Mtoto Asha mwanafunzi kiboko ya wanaume wakware

Muktasari:

 

 

 Huyu ni miongoni mwa wanafunzi wa kike wilayani Bahi wanaopanga mitaani, huku wakikabiliwa na vishawishi vya kila aina.

Tofauti na vyumba vya baadhi ya wanafunzi wenzake visivyo na milango, Chumba cha Asha Abdallah kina mlango wa bati unaofungwa kwa kutumia mnyororo wa baiskeli.

Huyu ni miongoni mwa wanafunzi wa kike wilayani Bahi wanaopanga mitaani, huku wakikabiliwa na vishawishi vya kila aina.

Kwa Aisha anayesoma katika Shule ya Sekondari Magaga, jitihada alizofanya za kuwa na mlango huu ni sehemu ya kujilinda siyo tu dhidi ya wezi, lakini pia wanaume wakware.

Katika wilaya hii, hasa mitaa wanayoishi Asha na wenzake, baadhi ya wanaume wana tabia ya kuwavizia wanafunzi wa kike kwa lengo la kuwarubuni ili waingie kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwishowe kuwa chanzo cha kukatisha masomo.

Kiboko cha wanaume

Hakuna anayemgusa Asha japo anaonekana kuwa na mwili mdogo. Wengi wanamchukulia kuwa ni msichana mkorofi.

Ukibahatika kukutana naye utakubaliana nami kwamba kwa umri wake wa miaka 14 na mambo anayoyafanya kijijini na shuleni ni vitu viwili tofauti.

Hana woga na ana ujasiri wa kipekee. Msichana huyo amepanga chumba katika kijiji cha Magaga ilipo shule yao.

Japo wapo wanaoshindwa kuendelea na masomo yao kwenye mazingira hayo hayo ambayo Asha anaishi, yeye anaamini kwamba siku moja atatimiza ndoto yake ya kuwa mwalimu wa sekondari.

“Dada zangu walio kidato cha nne wamenisimulia walivyoweza, kwa hiyo naamini siku moja nami nitaweza kutimiza ndoto yangu, Mungu ni mwema,”anasema na kuongeza;

“Nina ndoto za kuwa mwalimu, natamani niifikie kwa namna yoyote ile ndiyo maana namuomba Mungu nifanikishe na nitajitahidi, naamini nitaitimiza.’’

Asha anasema japo ni ukweli kwamba anaishi kwenye mazingira yanayotishia kushindwa kutimiza ndoto yake, hatakata tamaa.

Mwanafunzi huyo amepanga kwenye chumba kilicho umbali wa kama kilometa mbili hivi kutoka shuleni.

Si peke yake aliyepanga, wanafunzi wengi wanaotokea vijiji vilivyo mbali na shule hiyo wamepanga mitaani ili wapate nafasi ya kusoma jambo linalohatarisha usalama wao.

Amefanikiwa kujitengenezea sifa ya ziada shuleni hapo. Hujilinda yeye na wasichana wenzake kwa kuwa anaamini, wanaosababisha kukwama kwa ndoto za wasichana wengi ni wanaume.

“Binafsi siku hizi wavulana hawanifuatilii hata kidogo wananiogopa kwa sababu wanajua wakifanya hivyo nitawachukulia hatua kali,” anasema kwa msisitizo.

Hatua anazozisema ni zilezile za kuwashtaki kwenye uongozi wa kijiji au kwa mkuu wa shule, wanaume wenye tabia ya kuwatongoza wanafunzi hasa wanaoishi kwenye magheto kijijini.

“Imeshafikia hatua kwamba nikipita sehemu ambayo mvulana amesimama na msichana, wakiniona tu wanaagana. Mimi napenda hali hiyo kwa sababu natamani wote tumalize shule,” anasema na kuongeza:

“Kuna mvulana alikuwa anamsumbua sana rafiki yangu, nikaona mwisho anaweza kumkubali na kumpa mimba bure. Nikaenda kumwambia mwalimu, alimuita na kumuadhibu najua hatarudia tena.’’

Kiuhalisia wanafunzi wenzake wa kiume na hata wanaume wengine kijijini hawamgusi.

“Kusemelewa na kale katoto ni aibu, bora usikaguse kabisa,”anasema mmoja wa vijana kijijini hapo, Erick Matonya.

