Sunday, May 26, 2013

Christina Mbilinyi : Muziki wa Injili usitumike kwa dhana ya biashara

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi

Nikitaja wimbo wa ‘Nasubiria baraka’  itakuwa rahisi kutambua mapema ninayemzungumzia katika safu hii kwani wimbo huo umeokea umesambaa  na kujulikana ndani na nje ya nchi.

Dada huyu anaitwa Christina Mbilinyi (28), aliye na kipaji cha uimbaji alichokirimiwa na Mungu. Mashabiki wa nyimbo za Injili wanaposikia wimbo huo mara nyingi husimama na kucheza kwani unakubalika na kugusa maisha ya watu.

Kwa mara ya kwanza alipoanza kusikika masikioni kwa Watanzania, wengi walidhani dada huyu ni Mkenya kutokana na mpangilio wa mashairi na ladha ya uimbaji wake.

Msanii huyo amefanikiwa kushiriki mialiko mingi kwa ndani na nje ya nchi tangu alipotoa albamu ya wimbo huo mwaka 2011, amekuwa pekee kabla ya kumpata meneja aliyenaye kwa sasa.

Habari mpya kutoka kwa Christina ni sauti yake anayoipaza kwa waimbaji wa muziki wa Injili akionya uimbaji wa nyimbo hizo kutumika zaidi kama biashara.

“Sheria ya Mungu ni ngumu sana, Neno lake linasema walioitwa ni wengi ila watenda kazi ni wachache. Wengine wanafanya huduma kutoka ndani ya mioyo yao, wengine wanatanguliza sana pesa, wako kimasilahi zaidi, hiyo haipendezi,” anasema Christina.

Anafafanua kuwa kuna tofauti kati ya kuingia makubaliano na kuchangiwa gharama za mwaliko;  “Hilo linaeleweka, siyo lahisi kumwita mwimbaji bila kumwandalia nauli au marejesho ya gharama alizotumia kufika katika eneo hilo la huduma.”

Hata hivyo,  hakusita kueleza wazi kuwa baadhi ya mazingira yanawakatisha tamaa katika huduma hiyo na kusababisha waimbaji wengine kufikia uamuzi wa kupanga bei kama ilivyo kwa waimbaji wa nyimbo za mataifa.

Christina ambaye kwa sasa anatarajia kuipua albamu yake mpya itakayojulikana kwa jina la ‘Mtazamo wako’ , ni muumini wa Kikristo anayesali na kufanya huduma katika Kanisa la Mito ya Baraka lililopo Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Christina anajivunia mafanikio kwa kufahamika na kupata ushirikiano mzuri katika jamii pamoja na kuona watu wakipata baraka na faraja  kupitia kazi yake ya uimbaji.

 “Masuala ya mali ni ahadi tulizopewa, zipo tu zinakuja kwa wingi, maana amenibariki,”anasema Christina.

Nje ya Uimbaji

Baada ya kumaliza darasa la saba na kukwama kuelendelea kimasomo, Christina alijiunga na Chuo cha Ufundi Mbeya akisomea taaluma ya ushonaji.

Hata kabla ya kusikika,Christina alikuwa tayari ni fundi mzuri wa kushona na kudarizi nguo kwa mitindo mbalimbali inayofahimika mtaani.

“Kwa sasa natarajia kufungua ofisi kubwa itakayonisadia kufanya kazi zangu vyema, haitajihusisha zaidi  na ushonaji ila kuna kitu ninachofikiria kufanya kama biashara,” anasema Christina.

Historia yake

Binti huyu ni mzaliwa kutoka Kijiji cha Ivalalila wilayani Makete, Mkoa wa Iringa. Ni Mkinga aliyeokoka mwaka 2000 baada ya kukutana Kundi la Kwaya ya Shalom (EAGT) lililopo Mbeya Mjini.

Alianza kuimba akiwa na umri wa miaka 9 Kanisa la KKKT Usharika wa kijijini kwao. Hata hivyo, kutokana mapenzi aliyokuwa nayo juu ya uimbaji, ilijikuta akipata changamoto kwa wazazi wake baada ya kumwekea vikwazo vidogo vidogo.

“Nilikuwa na penda kuimba bila kujua hatima yangu itakuwaje, wakati mwingine nilijiuliza kwa nini inatokea hivyo?” anahoji Christina.

Akiwa mwanakwaya katika kundi hilo la Shalom alifanikiwa kukua na kutambua uwezo na kipaji chake baada ya kuaminiwa na mwalimu wa kundi hilo kuwa kiongozi na mtunzi wa mashairi.

Hata hivyo, hakuweza kudumu sana katika kundi hilo kutokana na changamoto alizokutana nazo kwa wanakwaya wenzake.

“Niliondoka bila kujua kama nilikwazika au la, ila namshukuru Mungu, yote nilishasamehe kwani yalikuwa ni majaribu ya kawaida ndani ya makundi ya kwaya,” anasema.

Christina ni yatima wa Baba,  ambaye alifariki miaka mingi iliyopita akiwa shule ya msingi.

“Ila mama yangu bado yupo na maisha yanaendelea,” anasema.

Uhusiano yake

Christina anasema kuwa uhusiano na jamii yake ni mazuri na anaishi kama mtu wakawaida tofauti na mtazamo unaoweza kuwepo.

Kwa huduma katika kanisa lake,Christina anasema kuna waimbaji wakubwa na muhimu sana. “Kuna waimbaji wengi tunashirikiana sana katika huduma pale kanisani ni msaada na washauri muhimu kwangu katika uimbaji,”anasema.

Baadhi ya waimbaji aliowataja Christina kanisani hapo ni pamoja na Bonifasi Mwaitege, Bahati Bukuku, Frola Mbasha, Masanja mkandamizaji na wengine wengi.

-->