AJIRA NA KAZI: Muongozo wa maisha ya kazi kwa mfanyakazi mgeni

Muktasari:

Changamoto ni kuwa utakutana na mazingira ambayo hujawahi kukutana nayo. Utajikuta unatakiwa kuanza kuelewana kikazi na watu ambao hukuwa ukijuana nao hapo kabla.

Unapokuwa mfanyakazi mpya kazini kuna vitu viwili utakutana navyo. Kwanza ni changamoto ya kimazingira, pili ni uzuri wa mazingira.

Changamoto ni kuwa utakutana na mazingira ambayo hujawahi kukutana nayo. Utajikuta unatakiwa kuanza kuelewana kikazi na watu ambao hukuwa ukijuana nao hapo kabla.

Uzuri wake ni kuwa utakutana na mazingira mapya utakayotakiwa kuyazoea, pamoja na watu wapya ambao utajenga nao urafiki mpya wa kikazi.

Watu wapya na mazingira mapya kwa kawaida huwa na mambo yake mazuri kuliko uliyozoea, vilevile kutakuwapo changamoto mpya ambazo hukuwahi kuzikabili.

Faida kubwa unapoanza kazi ni kuwa viongozi wako wanakuwa na imani kubwa nawe kuwa utatenda kazi bora kwa jinsi ambavyo uliweza kufaulu vizuri usaili wako.

Unapoingia kazini ni rahisi kupendwa. Mkuu wako wa idara hawezi kuzungumza na wewe kwa ukali, lugha itakayotumika ni ya majadiliano zaidi kuliko amri. Unachotakiwa ni kuichukua tabia hiyo ili iendelee kila siku.

Kutoka lugha ya majadiliano mpaka kuanza kufokeana kazini hapo ujue tayari kuna vitu ambavyo vimeshakaribishwa. Ni wewe kama mfanyakazi unakuwa umetengeneza mazingira ya kufokewa kutokana na utendaji wako mbaya au nidhamu mbovu.

Shika muongozo ufuatao ili ukusaidie kujenga mazingira bora ya kazi kuanzia ukiwa mpya kazini mpaka utakapotajwa kuwa mfanyakazi mzoefu miongoni mwa wazoefu

Nidhamu binafsi na kazi

Kila siku unatakiwa ujiheshimu na uiheshimu kazi yako. Kipindi ambacho viongozi wako wanakulea kutokana na upya wako kazini, wewe thibitisha kwa vitendo nidhamu yako binafsi na ya kazi.

Wafanye viongozi wako wabadili nyakati za kukupenda kwa upya wako mpaka kuvutiwa na wewe kwa utendaji na nidhamu yako binafsi.

Utashangaa maisha yako kazini yanakuwa mepesi kila siku. Unaweza kustaajabu bosi ambaye kila mtu anamwogopa kwa ukali na usumbufu mwingine, akija kwako mnazungumza kwa upendo na kuheshimiana.

Hivyo, jiheshimu, heshimu viongozi pamoja na wafanyakazi wenzako. Hakikisha uvaaji wako ni mzuri wenye kuendana na mazingira ya kazi yako, kisha uchape kazi kuzidi kiwango ambacho watu wangekitarajia kutoka kwako.

Unapaswa kuwa mtu mwenye malengo. Jiwekee malengo ya kazi na uyafikie. Njia hiyo itakufanya uonekane mtu bora zaidi kazini na utamvutia mwajiri kila siku.

Kuwa sehemu ya wafanyakazi

Ukiingia kazini, usitake kujionyesha kuwa wewe ni jeshi la mtu mmoja. Ni kweli unatakiwa uzingatie zaidi kile ambacho kimekufanya uajiriwe, lakini hapo kazini kuna wafanyakazi wenzako ambao kwa namna moja au nyingine utahitaji ushirikiano wao.

Unaweza kujiona unajitosheleza kikazi, kwa hiyo ukaona huhitaji kuuliza wala kumshirikisha yeyote kile unachofanya, lakini wewe ni binadamu. Unaweza kuumwa ghafla kazini na wafanyakazi wenzako ndiyo watakaotakiwa kukupa msaada.

