UCHAMBUZI: Mzegamzega utapunguza ufanisi wa Mkuu wa nchi

Muktasari:

Mmoja mbele na mwingine nyuma au kushoto na kulia au Mashariki na Magharibi.

Siku hizi ukimsikia mtu anamwambia mwenzake ameamua kuwa mzegazega basi maana yake ni kwamba ameoa mke wa pili.

Mmoja mbele na mwingine nyuma au kushoto na kulia au Mashariki na Magharibi.

Hata hivyo, miaka ya nyuma hadi katikati ya miaka ya 1970 unapomtaja mzegazega Zanzibar na sehemu nyingi za ukanda wa pwani, huwa anayeelezewa ni mtu anayechota maji na kuyauza kwa kutumia madebe mawili.

Madebe hayo mara nyingi ni yale yaliyokuwa yakitumika kuwekea mafuta ya taa au samli, huning’nizwa kwenye mti, moja mbele na jingine nyuma na mtu aitwaye mzegazega.

Siku hizi waliokuwa wakiutwa mzegamzega wametoweka na kama wapo ni wahache nao wachota maji na kuyauza kwa hutumia magari au mikokoteni.

Nilipokuwa mdogo nilivutiwa na ustadi wa wabeba mzegamzega kwa jinsi walivyoliweka katikati ya bega moja gongo lililobeba madebe mawili ya maji na kutembea kwa haraka walipokuwa wanakwenda kuyauza bila ya kudondosha hata tone njiani.

Madebe mawili yaliyokuwa na karibu kilo 20 za maji katika kila debe yalikuwa yakining’inia wakati wote mzegazega alipokuwa safarini kwenda kuyauza.

Kwa kweli ilikuwa kazi ngumu na yenye sulubu iliyohitaji siyo nguvu tu za misuli, bali pia maarifa, vinginevyo madebe ya maji yangelimwangusha au yangefika nusu kutokana na kumwagika njiani.

Anachotaka kufanya Magufuli

Hivi sasa ninaiona kazi anayotaka kufinya Rais John Pobe Magufuli ya kuwa kiongozi wa nchi (kama Rais) na wakati huo huo mwenyekiti wa CCM kama mzegamzega.

Pia, tusisahau kwamba kwa mujibu wa Katiba, kama za nchi nyingine, Rais ni Amiri Jeshi Mkuu wa nchi yetu.

Ni kweli marais wanne waliomtangulia, Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, waliifanya kazi hii ya mzegazega. Lakini tukitaka tusitake lazima tukubali kwamba zama zimebadilika na zitaendelea kubadilika.

Tangu kuja mfumo wa vyama vingi kazi ya mzegazega kwa Rais wa nchi hapa kwetu imekuwa na changamoto nyingi.

Hii ni pamoja na madai ya kuwapo mgongano wa masilahi na mara nyingine imekuwa vigumu katika baadhi ya shughuli anazofanya Rais kuelewa anafanya hivyo kama kiongozi wa nchi au wa chama chake.

Wapo waliowahi kuuliza na ni haki yao kufanya hivyo, kuwa pale Rais anapovaa sare za CCM na kunadi sera za chama hicho ni sawa kumpa heshima anazostahili kiongozi wa nchi au ni kumwona kama kiongozi mwingine wa chama cha siasa?

Vilevile, pamekuwapo na hisia zenye nguvu kwamba kutokana na Rais kuvaa kofia mbili, moja ya uongozi wa nchi na nyingne ya CCM, hata katika uendeshaji wake wa shughuli za Serikali huweka mbele masilahi ya chama hake badala ya Taifa.

Hili ni suala la mjadala, lakini tukumbuke kuwa wahenga ambao tumekuwa tukipenda kuchota hekima na busara zao walieleza: “Lisemwalo lipo, kama halipo linakuja”. Siyo vyema na si vizuri kupuuza maneno haya yaliyojaa hekima na busara.

Sasa Rais Magufuli anakabidhiwa kofia ya pili (sijui ipi ni kubwa kwa kichwa chake), lakini ninachokiona ni kuwa amebeba mzegazega.

Suala ni je, atawaweza kuwa na ustadi wa kubeba majukumu hayo mawili kwa usawa na wakati wote kuwa na imani naye kwamba anaweka mbele masilahi ya Taifa kuliko yale ya CCM?

Wapo wanaoweza kusema tusubiri tuone na kuremba hoja yao kwa kutumia msemo maarufu wa Kiwahili “Tusiandike mate na wino upo”. Lakini hivyo kweli ipo haja ya kubahatisha na je, mambo yakienda kombo na wananchi wengi kumwona kwanza kama kiongozi wa CCM na baadaye Rais wa nchi tumlaumu nani?

Mzegamzega uingie kwenye Katiba

Hili ni suala linalofaa kufanyiwa tafakuri ya kina na ikiwezekana kuwekwa bayana katika Katiba yetu kwamba anayeliongoza Taifa basi aonekane kwa uwazi zaidi kama kiongozi wa nchi na siyo wa chama cha siasa.

Ni kweli mtindo huu wa viongozi wa nchi kuwa wabeba mzegamzega upo katika nchi nyingi, hasa zile zinazoitwa za Kikomunisti na Kijamaa. Siyo vibaya kuiga tunachokiona katika nchi hizo. Ingawa Waswahili wanasema “Kiingiacho mjini si haramu”, lakini uzoefu umetuonyesha siyo kila kiingiacho mjini ni halali. Mfano ni matumizi ya dawa za kulevya, kuongezeka kwa vitendo vya rushwa na ufisadi, ufuska na mengine mengi.

Upo umuhimu wa kulitafakari kwa umakini suala hili na kuliangalia kwa jicho la uzalendo na siyo utashi wa kisiasa wa CCM au wa chama chochote kingine cha siasa.

Tunachotakiwa ni kupima je, tunachokiiga ni kizuri au kibaya, kuangalia faida na hasara zake na zaidi kwa kiasi gani kitaimarisha demokrasia na mfumo wa utawala bora, haki na sheria.

Sura ya vyama vingi ionekane

Tumekubali kuwa na mageuzi ya kutoka kwenye mfumo wa chama kimoja kwenda kenye mfumo wa vyama vingi na ili tufanikiwe katika safari yetu lazima suala hili lionekane kwa uwazi katika uongozi wa nchi yetu.

Tutafika tunakotaka kwenda kama tutaamua kufuata njia sahihi na tutaharibikiwa kama tutaweka mbele utashi wa vyama badala ya uzalendo.

Mwandishi ni mwanahabari mkongwe na mchambuzi wa masuala la siasa na jamii, anapatikana kwa barua pepe: [email protected] na [email protected]