kilimo kama vile nafaka, maziwa, mafuta ya kula, matunda na mbogamboga.

Vingine ni viwanda vya saruji na vifaa vya ujenzi. Hivi vina nafasi nzuri kwa sababu soko la ndani ni kubwa.

Mpango wa pili ungejikita na kufanya uchambuzi wa kina wa mambo ambayo Serikali itayatekeleza kuondoa vikwazo vinavyokwamisha maendeleo ya viwanda hivi.

Viwanda vya nguo vilianza kujengwa nchini tangu mwanzoni mwa miaka ya 1960, lakini uzalishaji umeporomoka. Tunalima pamba hatuzalishi nguo kwa wingi.

Tumekuwa wavaa mitumba. Viwanda vya nguo ndiyo viwanda vyepesi vinavyoanzishwa katika nchi maskini kama Tanzania.

Kabla ya mpango wa miaka mitano unaokamilika hivi sasa uzalishaji wa nguo ulikuwa mita za mraba milioni 141 mwaka 2008.

Baada ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo, Mwaka 2014 tumezalisha mita za mraba milioni 119. Uzalishaji huu ni mdogo sana miaka 53 baada ya uhuru. Kwa nini Serikali inashindwa kusimamia maendeleo ya viwanda vya nguo vinavyoweza kuongeza ajira kwa vijana wetu?

Ukuaji wa uchumi

Mpango wa kwanza wa miaka mitano ulikuwa na lengo la kukuza uchumi kwa asilimia nane kila mwaka. Hata hivyo wastani wa ukuaji wa uchumi katika kipindi cha mpango ni asilimia 6.7. Mpango wa pili haukufanya uchambuzi wa kina wa sababu za kutofikia lengo la ukuaji wa uchumi. Katika kipindi cha mpango wa kwanza mpaka mwaka 2014 sehemu ya pato la taifa iliyowekezwa katika miundombinu na vitega uchumi ilikuwa karibu asilimia 35.

Ukuaji wa pato la taifa ulikuwa mdogo wastani wa asilimia 6.7 ukilinganisha na sehemu kubwa ya pato la taifa lililowekezwa. Uwekezaji umekuwa hauna tija.

Kwa mfano fedha nyingi zimetumiwa katika kuwekeza kwenye kujenga barabara za mabasi yaendayo kasi jijini Dar es Salaam, lakini mpaka sasa hakuna huduma ya mabasi.

Kisiwani Mafia kuna gati lilimalizika kujengwa mwaka 2013 lakini hakuna meli inayotia nanga hapo kwa sababu liko juu zaidi ya mita tano ya usawa wa bahari.

Mpango wa pili hautoi majibu ya namna ya kuongeza ufanisi wa uwekezaji badala yake unazungumzia upungufu wa raslimali fedha.

Kimsingi mpango wa kwanza haukutekelezwa. Kwa mfano Mpango uliweka lengo la kujenga miundombinu ya kufua umeme ifikie MW 2780 mwaka 2015. Mpaka hivi sasa imefikia MW 1,483 tu.

Kuboresha kilimo

Mpango wa kwanza ulisisitiza ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji maji kufikia hekta milioni moja kutoka hekta 345,690. Katika miaka mitano eneo la umwagiliaji limeongezeka na kufikia hekta 461,326.

Pamoja na kauli mbiu ya Kilimo Kwanza, Ukanda wa Kilimo wa Kusini – Southern Agriculture Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT) ni hekta 115,000 ndizo zimeandaliwa kwa umwagiliaji maji kwa muda wa miaka mitano.

Serikali ina nia thabiti ya kuendeleza kilimo au tunabadilisha msamiati kuhusu kilimo? Tulianza na kilimo cha kufa na kupona, tukaletewa Azimio la Iringa la Siasa ni Kilimo, Ikasisitizwa kilimo ni uti wa mgongo na sasa Kilimo Kwanza, lakini hakuna kinachofanyika.

Ujenzi reli ya kati

Mpango wa kwanza ulizungumzia kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa standard gauge. Hotuba ya Waziri anayehusika na Mipango katika Bunge la Bajeti la 2015 alieleza: “katika eneo la miundombinu ya reli shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na: kupata mwekezaji wa kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa cha standard gauge.”

Waziri wa Fedha na Mipango amelieleza Bunge kwamba lengo la Mpango wa miaka mitano ilikuwa kukarabati km 170 tu katika reli yenye kilomita 2707.

Serikali imekarabati kilomita 150 tu. Injini na mabehawa bado ni tatizo. Tumeletewa mabehewa mabovu.

Barabara zetu zinaharibika kwa sababu mizigo inayopaswa kusafirishwa kwa reli inasafirishwa kwa barabara.

Reli ya kati ilisafirisha tani 1,446,000 mwaka 2002, lakini ikasafirisha tani 127,000 tu mwaka 2014. Serikali imeiachia reli ya kati ikiharibika bila kuikarabati.

Sasa inazungumzia kujenga reli mpya ya standard gauge. Imeshindwa kukarabati reli ya zamani itaweza kusimamia ujenzi wa reli mpya?

Waziri wa Fedha na Mipango ameeleza kuwa kuna baadhi ya miradi imepewa sifa kuwa miradi ya kielelezo (flagship projects).

Miongoni mwa miradi hiyo ni Mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma na Mradi wa Chuma Liganga. Mpango wa kwanza ulililenga hivi sasa Tanzania izalishe alau tani milioni 1 za chuma cha pua kila mwaka.

Mpaka sasa hata miundombinu inayopaswa kujengwa na Serikali haijakamilika. Hata wananchi wanaoishi kwenye maeneo ambayo mindombinu itapita na viwanda kujengwa hawajawekewa taratibu za kulipwa fidia.

Kitabu cha Mpango hakichambui miradi kielelezo. Kuna sentensi moja inaelezea makaa ya mawe kwa matumizi ya viwandani na majumbani. Pia, kuna sentensi moja inaelezea umuhimu wa viwanda vya chuma.

Sentensi hizo ziko ukurasa wa 41 wa Kitabu cha Mpango cha Kiingereza. Hivi sasa kuna ziada kubwa ya chuma cha pua na makaa ya mawe katika Soko la Dunia.

Viwanda vya chuma vinafungwa nchi za Ulaya na Marekani kwa sababu ya ushindani mkali wa viwanda vya China. Mpango wa Pili hauna uchambuzi wa kuonyesha kuwa mradi wa makaa ya mawe na chuma utahimili ushindani katika Soko la Dunia.

Ikiwa Rais Magufuli bado ana lengo la kuongeza ajira ya viwanda, Mpango wa Pili wa Miaka Mitano ulivyo sasa hautamsaidia kufikia lengo lake. Ni vyema Mpango ukachambuliwa kwa kina na kuandaliwa upya.