Muandae mtoto kufanikiwa kwa kukuza vipaji vyake

Muktasari:

  • Katika makala ya awali, nilitumia mfano wangu mwenyewe kujaribu kueleza namna wazazi wanavyoweza kukuza vipaji vya watoto.

Wazazi wenye ukaribu na watoto wao wana nafasi nzuri ya kupandikiza vitu vitakavyochipua kadri mtoto anavyoendelea kukua.

Katika makala ya awali, nilitumia mfano wangu mwenyewe kujaribu kueleza namna wazazi wanavyoweza kukuza vipaji vya watoto.

Wakati ninakua, nilijengewa mazingira ya kujieleza kwa maandishi kupitia kuandikiwa barua na kusoma vitabu. Mazingira hayo ya kimalezi yalipandikiza tabia ya kupenda kuandika.

Nikiwa shule nilikutana na mazingira yaliyonishinikiza kupenda sayansi. Walimu na wanafunzi wenzangu waliizungumzia sayansi kama fani ya pekee inayosomwa na watu wenye uwezo mkubwa.

Kwa kuwa nilikuwa na ufaulu mzuri, na kwa kuwa nilipenda ‘kuwa na soko kwenye ajira’, nilifuata mkumbo wa kusoma sayansi mpaka ngazi ya shahada ya kwanza.

Nilipuuza kipaji kizuri cha uchoraji nilichokuwa nacho. Nilifikiri mafanikio yangu yalitegemea ufaulu wa masomo yanayoheshimika katika jamii.

Hata hivyo, ninapotazama nyuma hivi sasa, ninaona namna maamuzi hayo yalivyokuwa yamesongwa na mchanganyiko wa kutojitambua na shinikizo la marafiki rika.

Ingawa nilifanya vizuri kwenye masomo hayo, bado sikuwa na mapenzi na kile nilichokisoma.

Kulikuwa na mstari wa dhahiri kati ya yale niliyokuwa nikijifunza darasani na kile nilichokuwa najisikia ndani yangu.

Kuhusianisha vipaji na kazi

Hata baada ya kuanza kufanya kazi, sikuona namna gani kazi ile iliniwezesha kutumia vipaji nilivyokuwa navyo.

Milango ya kuendelea na masomo ilipofunguka, niliamua kuheshimu sauti niliyokuwa nikiisikia ndani yangu. Sikufanya kosa la kuruhusu matarajio ya jamii na soko la ajira viniamulie mwelekeo.

Nilichagua kusoma kile nilichoamini tayari kilikuwa kinaota ndani yangu. Haukuwa uamuzi rahisi.

Hata hivyo, kwa mara ya kwanza nilionja ladha ya kufurahia kusoma kitu kinachoakisi matarajio yangu.

Nilipokwenda maktaba kupekua vitabu, kwangu ilikuwa namna fulani ya kuburudika. Hayakuwa mateso kama ilivyokuwa wakati nikisoma mambo yasiyooana na wito wangu. Alama za juu zilikuja kama matokeo ya kujifunza mambo niliyoamini ninahitaji kuyafahamu.

Uzoefu wangu kazini ulianza kuwa tofauti. Nilipenda kile ninachokifanya. Sikuhisi kulazimika kufanya kazi.

Hiki, naamini ndicho kipimo cha wito wa mtu.

Unapofanya kazi inayotumia vipaji vyako, unakuwa tayari kufanya kitu si kwa sababu ya malipo bali kupata utoshelevu wa kufanya kitu unachoamini ni sahihi.

Kadri unavyokifanya ndivyo ufanisi wake unavyoonekana na inakuwa rahisi kupata mafanikio zaidi. Hii ndiyo faida ya kufanya kitu kinachooana na wito wako.

Nafasi ya kipaji kazini

Kila mtu amezaliwa na kipaji, ingawa wapo watu wengi hawavifahamu vipaji walivyonavyo. Kipaji ni ule uwezo anaokuwa nao mtu wa kufanya kitu ambacho si watu wengi wanaweza kukifanya.

Kuna watu ni watangazaji hata kama hawajawahi kusomea utangazaji. Ndani yao kuna uwezo ambao sisi wengine hatuna.

Kuna watu wana vipawa vya biashara hata kama hawajawahi kwenda darasani kusomea ujasiriamali wala usimamizi wa biashara.

Hawa ukiwapa fedha kidogo, wanajua namna ya kuzizalisha. Wengine, wana vipaji vya ufundi.

