Msuva, utafika tu muda wa WEWE kujidai

Muktasari:

Bandiko hili liliambatana na maneno kuwa Msuva alikuwa kwenye harakati za majaribio na klabu moja inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania yaani La Liga.

Mchana mmoja kwenye mitandao ya kijamii zilisambaa picha zikimwonyesha Saimon Msuva akiwa eneo la hoteli ya kisasa. Msuva anaonekana amevalia suti nadhifu mithili ya kijana anayeelekea kutoa posa kwenye nyumba ya kifalme.

Bandiko hili liliambatana na maneno kuwa Msuva alikuwa kwenye harakati za majaribio na klabu moja inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania yaani La Liga.

Haikuteka akili yangu kwa kiasi kikubwa kwa sababu mawazo yangu yaliniambia pengine ilikuwa mapema kupita kiasi kwa suala lile kutokea huku nikiamini Msuva alikuwa bado na muda wa kufanya makubwa na klabu yake mpya ya Difaa El Jadidi, hivyo isingeweza kumruhusu mapema kiasi hiki kuondoka wakati akiwa ndio kwanza ameanza kuingia kwenye mfumo wao.

Bahati nzuri sikuwa mbali na taarifa zinazomuhusu hivyo nikafanya jitihada kupata ukweli wa mambo na kupitia vyanzo vinavyoaminika, kijana huyu wa Kitanzania ambaye alikacha fani ya “Mosses Iyobo wa WCB” na kuamua kutumia miguu yake kutafuta unga, alikanusha taarifa hiyo na kuweka bayana kuwa bado alikuwa na kazi ya kufanya pale Morocco. Ndio alikuwa bado na kazi ya kumfanya kocha Abderrahim Taleb kuamini katika miguu yake zaidi ya ilivyokuwa kawaida.

Ndani ya kikosi cha El Jadidi ama El Jadida kama wengine wanavyoita kutokana na eneo inapotokea, Msuva anasimama kama moja ya wachezaji muhimu kwa sasa, jambo ambalo hakuna aliyetarajia lingetokea kwa haraka kiasi hiki. Ndani ya ubongo wowote unaowaza vyema basi utagundua kuwa kuna vipaji vingi Tanzania ambavyo iwapo vikipata macho basi vitaona malisho mengi na ardhi zenye rutuba nje ya hii inayoitwa Tanzania.

Safari ya Msuva ambayo wengi hatutaki iwe na kugota, inatakiwa iwe mfano kwa wengi ambao walihisi Mbwana Samatta alikuwa na “bahati ya maisha.”

Kwenye karatasi yoyote ambayo utaandika vikosi ama majina ya wachezaji wa Tanzania, ni wazi kuwa utapata majina kama Ibrahim Ajib, Mo Ibrahim, Said Ndemla, Shaban Idd, Ramadhani Singano, Shiza Kichuya, Raphael Daudi na wengine wengi kuwa wana vipaji vya asili kuliko Msuva, lakini mwenzao huyu ana Baraka moja ambayo hawa wameshindwa kuishughulikia nayo; kujituma na kufahamu wanachotaka.

Inawezekana katika kundi hili bado wengi wana nafasi ya kufanya makubwa, lakini maisha ya Msuva ndani ya Ligi Kuu ya Vodacom na upinzani aliowahi kupata inakupa picha ni moyo wa aina ipi aliokuwa nao.

Kwenye michezo na hata maisha si kila binadamu huzaliwa na hulka ya kuwa mshindi au kuwa na roho ngumu na ndio maana si ajabu kwenye mpira wa kikapu kusikia kauli inayomsema Lebron James kuwa hakuzaliwa na roho ya kikatili ndani ya uwanja kama Michael Jordan au Kobe Bryant ambao waliweza kusaka ushindi vyovyote vile.

Lebron ilibidi ajifunze hili kwa kuishi jirani na washindi kama Dwayne Wade alipokwenda Miami Heat. Hivyo inawezakana pia Ajib asiwe na roho ya Msuva, lakini akawa na nafasi ya kujifunza. Swali pekee linabaki kuwa yupo tayari?

Moyoni mwangu na roho yangu ya Kizalendo ninaona kabisa maisha yetu kwa maana ya idadi na majaaliwa ya vipaji yapo katika sehemu na mlengo mzuri. Wachezaji wameanza kupata tamaa na msukumo wa kufika mbali na kufanya makubwa.

Huku kukiwa na taarifa za Himid Mao kutakiwa na Afrika Kusini ambako ataungana na Abdi Banda, idadi ya “maprofeshino” itapendeza zaidi pale majina ya Said Ndemla na Kichuya yakitoka kama inavyoendelea kutajwa ili kuendelea kufumbua macho ya wachezaji kama Mbaraka Yusuph ambaye ana nukuu ya kusikitisha ya kutoona umuhimu wa ligi za nje.

Nikiwa katika furaha na nikiwa na kusudio la kuonyesha umuhimu wa kuendelea “kuwafungulia njia” vijana wetu pale tunapopata nafasi, mikono yangu ilikuwa kwenye mtandao na nilikuwa natazama namna ligi ya Morocco inavyoendelea, Simon Msuva amenifanya niwe shabiki wao.

Hakuna sababu ya kuchambua umuhimu wa Mohamed Salah ndani ya Liverpool bila kutaka kufahamu ni kwanini Msuva ameanza kufanya makubwa kila akiitwa Taifa Stars.

Mpaka makala haya yanaenda kuchapishwa, kikosi anachochezea Msuva cha Difaa El Jadida kilikuwa kwenye nafasi ya tatu Ligi Kuu ya Morocco, maarufu kwa jina la Botola.

Ikiwa na pointi 14, El Jadida ilikuwa imefunga mabao 14, huku matano yakiwa yamefungwa na mchezaji wao Bilal El Megri na Msuva akiwa miongoni mwa wachezaji watatu waliofunga mabao mawili kila mmoja.

Kwa tafsiri nyingine ni kuwa Msuva ni miongoni mwa wachezaji wanaotegemewa katika kikosi cha kocha Abderrahim Talib.

Ukitazama namna ya mgawanyo wa mabao mpaka hapo maana yake ni kuwa kikosi chao kina mfumo ambao ni “free flowing” yaani mfumo huru ambao unatoa nafasi kwa wachezaji wengi kufunga mabao mengi.

Mfumo huu unarahisisha wachezaji kama Msuva wanaopenda kufunga wakitokea pembeni kupata faida na kuendelea kukomaa zaidi na hii inaweza kuwa faida kubwa kwa Msuva ambaye alipewa majukumu haya toka akiwa na kikosi cha Yanga, hii ni baraka kwake.

Si muda mrefu sasa tutakuwa tunaita kikosi cha Taifa Stars na majina mengi yakiwa ni yale yanayocheza nje ya ligi yetu. Ukomavu wa Banda unakupa sababu ya kwanini wachezaji hawatakiwi kuwa ndani, huku ufungaji wa Msuva ndani ya Taifa ni mabadiliko ya muda mfupi ambayo tunaombea yaendelee kuongezeka afike League One pale Ufaransa, ambako kutokea Morocco ni rahisi zaidi.

Naamini moyo wa Msuva ni wa kupigana. Naamini ni mshindi na ninaamini ni mwanaume wa shoka. Alikuwa na ndoto za kucheza soka la kulipwa, zimetimia. Sasa nataka arudi kitandani aweze kuanza kuota ligi kubwa zaidi kwam kuwa Ufaransa na La Liga kunafikika.

Hongera Msuva. Wenzio waanze kukutamani kila ukipiga hatua maana itasaidia Taifa kwa ujumla.