MARIAM MBEWA : Mtaalam wa kilimo cha Green house, ufugaji wa nyuki

Mariam Mbewa.

Muktasari:

Baadhi ya wadau wamelitazama suaa hili kwa mapana zaidi na kuja na suluhisho mmoja kati ya hao ni Mariam Melkizedeck Mbewa ambaye anasema sekta ya kilimo nchini itafanikiwa ikiwa tu Serikali itafanya uwekezaji.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya wakulima, lakini kutokana na changamoto mbalimbali, sekta ya kilimo nchini imeshindwa kukidhi matarajio ya wengi, licha ya kuwa na ardhi kubwa na yenye rutuba.

Baadhi ya wadau wamelitazama suaa hili kwa mapana zaidi na kuja na suluhisho mmoja kati ya hao ni Mariam Melkizedeck Mbewa ambaye anasema sekta ya kilimo nchini itafanikiwa ikiwa tu Serikali itafanya uwekezaji.

Mariam ni mmoja wa waanzilishi wa Kampuni ya Green Investment (T)ltd inayojishughulisha na utoaji elimu ya kilimo cha kisasa cha umwagiliaji ya Green House na Central Park Bees Ltd. uuzaji wa vifaa vya kisasa vya ufugaji na utoaji elimu ya ufugaji nyuki.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni mdau huyu wa kilimo alibainisha kuwa mambo mengi yanayoweza kuleta chachu ya maendeleo ya kilimo nchini ambayo ni pamoja Serikali kuondoa kodi katika vifaa vyote vya kilimo na kuwekeza katika utoaji wa elimu ya juu kwa wataalamu wa sekta hiyo.

“Jingine kubwa zaidi linaloweza kututoa hapa tulipo na kutupeleka mbele zaidi ni kuwapa fursa wataalamu wetu kwenda kupata ujuzi zaidi nje ya nchi na pia kuwalipa mishahara mizuri,” anafafanua.

Akizungumzia kuhusu wakulima , Mariamu ambaye pia kitaaluma ni mhasibu, anasema mkulima wa Kitanzania anakwamishwa na matatizo mengi, kubwa zaidi ni kipato duni.

Wengi wao hulima kilimo cha kutegemea mvua ambazo kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa zimekuwa hazitabiriki.

“Kilimo hiki ninaweza kusema kuwa ni cha kubahatisha, kwani mara nyingi mvua hii huwa haina uhakika, na pia haijulikani itanyesha kwa kiwango gani. Suala jingine ni katika mbegu na huduma za ugani,’’ anasema.

Lakini hata anapolima na kupata mazao yale machache yasiyo na ubora wa kutosha, suala la soko pia ni changamoto. Kutokana na hali ya mazao hayo wakulima hulazimika kuyauza nchini kwa bei ya chini.

Katika mapendekezo yake ya uboreshaji wa kilimo nchini, anawashauri wakulima kubadilisha mitazamo yao na kuhama kutoka kwenye kilimo cha asili na kwenda kwenye kilimo cha kisasa, kwa kuwa kinaelekeza matumizi ya eneo dogo la ardhi kwa kuzalisha kiasi kikubwa cha mazao yenye ubora.

Nchi yetu ina vyanzo vingi vya maji kama vile mito na mabwawa yanayozungukwa na ardhi yenye rutuba. Wakulima wanaweza kujikusanya katika vikundi na kutafuta wataalamu watakaowawezesha kulima kilimo cha kisasa.

“Kwa kujikusanya pamoja kutawapa urahisi katika kufikiwa na wataalam, lakini pia kushauriana na hatimaye kuongeza ufanisi katika kilimo chao. Ikiwa hili litasimamiwa ni wazi kuwa tutaweza kutoka kwenye hatua hii na kusogea kwenda mbele zaidi,” anafafanua.

Jambo la pili Serikali na sekta binafsi zitoe ruzuku na mikopo ya wakulima walio na nia ya kuingia katika kilimo cha kisasa.

Lakini pia watu waliosomea Kilimo wajitahidi kutoa elimu kwa wakulima na watu wajikite kutafuta elimu ya Kilimo ili waje kutoa msaada kwa wakulima.

Na wakulima nao wasisite kushiriki makongamano na pia usomaji wa vitabu vinavyohusiana na shughuli wanazosifanya.

Akizungumza kuhusu ufanisi katika kazi, anasema kupitia mpango aliouanzisha wameweza kufikia wakulima wa mikoa mbalimbali nchini ikiwamo Mbeya, Mwanza, Dodoma, Tabora, Lindi, Mtwara, Dar es Salaam na visiwani Zanzibar.

“Mpango tulio nao ni kuwafikia wakulima wengi zaidi nchini na kuhakikisha elimu ya kilimo na ufugaji nyuki wa kisasa vinaenea kote nchini,” anasema na kuongeza kuwa:

“Pia nina mpango wa kuanzisha kiwanda cha kutengeneza mizinga ya nyuki ya kisasa hapa nchini. Kwani kwa sasa tunaagiza kutoka China kwa gharama za juu. Pia nitahakikisha kunakuwa na wataalam wa kutosha watakaojikita na fani hiyo,”

Kwa upande wa kilimo, anasema ana mpango wa kuanzisha kiwanda cha kutengeneza vifaa vya umwagiliaji ili wakulima waweze kupata vifaa hivyo kwa urahisi na kwa bei rahisi.

Historia yake

Mariam alizaliwa mkoani Mbeya miaka 31 iliyopita. Alimaliza kidato cha nne mwaka 2003, kwa bahati mbaya matokeo yao yalifutwa. Kutokana na kuwa na hali ngumu ya maisha aliona suluhisho pekee ni kuingia jijini Dar es Salaam kutafuta maisha.

Aliingia Dar es Salaam na moja kwa moja akaanza kujishugulisha na biashara ndogo ndogo ili kupata pesa na kurudia mtihani wa kidato cha nne.

“Nilirudia mtihani huo na kufaulu na kuniwezesha kujiunga na kidato cha tano na cha sita kabla ya kujiunga na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM),” anafafanua.

Kwa sasa ana shahada ya usasibu aliyohitimu kutoka chuoni hapo.

Baada ya kumaliza masomo yake alifanikiwa kuajiriwa katika kampuni ya Consnet akifanya kazi kama mhasibu.

Kutokana na kiu ya kujiajiri aliyokuwa nayo baada ya kupata uzoefu wa kazi aliona ni bora akatoka na kuanzisha kampuni yake.