MAONI YA MHARIRI: Msajili asimamie suluhu ya mgogoro CUF

Maalim Seif na Lipumba

Muktasari:

Pande hizo zinahusisha CUF iliyo chini ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na ile ya Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba aliyejiuzulu nafasi hiyo na kisha baadaye kurejea.

Kwa miezi kadhaa sasa, Chama cha Wananchi (CUF), kimekuwa katika mgogoro wa kiuongozi, hatua iliyosababisha chama hicho kujikuta katika pande mbili kubwa zinazokinzana.

Pande hizo zinahusisha CUF iliyo chini ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na ile ya Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba aliyejiuzulu nafasi hiyo na kisha baadaye kurejea.

Ni dhahiri kuwa tangu kuanza kwa mgogoro huo uliotokana na uamuzi wa Profesa Lipumba kubatilisha uamuzi wake wa kujiuzulu uenyekiti, wanaCUF wameshindwa kukaa kitako na kuyamaliza yale yanayokisibu chama hicho kilichowahi kuwa kikuu cha upinzani nchini.

Siku zinakwenda na kwa namna mambo yalivyo, hatuoni kuwapo kwa dalili zozote za mgogoro huu kutafutiwa dawa. Chama cha CUF kimeendelea kumong’onyoka; watu waliokuwa marafiki zamani, sasa wamegeuka kuwa mahasimu. Kifupi ni kuwa hali si shwari tena katika chama hicho.

Pengine dawa ya kumaliza mgogoro huu ingepaswa kutoka nje ya chama baada ya jitihada za ndani kuonekana kugonga mwamba, lakini swali kuu ni nani atajitokeza kuifanya kazi ya kuirudisha CUF kwenye mstari?

Nani atawakabili mahasimu wawili, Profesa Lipumba na Maalim Seif na wafuasi wao kwa minajili ya kuwasihi wakae pamoja na kumaliza sintofahamu zao kwa ajili ya mustakabali wa chama hicho maarufu nchini?

Tunaamini swali hili linaweza kupata majibu, moja likiwamo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia kati na kunusuru hali ya mambo. Tuna sababu nyingi za kupendekeza taasisi hii kuwa sehemu ya kuinusuru CUF, mojawapo ni ule ukweli kuwa Msajili ndiye mdau na mhimili mkuu wa vyama vya siasa.

Tunaamini matatizo yanayoendelea sasa CUF yanaweza kupatiwa ufumbuzi kama ofisi ya msajili itaingilia kati na kuchukua nafasi yake ya ulezi wa vyama vya siasa.

Ikijivika jukumu la usimamizi kwa sura ya ulezi na kuacha kubagua au kuonekana kuwa na upande, ofisi hii ina kila uwezo wa kuwakalisha kitako Maalim Seif na Profesa Lipumba wakazungumza na kufikia mwafaka.

Hata hivyo, kinachoonekana sasa ni kama vile mlezi huyu ameamua kujinasibisha na upande mmoja wa mgogoro, hatua ambayo tunadhani inazidi kukuza tatizo. Kwa mtazamo wetu, kitendo cha ofisi hiyo kupeleka fedha za ruzuku katika akaunti ya upande mmoja wa mgogoro kimechochea tatizo badala ya kulipatia ufumbuzi.

Tunajiuliza ofisi ilitumia busara ipi kupeleka fedha hizo katika mazingira yaliyopo ya mgogoro wa kioungozi ambayo pamoja na mambo mengine, yanahusisha pia fedha na rasilimali nyingine za chama?

Kwa hatua hii, ofisi ya msajili inawezaje kukana hisia za baadhi ya watu kuwa imeamua kusaidia upande mmoja kati ya mbili zinazokinzana?

Kwa kuwa uhai wa CUF na hata ofisi ya msajili, unategemea fedha zinazotokana na kodi za wananchi, tunaikumbusha Ofisi ya Msajili kujirudi na kuchukua nafasi yake ya mlezi wa vyama vyote vya siasa. Mgogoro unaoendelea kufukuta CUF pasipo shaka yoyote una athari katika maendeleo ya siasa za nchi yetu.