Dk Edith Lyimo : Mwanamke shujaa hukabiliana na kila jaribu

Dk Edith Lyimo

Muktasari:

  • “Pamoja na magumu niliyowahi kupitia kwenye maisha yangu, sikuwahi kukata tamaa, namshukuru Mungu kwa sababu bidii imenifikisha hapa nilipo,” anasema.

Dar es Salaam. Kila mwenye mafanikio kuna njia alipita ili kuyafikia. Mkuu wa Idara ya Fasihi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Edith Lyimo anasema uvumilifu, kutokata tamaa na kufanya kazi kwa bidi ndio siri kubwa ya kila mwenye ndoto za mafanikio, kuzifikia.

“Pamoja na magumu niliyowahi kupitia kwenye maisha yangu, sikuwahi kukata tamaa, namshukuru Mungu kwa sababu bidii imenifikisha hapa nilipo,” anasema.

Kitu pekee ambacho hatakisau maishani mwake ni siku mwanae, alipochomwa sindano ambayo ilimuharibu viungo.

Wahenga walisema hujafa hujaumbika! Mwanae alizaliwa akiwa mzima na mwenye afya, na hakuwahi kutarajia kama ipo siku mtoto huyo atashindwa kutembea wala kuzungumza.

“Ilikuwa mwaka 2001, mwanangu Angel alipougua, nilimkimbiza hospitali ambako alikutwa na malaria hivyo akachomwa sindano iliyosababisha ulemavu wake mpaka leo,”anasema.

Edith anasema sindano hiyo iliongeza ugonjwa kwa mtoto huyo ambaye alihamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kulazwa chumba cha wagonjwa mahututi kwa siku kadhaa.

Alipata nafuu na kuruhusiwa. Tangu hapo mwanae amelemaa na hakuna matumaini tena ya kurejea kwenye hali hake ya zamani.

“Nilihangaika hospitali zote kupata tiba ya mwanangu lakini ilishindikana na mwisho wa siku madaktari wananisihi niendelee kumlea kwani, hatarejea katika hali ya awali,”anasema.

Tangu wakati huo mpaka sasa amekuwa akitumia muda mwingi kwa ajili ya kumhudumia kwa kuwa ana mahitaji maalumu, ikilinganishwa na wenzake waliozaliwa baadaye.

Edith anakiri kuwa mumewe, Humphrey Mongi hakuwahi kumkatisha tamaa wala kumsukuma ili arudi nyuma badala yake amekuwa msaada mkubwa katika malezi ya mtoto huyo na wengine jambo ambalo linamfanya aendelee kutimiza ndoto zake.

Kwa sasa yupo mbioni kuusaka uprofesa kwa kuendelea kuandika tafiti mbalimbali ambazo mbali na kumfikisha kwenye ndoto hiyo, zinasaidia kujibu maswali magumu yanayojitokeza kwenye jamii.

Safari yake kimaisha

Edith alizaliwa mkoani Kilimanjario akiwa mtoto wa kwanza katika familia yao.

Wakati akiwa darasa la saba katika shule ya msingi Mkyashi mwaka 1983, mwalimu wake Erast Tesha alibaini kipaji chake na kuwasihi wazazi wake, wamtafutie shule nzuri ya sekondari itakayosaidia kutimiza ndoto zake.

“Jambo hilo lilimchanganya mama yangu ambaye kwa wakati huo hakuwa na uwezo wa kunisomesha kwenye shule za gharama,”anasema.

Alibahatika kupata nafasi kwenye shule ya Sekondari Kibosho ambako alianza kidato cha kwanza na kufanikiwa kumaliza kidato cha nne akiwa miongoni mwa wasichana waliofaulu vizuri kwenye masomo yao.

Alijiunga na shule ya Sekondari Zanaki mwaka 1990, akisoma kidato cha tano na sita kabla ya kwenda jeshini Makutupora kama, sheria ilivyokuwa inataka.

Anasema kwa kuwa alikuwa mtoto wa kwanza kutoka familia inayoishi kijijini, hakuwa na mtu wa kumuongoza hivyo ilimlazimu kutumia akili ya ziada na hekima katika kufanya maamuzi na nini anapaswa kufanya kwa wakati huo.

Alijiunga chuo kikuu cha UDSM mwaka 1994 akisomea shahada ya ualimu na kuhitimu mwaka 1998.

“Mungu mwema kwani nilipata ajira Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita), na hapo sasa nikaanza kuwa msaada kwa wazazi wangu na wadogo zangu, ambao niliwasihi wafanya bidii kutimiza ndoto zao,”anasema.

Afunga ndoa

Anasema baada ya kuhitimu masomo yake, mwaka 1999 ulikuwa muafaka kwake kufunga ndoa na mumewe Mongi, ambaye mpaka leo wanaishi kwa furaha na upendo.

“Sijawahi kujuta kuolewa, tunaheshimiana na kupendana na kikubwa nilichojifunza kwenye ndoa ni kwamba tunapaswa kuchukuliana, kuvumiliana na kila mmoja kumuona mwenzake anathamani kubwa,”anasema.

Mwaka 2000 alipata mtoto wa kwanza, Angel ambaye kwa bahati mbaya alikutwa na ulemavu akiwa na umri wa mwaka mmoja.

Wakati anajifungua mtoto huyo, alikuwa tayari ameanza masomo yake ya Shahada ya Uzamili UDSM, hivyo akawa na wakati mgumu katika kujigawa.

“Kumbuka hapo nilikuwa mfanyakazi, mama wa mtoto anayenihitaji muda wote na mwanafunzi. Nilianza kukata tamaa nikitaka kuacha hayo mawili nibaki kumlea mwanangu ambaye, nilijua anahitaji ukaribu wangu kuliko wakati wowote,”anasema.

Mumewe na rafiki zake walimtia moyo kwa kumtaka asikate tamaa.

Hata hivyo, changamoto kubwa anayokutana nayo ni wasichana wa kazi wenye uwezo wa kumsaidia mtoto wake wakati anapokuwa kazini.

Azungumzia walemavu

Edith anasema jamii haipaswi kuwatenga watu wenye ulemavu badala yake, wawapende, kuwatunza na kuhakikisha mahitaji yote yanatimia.

Anasema matukio mengi ya watu wenye ulemavu kufanyiwa ukatili, yanalifanya kundi hilo kujisikia vibaya na kwamba, hawastahili kufanyiwa hayo.

“Ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu unatokana na mawazo mgando kwamba, hawastahili. Hawa ni watu kama wengine, lazima familia, jamii na taifa liweke mkakati namna ya kuwatunza na kwa wale wenye uwezo wa kufanya kazi, wawekewe mazingira mazuri,”anasisitiza.