Msaidie hivi mwanao wakati huu wa likizo

Muktasari:

Kuishi na watu wengine wasio sehemu ya familia, tena kwa muda mrefu, si jambo rahisi kwa mtoto. Likizo, kwa muktadha huu, inakuwa kipindi cha furaha.

Likizo imeanza kwa wanafunzi wengi wa shule za msingi na sekondari.

Kwa watoto wa bweni, huu ni wakati wa kuungana na familia zao baada ya miezi kadhaa ya kuwa mbali na nyumbani.

Kuishi na watu wengine wasio sehemu ya familia, tena kwa muda mrefu, si jambo rahisi kwa mtoto. Likizo, kwa muktadha huu, inakuwa kipindi cha furaha.

Kwa watoto wa shule za kutwa, likizo ni fursa ya kupumzika na kufurahia ratiba tofauti na kwenda shule kila siku. Likizo humpa mtoto nafasi ya kutosha kufanya shughuli nyingine za ziada kwa ukaribu na familia.

Kwa jumla, likizo humsaidia mtoto kukusanya nguvu tayari kwa muhula mwingine wa masomo mwaka unapoanza.

Hata hivyo, likizo inaweza kuleta changamoto kadhaa kwa mtoto. Kwanza, ni kubadilika ghafla kwa mazoea. Shule, kwa kawaida, zimeweka utaratibu wa kumsaidia mtoto kujua muda wa kuamka, muda wa kufanya usafi, kupata kifungua kinywa na shughuli nyinginezo za kila siku.

Anaporudi kwenye mazingira yasiyoendeleza mazoea hayo, mtoto anaweza kupata shida ya namna bora ya kuutumia uhuru wake. Uhuru huu usipodhibitiwa, unaweza kusababisha matukio yasiyotarajiwa.

Tutazame namna mzazi unavyoweza kumsaidia mwanawe kuifanya likizo iwe kipindi cha manufaa.

 

Msaidie kutathmini maendeleo yake

Ripoti ya maendeleo ya mtoto kitaaluma, kwa shule nyingi, hupatikana wakati wa likizo. Lengo la ripoti ya taaluma ni kumsaidia mzazi kutambua aina ya msaada anaoweza kumpa mwanawe kwa ajili ya muhula unaofuata.

Hakikisha umeiona ripoti hiyo na kupata muda wa kuijadili kwa kina na mwanao.

Ikiwa maendeleo yake ni mazuri, tambua juhudi zake. Mpe zawadi ndogo inayomtumia ujumbe kuwa unajisikia fahari kwa maendeleo yake. Kutambua jitihada za mtoto ni hamasa ya kufanya vizuri zaidi.

Wakati mwingine matokeo yanaweza kuwa mabaya. Usiwe mwepesi kumkatia tamaa mtoto.

Hata katika mazingira ya kutofanya vizuri, nafasi yako kama mzazi ni kumjenga kisaikolojia na siyo kumlaumu na kumsimanga.

Pamoja na kuzungumza na mwanao kujua namna unavyoweza kumsaidia, bado una wajibu wa kuthibitisha kuwa una imani na uwezo wake.

Wasiliana na walimu wake uelewe tatizo liko wapi na namna unavyoweza kusaidia kulitatua. Pokea ushauri wao na utumie kuweka mikakati madhubuti ya kumsaidia mtoto.

 

Msaidie kutengeneza ratiba ya siku

Ratiba ni zana muhimu katika kumwezesha mtoto kujifunza. Mtoto anaporudiarudia shughuli fulani anajenga hali ya kuelewa matarajio ya wengine kwake.

Ni muhimu kumsaidia kutengeneza ratiba itakayoongoza shughuli zake kwa kipindi chote cha likizo.

Ratiba ya mtoto lazima izingatie umri, matakwa yake pamoja na uhalisia unaouona wewe kama mzazi. Ndiyo kusema ratiba inayomfaa mtoto ni ile inayoandaliwa kwa ushirikiano na mtoto mwenyewe.

Mtoto anaposhirikishwa katika kutengeneza ratiba yake, ni rahisi kuiheshimu na kuifuatilia.

Unaweza kuzungumza naye, kwa mfano, kuamua muda upi anapaswa kuamka, kwenda kwenye masomo ya ziada, kwenda ibadani na muda atakaoshiriki kazi za ndani kulingana na umri wake.

Jambo la kuzingatia ni kuwa, ni vizuri muda wa kuamka na kulala usitofautiane sana na ule wa nyakati shule zikiwa zimefunguliwa. Mabadiliko makubwa yanaweza kuleta matatizo hasa shule zitakapofunguliwa.

Mshirikishe kazi za nyumbani

Ingawa ni rahisi kufikiri kumpangia mtoto kazi wakati wa likizo ni kumnyima uhuru wa kufurahia mapumzikio, ukweli ni kuwa anapofanya shughuli ndogo za nyumbani unamjenga kimwili, kiakili na kiuhusiano.

Usimruhusu mtoto awe mtu wa kungoja watu wengine wamhudumie kwa mambo madogo ambayo kimsingi angeweza kuyafanya mwenyewe. Mfanye aamini kuwa kazi si mateso bali majukumu ya lazima katika maisha.

Kwa kuwa shule zinapofunguliwa si rahisi mtoto kushiriki vizuri kazi za nyumbani, wakati wa likizo ndiyo muda mwafaka.

Mpe kazi ya kutunza bustani, kushiriki usafi na kufanya shughuli nyingine kadri zinavyojitokeza.

 

Pata muda wa kutosha na mwanao

Kama mwanao alikuwa shule ya bweni, ni wazi hamkuwa mkionana mara kwa mara.

Katika hali kama hiyo, ni rahisi mtoto kujenga uhusiano na watu wengine ambao pengine huwafahamu. Tumia wakati wa likizo kurudisha uhusiano wenu.

Fanya mkakati wa kukuza mawasiliano kati yenu. Jaribu kujua kitu gani kinamgusa na kitamfanya ajisikie kuthaminiwa.

Kifanye. Jitahidi kupata muda wa kufanya naye mazungumzo yasiyo rasmi kujenga kuaminiana.

Kwa kufanya bidii ya kujenga ukaribu nae, atakupa haki ya kujua yanayoendelea katika maisha yake. Atakuambia siri zake na pia utaweka alama muhimu atakayorudi nayo shuleni.

 

Inapobidi, mtafutie masomo ya ziada

Kusoma kwa bidii kwa miezi kadhaa kunachosha akili. Unapomtaka mtoto aliyechoka aende kupata masomo ya ziada wakati mwingine ni kuwa na matarajio makubwa kupita kiasi.

Badala ya kuendelea kusoma mtoto anahitaji kupumzisha akili kwa kushiriki shughuli nyingine kama michezo na kusoma vitabu vya kiada.

Hata hivyo, panapokuwa na sababu ya msingi, mfano pale maendeleo yake kitaaluma yanapoonyesha udhaifu, ni busara kumwekea utaratibu mzuri wa kupata msaada kutoka kwa walimu wenye sifa zinazotambulika.

 

Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754 870 815