Myoma haina uhusiano na saratani

Muktasari:

“Baada ya kufikiria kila jambo ikiwamo kurogwa nilikata shauri kwenda hospitali, nilianzia Arafa Mbagala , kabla ya kuhamia Temeka kwa vipimo zaidi, ambapo nilibainika nina uvimbe tumboni na nikaelezwa ni wa aina gani na una tofauti gani na fikra nilizokuwa nazo, ”anaanza kueleza Jamila Kulwa mkaazi wa Mbagala Rangi tatu (42) mchuuzi wa mbogamboga, aliyefanyiwa upasuaji kuondoa Myoma.

Dar es Salaam. “Nimeteseka kwa miezi sita sasa, nikiwa kwenye siku zangu damu inakuwa nyingi, sikuwahi kufikiria kuhusu uvimbe tumboni na kila niliyesikia ana uvimbe nilihisi anaweza kuwa na saratani.

“Baada ya kufikiria kila jambo ikiwamo kurogwa nilikata shauri kwenda hospitali, nilianzia Arafa Mbagala , kabla ya kuhamia Temeka kwa vipimo zaidi, ambapo nilibainika nina uvimbe tumboni na nikaelezwa ni wa aina gani na una tofauti gani na fikra nilizokuwa nazo, ”anaanza kueleza Jamila Kulwa mkaazi wa Mbagala Rangi tatu (42) mchuuzi wa mbogamboga, aliyefanyiwa upasuaji kuondoa Myoma.

Anasema alipoambiwa ana uvimbe tumboni akili ilizunguka mara kadhaa na kuona ndio basi tena ameshapata saratani ya tumbo, baada ya kupata maelezo ya kina kuhusu ugonjwa huo akagundua kuwa siyo tatizo kubwa kama alivyokuwa akifikiri.

“Nilishauriwa kufanyiwa upasuaji kutokana na hali yangu nilikuwa napata hedhi nyingi kiasi cha kupungukiwa damu, huu mwezi wa tatu tangu nifanyiwe napata kama kawaida na sisikii maumivu yoyote ikiwamo ya mgongo yaliyokuwa yakinitesa, ”anasema.

Kwa mujibu wa mtandao wa taifa wa afya ya wanawake wa nchini Uingereza umeeleza asilimia 30 ya wanawake wanapata myoma wakiwa na umri wa miaka 35 na asilimia 70-80 hupata maradhi hayo wakiwa na umri wa miaka 50 wengi kati ya hao hawana uelewa kuhusu maradhi hayo.

Bingwa wa magonjwa ya kina mama katika Hospitali ya Temeke Zaituni Mgaza anawataja wanawake waliopo katika hatari ya kupata maradhi hayo ni wanawake ambao wamekaa muda mrefu bila kuzaa, ingawa sababu hasa ya maradhi hayo haijulikani.

Myoma au Fibroids ni nini?

Dk Mgaza anaeleza kuwa myoma au Fibroids ni uvimbe wa misuli laini vimbe ambao hutokea kwenye tumbo la kizazi ambao huu uvimbe unaweza kuwa ndani ya kizazi(ukutani mwa kizazi) au ndani ya nyama ya kizazi na nje kwenye ukuta wa kizazi.

Anasema Fibroids ni uvimbe ambao mara nyingi (asilimia 99) hauna madhara kiafya na wala kuhusiana na ugonjwa wa kansa.

Anafafanua kuwa uvimbe wa fibroids unakuwa na ukubwa tofauti tofauti, unaweza kuwa mdogo kama harage au kufikia ukubwa wa tikiti maji.

Chanzo Cha Fibroids

Sababu hasa za kuota kwa fibroids katika viungo vya uzazi vya mwanamke bado hazieleweki vizuri ingawa inaamika kwamba kila uvimbe wa fibroid unatokana na seli ya misuli ya uterus ambayo imeamua kuwa na tabia ya tofauti na nyingine na ikaanza kukua kwa haraka ikichangiwa na uwepo wa homoni ya estrogen.

Dalili za Fibroids

Dk Mgaza anasema baadhi ya kina mama huwa hawaoni dalili zo zote zile (wengi hawajui kama wana fibroids) au kuona dalili kidogo na kwa wengine dalili hizi hujitokeza sana na kuwasumbua hadi kufikia kutafuta tiba.

