Mwanafunzi asifungwe na darasa kupata maarifa

Muktasari:

Wengine wanahusianisha maarifa, elimu na majengo ya madarasa kuwa ndio chimbuko la maarifa. Wengine wanaeleza kuwa maarifa yanaweza kupatikana hata nje ya jengo la darasa ikiwamo kupitia maono na ndoto.

       Kuna mijadala mingi kuhusiana na vyanzo vya mtu kujipatia maarifa, ujuzi au stadi mbalimbali za maisha.

Wengine wanahusianisha maarifa, elimu na majengo ya madarasa kuwa ndio chimbuko la maarifa. Wengine wanaeleza kuwa maarifa yanaweza kupatikana hata nje ya jengo la darasa ikiwamo kupitia maono na ndoto.

Kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili ya Longhorn 2017, neno maarifa lina maana ya ujuzi aghalabu wa kuzaliwa nao, anaoutumia mtu kupambana na maisha yake kila siku; au mbinu; hekima na busara. Pia, maarifa ni elimu aipatayo mtu kutokana na kusoma, kusikia au kutenda; uzoefu au ustadi.

Vilevile, maarifa huweza kufasiliwa katika dhana mbalimbali za kifalsafa kama epistemolojia; kama mojawapo ya tawi la falsafa linalojihusisha na hali na upana (vikwazo) vya maarifa.

Hapa maswali kadhaa huhojiwa. Kwa mfano, maarifa ni nini; maarifa hupatikana wapi; je, watu hujua nini; na je hujua vipi kile ambacho wanajua?

Dhana hiyo imejikita katika uchambuzi wa hali ya maarifa na jinsi maarifa yanavyohusiana na dhana sawa kama vile imani, ukweli ama ushahidi. Pia, inahusu mbinu na uzalishaji wa maarifa na shaka kuhusu madai mbalimbali ya maarifa.

Mwanafunzi ni mtu anayepata mafunzo ya taaluma au stadi akiwa chini ya uangalizi wa mwalimu. Maswali ambayo watu wanaweza kujiuliza ni kwamba katika jamii yetu maarifa na ujuzi mbalimbali hupatikana katika shule pekee?

Nchi nyingi zilizoendelea zilifanya juhudi kubwa katika kuwekeza katika maarifa kwa watu; na maarifa hayo kuendelea kupatikana hata nje ya jengo la darasa. Kwa kufanya hivyo walijikuta wakivumbua vitu vingi vilivyo msaada kwa dunia yote.

Ni kweli kwamba uvumbuzi wao umerahisisha kazi na ni wajibu wetu kutafuta maarifa ya kutengeneza na kuongezea uwezo wa walivyovumbua.

Ni vema wanafunzi wetu wakafahamu kuwa uwekezaji unaofanyika kwao wa kupata maarifa, ndiyo utakaokuwa na mchango mkubwa katika maendeleo yao binafsi, jamii na taifa kwa jumla.

Hivyo wapatapo fursa za kuwa shuleni wahakikishe wanapata maarifa stahiki kwa kadri inavyopaswa. Kwa mfano, nchi inapokuwa na maono ya kuwa taifa la uchumi wa kati kupitia mabadiliko makubwa ya uchumi wa viwanda, ni wajibu hata kwa walimu kusaidia kwa kubadilisha mtazamo wao. Na wanafunzi nao wawe tayari kupokea maarifa katika mtazamo huo wa uchangiaji katika sekta ya viwanda.

Kwa lugha nyingine ni pale jamii itakapoweza kuwekeza kwenye maarifa ya watu wake, basi maendeleo ya kweli na endelevu hayakosi kuwapo. Si rahisi kuendelea bila maarifa ya uzalishaji. Kujitegemea kutokane na juhudi za jamii na wasomi wenye maarifa ya kujizalishia vitua au kwa maendeleo yao na kwa biashara.

Shule zinaruhusu watu kupata maarifa nje ya darasa?

Mbinu za ujifunzaji na ufundishaji za mwalimu zichokoe kiu ya ndani ya mwanafunzi katika kujenga hali ya kujitegemea kufikiri na kutafuta maarifa mengine hata nje ya mipaka ya darasa. Wanafunzi wasifungwe na mipaka ya shule katika kupata maarifa au stadi zenye faida kwao na kwa jamii husika.

Kwa mfano; sehemu za wafugaji maarifa ya ufugaji bora utakaokuza uchumi na kubadilisha hali za maisha kuwa bora ni jambo la kuhamasisha.

Wengine wanaotoka katika maeneo ya uwindaji, uvuvi, kilimo, uchongaji na ususi, nao wanapaswa kupewa fursa ya kupata maarifa katika shule na mazingira yanayowazunguka ili elimu wanayoipata iweze kuleta maana na manufaa kwao.

Pia, wazazi wana mchango mkubwa katika kuhakikisha mtoto au mwanafunzi habanwi na ile dhana kuwa elimu hupatikana shuleni tu. Wao pia wanaweza kuwajengea watoto na vijana kuwa na nidhamu ya kazi na kupenda kufanya kazi tangu wakiwa nyumbani na kwenye jamii. Kwa sababu nidhamu, jitihada na nia ya dhati ya kufanya kazi kwa bidii na maarifa, hunyanyua taifa.

Walimu na jamii kwa pamoja wana kazi ya kujenga elimu ambayo haina malengo ya kibinafsi ila yenye malengo ya kuleta mapinduzi kwenye jamii na taifa kwa jumla. Hii ni elimu ambayo itasaidia kuinua jamii na siyo kuiangamiza; ambayo hujenga mwelekeo wa kitaifa na sio wa kibinafsi; na ambayo hujenga maadili ya watu kwa kujua kati ya usahihi na upotofu na hatimaye kufuata kilicho sahihi kwa faida ya taifa letu.

Mathalani, wapo watu ambao husoma lakini wanajiangalia wenyewe tu badala ya kusaidia jamii yao; jambo ambalo husababisha elimu yao kuwa na manufaa madogo katika kuleta mapinduzi kwenye jamii.

Watu hawa kimsingi wanapaswa kuleta mabadiliko kwenye jamii inayowazunguka, ili kukamilisha ile dhana ya thamani ya elimu.

Hivyo, maarifa yatokanayo na mbinu na njia mbalimbali za ufundishaji na ujifunzaji za walimu shuleni, zinapaswa kujenga misingi imara ya kimaadili. Jitihada za kutafuta maarifa na stadi stahiki zijengwe kwenye maadili ya jamii na taifa.

Hakuna taifa ambalo watu wake wameendelea bila kuwa na maarifa. Kwa hiyo ni muhimu kujifunza na kusoma bila kuchoka hata nje ya darasa rasmi na kutumia maarifa hayo kwa faida ya taifa na jamii kwa jumla.

Ni wajibu wa jamii nzima kuhakikisha kuwa watoto na vijana wetu wanaosoma katika shuleni na vyuoni, hawabanwi na mawazo kwamba maarifa na stadi pekee hupatikana katika majengo ya shule.