MAONI YA MHARIRI: Mtoto kushiriki uhalifu ni kasoro ya wazazi kukosa umakini

Muktasari:

Panya Road hao wanadaiwa kuhusika na uporaji siku ya tamasha la Singeli lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Mbagala Zakhem Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, ambapo tangu uporaji huo ufanyike hasira za wananchi zimekuwa juu kwa kujichukulia sheria mkononi.

Gazeti hili toleo la jana kwenye ukurasa wa kwanza kulikuwa na habari kubwa iliyosema Mwanafunzi apigwa Dar ‘afa, afufuka’ mochwari. Habari hiyo ilizungumzia kuibuka kwa kikundi cha uhalifu kilichojipachika jina la Panya Road, lakini wahusika wake wengi ni watoto wa chini ya umri wa miaka 18 na wengine ni wanafunzi wa sekondari.

Panya Road hao wanadaiwa kuhusika na uporaji siku ya tamasha la Singeli lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Mbagala Zakhem Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, ambapo tangu uporaji huo ufanyike hasira za wananchi zimekuwa juu kwa kujichukulia sheria mkononi.

Mbali na Panya Road kuna makundi mengine yanayohusisha watoto yaliyojipachika majina ya Mbwa Mwitu na Watoto wa Mbwa, haya makundi yana mtindo mmoja wa uporaji kwa makundi kwa kufanya operesheni maalumu katika baadhi ya maeneo.

Kinachotisha zaidi makundi haya yanahusisha watoto ambao bado wako chini ya uangalizi wa wazazi au walezi wao, kwa maana nyingine uhalifu huu unafanywa na wanafunzi wa sekondari ambao bado wanalelewa na wazazi wao.

Tunakubaliana na kauli ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Gilles Muroto kwamba kuibuka kwa uhalifu unaohusisha makundi ya watoto kuna haja ya kuanza kuwafungulia mashtaka wazazi na walezi kwa kutumia Sheria ya Watoto ya mwaka 2009.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, wazazi na walezi wana wajibu wa kuhakikisha watoto wao wanakuwa chini ya uangalizi wao. Kifungu cha 14 cha sheria hiyo kinasema mzazi atakayeshindwa kutekeleza hayo atafikishwa mahakamani na akitiwa hatiani atapewa adhabu ya kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh5 milioni.

Wahenga walisema samaki mkunje angali mbichi kwa maana akikauka hawezi kukunjika, usemi huu unafundisha kuwa watoto waonyeshwe malezi na njia nzuri wakiwa bado wadogo kwa kuanzia na upendo na kuthaminiwa.

Pia, nyumba yenye msingi imara husimama imara bila kuteteleshwa na chochote kile, vivyo hivyo kwa mtoto, kabla hajafikia umri wa kwenda shule na kujichanganya na makundi ya watoto wengine anatakiwa awe tayari amepata msingi bora na imara kutoka kwa wazazi wake.

Wazazi wote tunafahamu msingi bora na imara kwa mtoto humsaidia asitikisike ama kujifunza mambo mengine yasiyofaa kutoka kwa makundi anayokutana nayo ambayo yanaweza kumhatarishia ustawi wa maisha yake ya baadaye.

Tunaamini kufanikisha ustawi huo katika maisha yao, hawahitaji kuona mpasuko kwa wazazi ama familia zao, kwani sababu hizo nazo huchangia kuweka doa katika makuzi yao bora.

Kwa mantiki hiyo, wazazi na walezi wasio makini wanaweza kuwa ni adui namba moja wa kumharibu mtoto kwa kushindwa kukua vyema hata kuwafanya wazoee ukatili au uhalifu.

Takwimu za watoto wanaowekwa rumande kwa tuhuma za uhalifu ni kubwa na kinachotakiwa hapa ni ushirikiano kati ya wazazi, walezi na jamii kuwafunza watoto wao kwa sababu baadhi yao wamekuwa wakifanya makosa pasipo kujitambua.

Ni vigumu kumtetea mtoto anayehusishwa na uhalifu unaofanyika mchana ukihusisha vikundi vya uporaji. Pia, ni vigumu kumtetea mzazi au mlezi anayetoka hadharani akidai hajui kama mwanaye anahusika na uhalifu.

Kuondokana na hayo ni vema wazazi na walezi wanaoshindwa kulewa watoto wao wakachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.