Hivyo, ukiingia kazini jambo la kwanza hakikisha unafahamiana na wafanyakazi wenzako. Hakikisha unajuana nao majina, na umwite unayemhitaji kwa jina lake. Ni kosa kumaliza wiki nzima kazini ukiwa hujachukua hatua yoyote kujua majina ya wafanyakazi wenzako.

Ukiwa mgeni kazini, hakikisha kila siku katika siku zako za mwanzo, uwe unatumia angalau dakika 20 kuzungumza na wafanyakazi wenzako japo wawili, mbadilishane uzoefu kuhusu kazi. Upate kile ambacho wamekuwa wakifanya kila siku, nawe utoe ulichonacho.

Mazungumzo na wafanyakazi wenzako, yatakusaidia kujua mwajiri wako anapenda nini na mambo gani hapendi. Utakachokipata kitakusaidia kujitengenezea njia za kuishi ukiwa kazini.

Hakikisha mahudhurio mazuri

Siku za mwanzo ingia kazini mapema na ujitahidi kutoka kazini ukiwa umechelewa. Baada ya hapo, hakikisha hiyo ndiyo inakuwa tabia yako siku zote.

Ukiwa mpya kazini epuka visingizio na maombi ya ruhusa ya hapa na pale. Onyesha kuwa umeanza kazi rasmi na upo tayari kiakili na kimwili. Ukianza kutia doa mapema, utamfanya mwajiri wako akuone una upungufu.

Weka vizuri rekodi yako ya mahudhurio. Kumbukumbu za kiofisi zikitazamwa wewe uonekane hukosi kazini na muda wako wa kuingia ni mapema kisha huchelewa kutoka.

Una wagonjwa? Watembelee katika muda ambao unakuwa umeshatoka kazini. Safari nyingine fanya siku zako za mapumziko. Fanya hivyo ili kutetea rekodi zako za kiofisi hasa kwenye eneo la mahudhurio.

Usishiriki majungu, siasa

Kila ofisi majungu na mazungumzo ya siasa yapo, ni kutokana na kukutanisha watu wa aina tofauti. Unachotakiwa kutambua ni kuwa umeingia kazini kufanya kazi na siyo kupiga soga, kusengenya watu na kuendekeza ubishi wa kisiasa.

Onyesha tofauti kwa kujiweka mbali na vitendo hivyo. Hakuna mwajiri ambaye anaweza kuwapenda watu ambao muda wa kazi wanakuwa wanabishania siasa. Ukijiunga nao, unamfanya mwajiri akuchukie ukiwa bado mgeni kazini.

Kama una damu ya siasa na unapenda kuzijadili, siyo vibaya kama utazipangia muda wake, nyakati za mapumziko ya chakula au kipindi cha kuupoza ubongo. Siyo unaingia kazini kabla hujashika faili lolote au hujawasha hata kompyuta unaanza siasa. Ukiwa mtu wa aina hiyo, utayaona mazingira ya kazi ni magumu na utajishushia heshima mbele ya mwajiri.

Mazungumzo na wafanyakazi wenzako muda wa kazi yawe yanahusu kazi. Siyo kujadili mfanyakazi mwenzako ana uhusiano wa kimapenzi na nani. Hayo siyo ambayo yaliwavutia wasaili wako kisha wakakuona unafaa kupewa kazi.

Tengeneza mtandao mzuri

Ni mtandao wa kazi. Ndani ya ofisi na nje. Hiyo ni kukusaidia kutimiza wajibu wako inavyotakiwa. Itakusaidia wakati wowote pale unapojiona umekwama kupata msaada wa haraka.

Waajiri wengi wana nongwa, hawapendi kuona mtu anasimama na kutembea kutoka meza moja kwenda nyingine akiwa kazini. Kwa hiyo, unapohitaji msaada kutoka kwa mfanyakazi mwenzako, mtumie barua pepe au ujumbe wa simu, kisha naye akujibu.

Mtambue mfanyakazi mzuri

Ukiwa mgeni kazini unatakiwa kumtambua mfanyakazi mzuri, anayetimiza wajibu wake na ambaye anamvutia hata mwajiri wako. Ukimshamjua mfanye kuwa rafiki na mshauri wako wa mambo ya kazi.