Muziki na siasa ni ndugu moja

Msanii Roma Mkatoliki

Muktasari:

  • Dk Mwakyembe ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuchukua nafasi ya Nape Nnauye alitoa tamko hilo alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule ambaye pia ni mwanamuziki maarufu kwa jina la Profesa J, kuhusu unyanyasaji wa wasanii wanaoimba nyimbo za siasa.

Wakati mashabiki na wasanii wakisubiri hatma ya tukio la utekaji wa wasanii Roma Mkatoliki, Moni Centrozone na Imma, hili ni pigo lingine kwa msanii mwenye wazo au aliyerekodi nyimbo zenye ujumbe wa siasa kutokana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kuwataka wasijihusishe na siasa.

Dk Mwakyembe ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuchukua nafasi ya Nape Nnauye alitoa tamko hilo alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule ambaye pia ni mwanamuziki maarufu kwa jina la Profesa J, kuhusu unyanyasaji wa wasanii wanaoimba nyimbo za siasa.

Kauli ya Dk Mwakyembe imeibua hoja katika mitandao ya kijamii kuhusu uhalali wa wasanii kuimba nyimbo zenye ujumbe wa kisiasa ambapo baadhi ya wadau na mashabiki wanakiri kauli hiyo itabana uhuru wa wasanii katika kazi zao huku wengine wakihoji ni siasa gani ambazo wasanii hawapaswi kujihusisha.

Binafsi naungana na kundi la watu wanaohoji kuhusu utata wa kauli hii kuingilia uhuru wa msanii suala lililofanya nijiulize mara kadhaa kwa nini sasa? Kwa nini umuhimu wa wasanii kutojihusisha na siasa uonekane sasa? Ni kipi hasa kimelazimu Waziri kutoa kauli hii? Au ni mafanikio ya wasanii wasioimba muziki wa siasa kama anavyodai?

Alipokuwa akijenga hoja hii Dk Mwakyembe alisema hakuna msanii aliyefanikiwa kwa kuimba siasa huku alimtaja Fella Kuti pekee kama msanii aliyeimba muziki wa siasa lakini aliishia pabaya. Imenishangaza Waziri kusahau kuwa Mbunge aliyemuuliza swali hilo Joseph Haule ndiye muasisi wa nyimbo za siasa hasa kwa tungo zake za ‘Ndio Mzee’ , Nang’atuka na ‘Sio Mzee’ zilizobadilisha mtazamo wa jamii kuhusu muziki wa kizazi kipya. Je, Profesa J sio mwanamuziki mwenye mafanikio au Waziri anapima vipi mafanikio ya msanii?

Ni siasa zipi hasa Dk Mwakyembe anataka wasanii wasijihusishe ikiwa chama chake cha CCM kinachoongoza dola kinamiliki bendi ya muziki inayotunga nyimbo zinazosifu siasa za chama hicho, kwani wale sio wasanii? Kama ni sawa kwa msanii kuimba nyimbo za kusifu uongozi kwa nini isiwe hivyo wanapohoji utendaji wa kazi za viongozi hao? Najua Mwanasiasa si mwenye ukamilifu usiohitaji kukosolewa hivyo wasanii waachwe wafanye kazi yao bila kuchaguliwa nini cha kuimba bali wasimamiwe katika maudhui ya nyimbo zao na ndio maana kuna Baraza la Sanaa Tanzania (Basata).

Kuna mifano mingi ya wasanii waliofanikiwa kwa kuimba tungo zenye ujumbe wa siasa, mwaka 2012 msanii Roma Mkatoliki alikuwa miongoni mwa wasanii waliofanya shoo nyingi nchini kuliko wengine na ndani ya mwaka huo alikabidhiwa tuzo ya Wimbo bora wa mwaka na Mwanamuziki bora wa Hip Hop katika tuzo za Muziki za Kilimanjaro kupitia wimbo wa Mathematics wenye maudhui ya siasa na utawala.

Ukitaja wasanii waliofanikiwa kimuziki nchini huwezi kumuweka pembeni Nay wa Mitego katika orodha hiyo, ni juzi tu Mwanamuziki wa nchini Marekani Katy Perry ameachia wimbo wa ‘Chained to the Rhythm’ unaofanya vizuri sokoni licha ya kuwa na ujumbe unaopinga siasa za Rais wa taifa hilo, Donald Trump.

Hata hivyo, nimkumbushe Waziri mafanikio ya msanii hayapimwi kimasilahi pekee, Muziki wa Hip hop una uzao tofauti ‘Genre’ kama Conscious, Rap na Trap katika Conscious ‘ngumu’ msanii hulenga kufikisha ujumbe katika jamii kuhusu mtazamo fulani alionao hapa msanii hutumia kipaji chake katika uchoraji wa mashairi kuliko kubuni mdundo na melodi ambavyo vina mvuto katika muziki wa biashara. Wasanii wanaofanya aina hii ya muziki ni kama Common wa nchini Marekani, Niki Mbishi, One the Incredible pamoja na Solo Thang katika wimbo wake wa Miss Tanzania.

Rai yangu kwa Waziri Mwakyembe, msanii hafanikiwi kwa kutokuimba siasa bali ni ubunifu anaoutumia katika kazi zake ndio utakaompatia mafanikio, kumchagulia msanii nini cha kuimba ni kubana uhuru wake utakaosababisha kuua vipaji vya wasanii wengi ambao asilimia kubwa ni vijana wanaotegemea kupata kipato kupitia muziki.

0755068131