Muonekano wako ni msingi wa maendeleo yako kiuchumi

Muktasari:

  • Kuna utafiti uliodhihirisha kuwa umaridadi huhusishwa na uaminifu, uungwana na utu. Watu wengi wamewahi kudanganyika na wakathamini watu wasio na mbele wala nyuma, kutokana na namna walivyovaa kama mamilionea.

Namna mtu anavyoonekana kuanzia mavazi, mtindo wa nywele, mapambo au vitu vingine vilivyomo mwilini mwake hutoa ujumbe usio wa maneno. Kwa hakika muonekano huo huweza kuwa na mawasiliano yenye nguvu sana.

Kuna utafiti uliodhihirisha kuwa umaridadi huhusishwa na uaminifu, uungwana na utu. Watu wengi wamewahi kudanganyika na wakathamini watu wasio na mbele wala nyuma, kutokana na namna walivyovaa kama mamilionea.

Kuna usemi maarufu kuwa mavazi ndiyo yanayomfanya mtu kuwa mtu. Licha ya umaridadi, kumfanya mtu apate hadhi mbele za wenzake, vitu vingine kama muonekano wa nywele huweza kufanya akawekwa katika kundi fulani. Leo hii kuna nchi ambazo zina imani tofauti na muonekano wa nywele ndefu na ndevu nyingi. huhusisha muonekano huo na ugaidi.

Kuna muonekano unaokubalika katika jamii. Kwa mfano, katika mataifa mengi imekubalika kuwa mwanamke huvaa pete kuashiria kuchumbiwa au kuolewa. Imekubalika ingawa baadhi ya mataifa hutofautiana kuhusu sehemu ya kuvaa pete hiyo. Nchini Marekani, pete hiyo huvaliwa mkono wa kushoto wakati Ulaya huvaliwa mkono wa kulia.

Siri ya maumbile

Wachambuzi wa masuala ya saikolojia ya mwonekano wanatambua kuwa, maumbile hutoa aina fulani ya ishara muhimu za mawasiliano. Hilo limethibitishwa na wataalamu mbalimbali duniani.

Kutokana na utafiti mbalimbali uliowahi kufanywa, zipo aina tatu ya mwonekano ambao mtu anaweza kuwa katika upande mmoja au mwingine, au kwa pamoja kutokana na maumbile yake.

Goigoi

Goigoi ni mtu ambaye ni vigumu kuelezea fikra, imani na hisia zake kwa uwazi hivyo kutokuwa na faida kwenye mengi anayoyafanya au kushiriki. Huwa na mtazamo wa kushindwa, sauti nyembamba na malalamiko yasiyokwisha.

Inaelezwa kwamba anapenda kutumia viunganishi vya “uh” na “um.” Hushindwa kutumia macho kwa mawasiliano, badala yake anapenda kutazama chini au pembeni.

Hupendelea kukwaruza koo wakati wa kuzungumza. Hupenda kuomba msamaha bila utaratibu na mara kwa mara. Huziba mdomo au macho na hupenda zaidi kukunja mikono wakati wa mazungumzo.

Wapo watu wengi wenye sifa hizi ambazo wataalamu wanashauri kuziepuka, ili kujitegemea kiuchumi. Ni muhimu kuelewa kuwa u oigoi kwa asilimia kubwa ni adui wa kukabiliana na umaskini, hivyo ni muhimu kukutana na wataalamu wa saikolojia kukusaidia kuvua gamba lake.

Jeuri au katili

Ni mtu mwenye fikra, imani na hisia zenye kulazimisha wengine kwa manufaa yake. Hii ni pamoja na kuwa na mitazamo hasi na tabia za kikomandoo, kuwa na sauti kali na kavu.

Mara nyingi hutoa maneno ya lawama, shutuma, matusi na huwa na uso mkakamavu. Hupendelea kukunja mikono kwa ukakamavu. Wataalamu wa saikolijia wanasisitiza kuwa, si vizuri kuwa na asilimia kubwa ya hizi sifa kwani ni hatari kwa afya, kisaikolojia hata kiuchumi.

Tabia hizi ni kinyume cha zile za goigoi, ambaye mara zote huwa ni mtu wa ndiyo wakati jeuri ni mtu wa hapana.

Hodari au jasiri

Watu wenye sifa hizi huwa na asilimia 50 za goigoi na asilimia 50 za mtu jeuri. Hisia, imani na fikra zao hutolewa kwa kujiamini na kwa uwazi kwa faida ya wote; mtoaji na mpokeaji.

Wana tabia ya kijasiriamali, ustaarabu na ushindi. Watu mbalimbali waliofanikiwa katika maisha wamejendwa katika mwonekano wa kijasiri. Watu hawa ni wale wenye mtazamo chanya, unyoofu na sauti ya utulivu.

Ni watu makini na wenye uwazi, wasikilizaji pia. Hutumia mikono wakati wa kuongea na hutabasamu kwa wakati mwafaka hasa mara ya kwanza kuonana na mtu mpya. Pia, hupenda kuwa wasikivu na tayari kujifunza.

Kutokana na sifa hizi unaweza kujitathmini unaangukia kwenye kundi lipi kati ya goigoi, jeuri na katili au hodari na jasiri. Ukisahafahamu ukweli wako, ni rahisi kufanya marekebisho muhimu yatakayokuimarisha zaidi.

Mwadamu hakuumbwa kuwa goigoi au katili, hayo yanajengwa kutokana na aina ya maisha tunayoyapita. Kwa mfano, waliokulia kwenye umaskini na ufukara ni rahisi kwao kuwa goigoi wakati mila potofu huzalisha watu goigoi na katili.

Tunaweza kubadilika kulingana na muda na wakati kadri tupendevyo. Njia za kubadilika toka kwenye ugoigoi, ujeuri na kuwa hodari zipo na kila anayependa kufanya hivyo hufanikiwa.

Pata msukumo wa kujifunza, kutenda na kusimamia maisha. kuwa msikivu, makini na muwazi kila inapohitajika ili kuongeza ushawishi wa masuala unayohusika nayo. Kujifunza mambo mapya ni kitu muhimu na inashauriwa kufanya hivyo kila inapohitajika.