Mwandae hivi mwanao kwa mwaka mpya wa masomo

Muktasari:

Kuanza kwa muhula mpya wa masomo kunaweza kuleta changamoto fulani kwa watoto. Kwanza mtoto anatoka kwenye ratiba yenye kiasi fulani cha uhuru nyumbani na anarudi kwenye mazingira atakayolazimika kufuata ratiba isiyobadilika.

Shule zimeanza kufunguliwa wiki hii na watoto wanaanza muhula mpya wa masomo baada ya mapumziko marefu ya mwisho wa mwaka.

Kuanza kwa muhula mpya wa masomo kunaweza kuleta changamoto fulani kwa watoto. Kwanza mtoto anatoka kwenye ratiba yenye kiasi fulani cha uhuru nyumbani na anarudi kwenye mazingira atakayolazimika kufuata ratiba isiyobadilika.

Lakini pia mtoto anaporudi shuleni, anaachana na watu wa karibu wa familia yake, ambao ndio hasa wanaomwelewa na pengine kumsikiliza vizuri zaidi na kwenda kukutana na watu ambao wakati mwingine hawana nafasi ya kujenga uhusiano wa karibu naye. Haya mawili yanaweza kumfanya mtoto asifurahie sana kurudi shule.

Kwa upande wa mzazi, hiki ni kipindi cha pilika nyingi za kuhakikisha mtoto anapata vifaa na mahitaji muhimu yanayohitajika shule ikiwa ni pamoja na sare mpya za shule, viatu, begi, madaftari, kalamu, vitabu na vifaa vinginevyo vya lazima shuleni.

Kwa kuzingatia kupanda kwa gharama za maisha, hiki kinaweza kisiwe kipindi kizuri kwa wazazi wenye majukumu mengi ya kufanya.

Katika makala haya, nakusaidia kutazama namna gani unaweza kumwandaa mwanao kuanza mwaka mpya wa masomo hata katika mazingira magumu kiuchumi.

Unatambua uwezo wake?

Wajibu mkubwa ulionao mzazi ni kumfanya mtoto si tu atambue uwezo wake, lakini aweze kuukuza na kuuishi. Mtoto anayesoma tu bila kujua uwezo wake ni sawa na gari zuri lisilo na tatizo, lakini linaendeshwa na dereva asiyejua wapi anakwenda. Uwezekano wa kupata matatizo unakuwa mkubwa.

Ni muhimu mzazi kufanya jitihada za kujua uliko moyo wa mwanao. Jitahidi kadri unavyoweza kujaribu kumsaidia kujitambua mapema. Mtoto akiujua uwezo wake, atakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kufahamu afanye nini na elimu atakayoipata darasani.

Kuna namna nyingi za kumsaidia mtoto kujua uwezo wake. Mojawapo ni kumruhusu kushiriki shughuli mbalimbali zinazomfanya aguse vitu vingi vinavyohitaji ujuzi wa namna mbalimbali. Mtoto anaposhiriki shughuli hizi itakuwa rahisi kujua wapi ana uwezo zaidi na wapi moyo wake hauelekei.

Unaonyesha imani kwake?

Kama kuna jambo la msingi unaloweza kumfanyia mwanao ni kumfanya ajiamini. Mtoto asiyejiamini hawezi kufanya mambo mengi. Ndani yake kutakuwa na sauti inayomzomea muda mwingi na atakuwa na tabia ya kujisema maneno ya kujikatisha tamaa.

Maneno unayomwambia mara kwa mara ndiyo hasa yanayotengeneza sauti hii inayoweza kutoka ndani yake kumkatisha tamaa. Kama mzazi, shiriki kazi kubwa ya kutengeneza sauti chanya atakayoisikia mwanao. Mfanye ajiamini na kujisemea maneno yanayomwongezea hamasa ya kufanya mambo.

Kikubwa unachoweza kukifanya ni kumwonyesha mwanao kuwa una matarajio makubwa kwake. Hata katika mazingira ambayo hafanyi vizuri darasani kama unavyotaka, bado unaweza kuzungumza nae kwa namna inayotuma ujumbe kuwa unamwamini.