Hawajasoma sana, lakini wanaweza kutengeneza vitu ambavyo sisi wengine hata tungefundishwa, tusingeweza.

Kipaji cha mtu kikikuzwa kina nafasi kubwa wa kuamua kiwango cha mafanikio yake. Fikiria wachezaji wa kandanda, wanamuziki, waandishi mashuhuri waliofikia kilele cha mafanikio kwenye fani zao.

Watu hawa hawakwenda shule kusomea vipaji vyao. Walielekeza bidii kwenye maeneo waliyoamini wanayaweza zaidi.

Watu hawa wanapata mafanikio kwa sababu kwanza, wanapenda kile wanachokifanya. Mbwana Samatta anapoingia uwanjani, anafurahia kazi yake.

Tofauti na watu wanaofanya kazi wasizozipenda, Samatta analipwa fedha nyingi kwa kufanya kitu anachokipenda.

Lakini, mbali na kupenda kile anachokifanya, mtu anayetumia kipaji chake anakuwa mbunifu. Fikiria mtu kama Lucas Mhavile, maarufu kama Joti.

Watu wanamlipa fedha nyingi ili afanye kile anachokipenda. Wanaweza kuwapo watu wengi wenye shahada za sanaa ya maonyesho na maigizo lakini wasiweze kuwa wabunifu kama Joti. Kipaji kinakufanya uwe mbunifu kwenye kazi yako.

Tunawafahamu watu wengi wenye kiwango kikubwa cha elimu lakini hawapati mafanikio na wala hawajisikii utoshelevu ndani yao. Sababu zinaweza kuwa nyingi.

Moja wapo, inawezekana watu hawa walitumia muda mwingi kusomea maeneo yasiyokuza vipaji vyao.

Huwezi kuonyesha tofauti kwa kufanya kitu kisichoanzia ndani yako. Hili ni somo kwa wazazi. Tunao wajibu mkubwa wa kukuza vipaji vya watoto wetu.

Kuchochea kipaji cha mtoto

Kwa bahati mbaya, mfumo wetu wa elimu hausaidii kuibua na kukuza vipaji vya wanafunzi. Imejengeka dhana kwamba ufaulu ndiyo unaoamua mafanikio ya mtoto.

Matokeo yake, shughuli zote zinazofanyika shuleni, zinalenga kumwezesha mwanafunzi afaulu mitihani.

Ufaulu huu hata hivyo, haumhakikishii mwanafunzi mafanikio baada ya kuondoka darasani. Kama wazazi, tuna wajibu mkubwa wa kuwasaidia watoto kuwianisha vipaji walivyonavyo na masomo.

Namna moja ya kuibua vipaji vya mtoto, ni kumtengenezea mazingira sisimuzi tangu mapema.

Tangu akiwa mdogo mpe mtoto fursa ya kuonyesha uwezo wake bila kumwingilia. Mwache mtoto awe yeye bila kujaribu kumfanya awe toleo jipya la wewe mzazi.

Nafahamu baadhi ya wazazi wakati mwingine tunapenda watoto wafanye kile tunachokifanya sisi.

Upo uwezekano wa mazingira ya malezi kuumba kipaji fulani. Mfano, mtoto aliyezaliwa na mwanamuziki, si ajabu na yeye akawa mwanamuziki baadaye.

Kile anachokiona mtoto na akakipenda, kina nafasi kubwa ya kuwa mbegu ya kitu atakachokifanya akiwa mkubwa.

Ikiwa ungependa mtoto wako aige kazi yako, basi kuwa karibu naye. Urafiki wa karibu na mtoto utamfanya ajitambulishe na kile unachokifanya.

Nilijitolea mfano wangu mwenyewe. Ukaribu wangu na baba yangu ulinifanya nikavutiwa kupenda maandishi.

Lakini pia, pengine hupendi mtoto afuate nyazo zako. Ikiwa hivyo, mtambulishe kwa watu waliobobea kwenye fani unazotaka mtoto azipende.

Msimulie hadithi, msomee vitabu, mwonyeshe filamu za watu walioonyesha mafanikio kwenye maeneo yao. Pia, unaweza kumpeleka kwenye maeneo yatakayomkutanisha na watu wanaofanya kazi tofauti.

Kupitia yote hayo, mtoto ataanza kujitambulisha na eneo fulani. Michezo yake, mazungumzo yake na shughuli anazozifanya katika muda wake wa ziada vinaweza kuanza kuonyesha mwelekeo fulani. Huo unaweza kuwa mwanzo wa wito wa mtoto.

Blogu: http://bwaya.blogspot.com