Anazitaja baadhi ya dalili kuwa ni pamoja na kutokwa na damu kwa wingi wakati wa siku au kutokwa na damu kwa muda mrefu.

Anasema wengine hutokwa na damu hata kama wamemaliza siku zao, maumivu yanyonga na kupata haja ndogo mara kwa mara, maumivu ya mgongo.

Dk Mgaza anasema kuwa wagonjwa wa ugonjwa huo wameongezeka kwa kiasi fulani ambapo hupokea wanne au watano kwa siku na wakati huo huo wodini wanakuwapo wawili au watatu wanaosubiri upasuaji.

“Tunahakikisha kwa wiki tunawafanyia upasuaji wagonjwa wa myoma wawili , na wanaolazwa ni wale wanaokuja katika hali mbaya kutokana na kupoteza damu nyingi.

“Ugonjwa huo kwa baadhi ya kina mama kama nilivyokwisha sema huwafanya watokwe na damu nyingi, hivyo uhishiwa damu mwilini na hupata maumivu makali, ”anasema Dk Mgaza.

Kutokana na ongezeko la kina mama wenye ugonjwa huo Naibu Waziri wa Wizara ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Hamisi Kigwangalla aliutolea ufafanuzi ugonjwa huo.

Dk Kigwangalla anasema Myoma au kwa jina la kitaalamu unajulikana kama ‘Uterine Fibroid’ ni uvimbe unaoota kwenye misuli ya tumbo la uzazi wa mwanamke.

Anasema Chanzo halisi cha Myoma hakijulikani ila kila Myoma huanza kwa ukuaji hovyo wa seli moja, ambayo hutoa protini kwa wingi. Tafiti pia zimeonyesha Myoma hutokana na mabadiliko ya vinasaba kwenye seli za Myoma ambazo hubadilisha ukuaji wa seli hizo.’

“Myoma ni uvimbe ambao siyo Saratani, na hauna tabia ya kubadilika kuwa saratani, Myoma ikiwa kubwa huweza kuonyesha dalili kama kuvimba tumbo, kuvuja damu kwa wingi na maumivu makali ya tumbo chini ya kitovu, ”anasema Dk Kigwangalla.

Dk Kigwangalla anawashauri kina mama kupima maradhi hayo badala ya kusubiri hadi yawaletee athari kulingana na dalili zake.

Matibabu

Kwa mujibu wa Dk Godwin Singalu (hakuwa tayari kutaja hospitali anayofanyia kazi kwa madai kuwa siyo msemaji wake), alisema

Kwa hapa nchini tiba kuu ni upasuaji ambao pia hutegemea aina ya uvimbe ukubwa kero zake kwa muhusika ikiwamo kutoka damu isivyo kawaida na maumivu makali.

Anaitaja miongoni mwa aina za upasuaji inajulikana kwa kitaalamu kama Myomectomy , huu ni upasuaji wa kuondoa uvimbe mmoja mmoja bila kuondoa kizazi kwa wale wenye uvimbe mmoja ulioko sehemu nzuri.

Anaitaja aina nyingine kuwa ni Total abdominal hysterectomy. Upasuaji huu unaondoa kizazi chote kama uvimbe umekaa vibaya na viko vingi.

Ni lazima kupata tiba ya ugonjwa huu?

Dk Singalu anasema kila kama mwanamke hapati usumbufu wa namna yoyote katika shughuli zake za kawaida, anaweza asipewe tiba ya aina yo yote hata kama imegundulika kuwa ana uvimbe wa fibroid.

Anasema hasa kwa kina mama wenye umri mkubwa kwa sababu mwanamke anapokaribia kukoma hedhi fibroids hunyauka zenyewe na mara nyingine kutoweka kabisa.

Anafafanua kuwa iwapo atalazimika kupatiwa tiba , anaweza kupewa dawa au kufanyiwa upasuaji kutokana na hali iliyopo.

“Tiba zipo aina nyingi lakini kwa hapa nchini bado zinatumika hizo, kuna ambao wanapewa dawa za kunyausha ambazo kitaalamu siyo nzuri sana ndiyo maana hali ikiwa mbaya unafanyika upasuaji, ”anasema Dk Singalu.