Mwalimu Mkuu msaidizi wa Shule ya Sekondari Magaga, Daudi Gingi anakiri kuwa binti huyo ni mkali na anatamani, wasichana waige mfano wake.

“Huyu binti ni mkali sana, hachezewi ovyo, laiti kama wasichana wote wangekuwa kama huyu kesi za mimba tusingepata kabisa,”anasema.

Ujasiri wake wa kupambana na wanaume wakware, umemfanya aonekane jasiri.

Maisha ya Asha

Msichana huyo anaishi kwenye mazingira magumu kama wanavyoishi wasichana wengine waliopanga mtaani.

Japo nyumba anayoishi ni ya bati na tofari. Vyumba vyake havina mlango.

“Zamani kulikuwa hakuna mlango lakini tukawa tunaibiwa chakula na vitu vingine. Nikaogopa kwamba hao wanaoingia kuiba hasa tukiwa shule wanaweza kuja wakati nimelala,” anasema.

Ilibidi ahamishie chakula na vitu muhimu kwenye chumba cha rafiki yake ili kiwe salama. Hata hivyo, anasema lilimjia wazo la kutengeneza mlango.

“Mwanzoni nilimuomba mama mwenye nyumba anitengenezee mlango, lakini akasema hana fedha. Japo kwa mwezi nalipa kodi Sh5,000, lakini chumba chenyewe naishi kwa roho ngumu tu,” anasema.

Chumba chake kwa sasa kina mlango wa bati. Japo sio salama, lakini walau anaweza kuufunga kwa mnyororo akiwa ndani.

Hata hivyo, anasema kuna wakati huja baadhi ya vijana wa kijiji na kuwaibia chakula chao wawapo shuleni.

“Imebidi chakula nikiweke kwa jirani zangu, naogopa kuibiwa. Huku kuna nguo tu,” anasema.

Hakuna jiko kwa ajili ya kupikia. “Ilibidi tutafute mabati mengine yaliyochakaa, tukajenga jiko ambalo halitusaidii sana,” anasema.

Anasema matumizi ya kuni pia yamekuwa sababu ya kuwapotezea muda. Kuna wakati huwa analazimika kwenda kutafuta kuni porini kwa ajili ya kupikia.

“Siku ikitokea kuni chache na kuna upepo, chakula huwa hakiivi, inabidi tule kibichi. Haya ndiyo mazingira yangu,”anasema.

Pamoja na hayo yote, anaamini siku moja atamaliza masomo yake na kufikia ndoto yake ya kuwa mwalimu.

Kuna wakati hulala na rafiki yake, Maria Patrick ambaye anasema anafurahia kulindwa.

“Ni mdogo wangu lakini kwa kweli anaogopwa, hapendi ujinga huyu. Watu wote wanamuelewa hivyo,” anasema.

Mwenyekiti msaidizi wa Kijiji cha Magaga, Laurent John anasema sifa za binti huyo anazo.

“Ubebaji wa mimba ni mkubwa na hatari zaidi ni kwa wasichana wasio na msimamo. Asha anajitambua ndiyo maana akisumbuliwa huwa anakuja kusema,” anaeleza.

Maendeleo ya taaluma

Mwalimu Gingi anasema Asha ni kati ya wanafunzi wanaofanya vizuri darasani.

“Ni msikivu na mwelewa sana, naamini wasichana wote wangekuwa hivi, wangefikia ndoto zao kimaisha licha ya changamoto za hapa na pale,” anasema.

Wenzake wanamzungumziaje?

Asha Abdallah akiwa na wanafunzi wenzake wa shule ya sekondari.Picha na Tumaini Msowoya

Pengine tabia yake ya kuwashtaki wanaume wakware wanaowasumbua wanafunzi wa kike, ingemfanya achukiwe hasa na rafiki zake wa kike.

Lakini haiko hivyo, Asha anapendwa na wenzake kiasi kwamba hata mwandishi wa makala haya alipofika katika chumba chake, alikutana na wanafunzi wengi waliokuwa wamekwenda kumtembelea.

Mama mwenye nyumba anakoishi, Ediana Nuru anakiri kuwa binti huyo anajitunza na mara nyingi amekuwa akizungumza naye kuhusu maisha.