Usifanye kosa la kuonyesha umemkatia tamaa. Mtoto anahitaji kujua mzazi wake anamwamini.

Umemwekea mazingira mazuri?

Mazingira mazuri ya kujifunzia yana nafasi kubwa ya kusababisha mafanikio ya mtoto. Watoto wanapokutana na mazingira yanayowahamasisha kujifunza, wanakuwa na kazi nyepesi ya kufanya.

Tunapozungumzia mazingira mazuri tuna maana ya kuhakikisha anapata vifaa anavyovihitaji katika kujifunza; ushirikiano wa karibu kati yake na mzazi na kuona wanaomzunguka nao wanathamini kujifunza.

Hebu anza mwaka kwa kuhakikisha mtoto anajifunza bila wasiwasi. Kadri inavyowezekana, msaidie kujua unafuatilia masomo yake. Hakikisha amefanya kazi za shule anazorudi nazo nyumbani. Kagua madaftari yake mara kwa mara na pia jenga tabia ya kuulizia amejifunza nini shuleni.

Aidha, ni nyema kutengeneza mazingira rafiki nyumbani yatakayomhamasisha mtoto kujifunza. Msaidie kutengeneza ratiba ya siku anaporudi nyumbani ili ajue anapaswa kufanya nini kwa wakati gani.

Dhibiti matumizi ya televisheni lakini pia mpe kiasi fulani cha uhuru wa kufanya mambo mengine nje ya masomo.

Umemsaidia kujua ndoto zake?

Ndani ya kila kichwa cha mtoto kuna matamanio ya kufanya kazi fulani. Mtoto anaona watu wazima wanaofanya kazi tofauti tofauti. Watu hawa kwa namna moja au nyingine wanamjengea ndoto fulani katika maisha.

Ukimuuliza mtoto yeyote anataka kuwa nani, hatokosa kukutajia kazi anazozifahamu kwenye mazingira yake. Hata hivyo, matamanio haya si lazima yawe ndoto zake. Wakati mwingine kazi anazosikia zina heshima katika jamii, ndizo zinazojenga matamanio yasiyoendana na uhalisia wake.

Mwaka huu jipange kumsaidia mtoto kujitambua. Mruhusu mtoto akacheze michezo mingi inayomfanya aigize shughuli mbalimbali anazoziona kwenye mazingira yake. Mkutanishe na watu maarufu wanaofanya vizuri kwenye maeneo yao ya utaalamu.

Msimulie hadithi za watu waliowahi kufanya mambo makubwa katika maeneo yao ya utaalamu. Ikiwezekana, mpeleke mtoto kwenye maonyesho, maeneo ya kihistoria, maktaba na hata kutembelea vyuo vikuu.

Changamoto hata hivyo, wazazi wengi tuna tatizo la kutaka watoto wawe vile tunavyotaka sisi. Kwa maana nyingine, ni kama tunataka watoto wawe nakala ya maisha yetu badala ya kuwaruhusu kuwa vile walivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu.

Mpe mtoto mwongozo unaomwezesha kuwa kile alichokusudiwa kuwa. Usijaribu kutimiza ndoto zako ulizoshindwa kuzitimiza kwa kumtumia mtoto.

Unamsaidia kuweka malengo?

Wajibu mwingine muhimu kwako kama mzazi ni kusaidia mtoto kujiwekea malengo yake ya kimasomo. Watoto wengi hushindwa kufanya vizuri darasani kwa sababu hawana malengo. Hawajui wanalenga kufikia hatua gani kwa mwaka husika.

Msaidie mwanao kujipanga mapema kipindi hiki anapoanza masomo. Kaa naye muweke malengo yanayolingana na hali halisi. Kwa mfano, kama mtoto anashika nafasi ya chini darasani, zungumzeni muone anaweza kupanda mpaka wapi kwa muhula huu wa kwanza.

Kosa unaloweza kulifanya mzazi ni kumwekea malengo ya juu mno yasiyoendana na uwezo na mazingira yake. Lakini pia ni muhimu kuelewa kuwa malengo yasiyopimika kila mara, hayana maana. Msaidie mtoto kuweka utaratibu mzuri wa kupima maendeleo yake kila mara.

Blogu: http://bwaya.blogspot.com