Muziki wa taarabu unapotea kwa kukimbizana na mabadiliko

Muktasari:

NYIMBO ZIWE FUPI

Kinachokwamisha nyimbo za taarabu kuchezwa katika vipindi vingi ni urefu wa nyimbo zenyewe. WImbo wa Taarabu una urefu wa dakika 20 mpaka 30 wakati Bongo Fleva ni dakika 3-5.

Muziki wa Taarabu ulianza kukwama  pale Abdul Misambano na vijana wenzake walipoanza kuupa kisogo ule wa asili.

Yalikuwa ni mabadiliko ya muda mrefu, yalianzia kwa kibao kama ‘Asu’ lakini miaka michache baadae yakazaa bendi kama Jahazi na nyingine nyingi ambazo kwa pamoja zilijinasibu kwamba zinafanya muziki uitwao ‘Morden Taarab’  au Taradansi.

Tangu pale mambo yakawa tofauti, sasa hata wasanii wa taarabu wakaanza kupata fedha iliyowapa nguvu ya kujivunia wanachokifanya ingawa siyo kwa kiasi kikubwa.

Pengine yale ndiyo yalikuwa mabadiliko ya pekee ya maana kwa muziki wa taarabu tangu kuumbwa kwa dunia.

Bila shaka baada ya pale hakuna mabadiliko ya kimaendeleo yaliyowahi kufanywa katika aina hii ya muziki kama ilivyo kwa Bongo Fleva.

Kimsingi bendi na wasanii wanaoimba taarabu kwa sasa ni kama hawaelewi wanachofanya. Hawaelewi wamesimama upande gani, wanafanya aina gani ya muziki; dansi, singeli au muziki wa pwani.

Ni kama hawaelewi wanafanya muziki kwa ajili ya mashabiki wa enzi gani, enzi za  Baba wa Taifa au Magufuli. Hii inawapa ugumu hata kujua jinsi gani wanaweza kuboresha muziki wao.

Inashangaza  mpaka leo wenye taarabu  wameshindwa kuufanya muziki huu kuwa wa kusikilizwa na kila mtu. Taarabu imekuwa ni ya kusikilizwa na aina fulani ya watu ambao kwa mtazamo wa kawaida wanaonekana ni wanawake hasa wenye tabia za kupenda ‘Uswahili’.

Wameshindwa kuiga mfano wa Bongo Fleva ambapo wakati wanaanza ulikuwa ukionekana ni muziki wa wavuta bangi, lakini leo hii wasanii  wanaitwa Ikulu kuburudisha zinapofanyika hafla mbalimbali.

Nyimbo ndefu

Inashangaza hadi leo wanaoimba taarabu wameshindwa kutengeneza nyimbo za muda mfupi ili kwamba muziki wao usikike katika vipindi mbalimbali vya redio na televisheni.

Taarabu  inaishia kupigwa kwenye vipindi maalumu kwa sababu vipindi vingine vinahitaji burudani fupi isiyotafuna muda.

Video hazina ubora

Hadi leo hii nyimbo za taarabu zina video za kizamani ilihali wenyewe wanajiita ni ‘modern’ kwa maana ya muziki wa kisasa.

Zinaitwa video kwa sababu picha zake zimerekodiwa kwa kamera yenye kunasa mijongeo na mawimbi ya sauti.

Ni video zinazoonesha wanawake wa bendi husika wamevaa magauni bila mpangilio maalumu unaopendeza, wanachezacheza tu alimradi, kana kwamba wanakwenda kumtunza mwenzao kwenye ‘kitchen party’.

Inashangaza sana; wakati Bongo Fleva wanahangika huku na kule duniani kutafuta maeneo ya utofauti ya kupigia picha za video zao, taarabu wenyewe bado kila video yao wanayoitoa lazima kuwe na kipande cha ufukwe tena zilezile za kila siku ambazo hata hazijatengenezwa vyovyote kuendana na umuhimu wa zoezi la upigaji picha za video.

Haina ubishi kwamba taarabu ni moja ya lulu za kiburudani tulizobarikiwa Watanzania. Ni miongoni mwa muziki mkongwe na wa kwanza kuingia nchini.

Bila shaka ili kuilinda na kuitunza lulu hii wanaoimba taarabu wanastahili kuangalia jinsi ya kuboresha muziki wao  na ili kufanikiwa katika hilo ni lazima wawe na mada tofauti katika miziki yao au  hata kama ni zile zile waziimbe kwa ubunifu kidogo.

Waangalie jinsi ambavyo wanaweza kuufanya kwa kutengeneza nyimbo fupi ili pia isiwe tabu kutumika kwenye vipindi mbalimbali vya redio na televisheni vinavyopambana.

Pia, wawe na msimamo, sio kila kukicha wanaitohoa taarabu  ya aina nyingine ya muziki. Miluzi mingi humpoteza mbwa.